Tuesday, March 20, 2012

Lowassa awakaanga vigogo Serikali ya JK


ASEMA WAMEKWAMA KUMALIZA TATIZO LA AJIRA, AWATAKA MAASKOFU WAINUSURU, RUWAICHI AIPONDA KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI
Juma Mtanda, Ifakara
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema anashangazwa na Serikali kuendelea kulifumbia macho tatizo la ajira kwa vijana na kuwaomba maaskofu wasaidie kulimaliza akisema hilo ni bomu linalosubiri kulipuka.

Lowassa alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu zake kwenye sherehe za uzinduzi wa jimbo jipya la Kanisa Katoliki la Ifakara zilizofanyika katika Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Edward, Ifakara.

Alisema viongozi wa juu serikalini wameshindwa kulitatua na kulifumbia macho tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana hivyo kuwaomba maaskofu waliangalie kundi hilo ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi.

“Suala la ajira kwa vijana hakuna kiongozi anayelishughulikia ipasavyo ndani ya Serikali, hivyo niwaombe maaskofu nchini walione hili. Nawaomba katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la tatizo la ajira kwa vijana,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Kanisa Katoliki limekuwa likisaidia sana katika sekta ya elimu na afya kwa hiyo sasa waelekeze nguvu hizo katika kusaidia ajira kwa vijana. Wengi wanaomaliza elimu ya sekondari na vyuo wanakabiliwa na tatizo kubwa la ajira. Hili kama tunavyosema ni bomu linalosubiri kulipuka, sasa naliomba Kanisa lisaidie juhudi za Serikali kutatua tatizo hili,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Ruwaichi na mgomo
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Dadeus Ruwaichi alisema mgomo wa madaktari nchini umedhihirisha udhaifu wa Serikali katika kushughulikia migogoro na kusema ni aibu kwa Tanzania.

“Watu wengi wamekufa katika mgomo ule na hii imeonyesha Tanzania ni taifa lisilo na dira,” alisema Askofu Ruwaichi huku Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda ambaye ni Mbunge wa Ulanga Mashariki akimsikiliza.

“Hakuna hata uharaka uliochukuliwa kushughulikia mgomo ule na hii ni kwamba nchi yetu sasa imefikia pabaya kwani inaonekana imeshindwa kushughulikia matatizo,” alisisitiza.

Katika salamu hizo kwa Askofu mpya wa jimbo jipya la Ifakara, Salutaris Libena, Askofu Ruwaichi alisema kanisa litaendelea kupiga vita umasikini.

Alimtaka askofu huyo kutoogopa kukemea maovu yanayofanywa na viongozi wa Serikali na kusababisha pengo kati ya wenye nacho na wasionacho.

Mwinyi asisitiza upendo
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimtaka Askofu Libena kutumia nafasi yake kuleta amani na upendo miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali.

Mwinyi alisema uaskofu ni daraja kubwa linalofanana na nafasi ya uwaziri katika Serikali hivyo waumini wa dini ya Kikristo katika jimbo jipya la Ifakara wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kiongozi huyo aliyesimikwa kutumikia dini hiyo na Watanzania kwa ujumla.

“Nafasi ya uaskofu haifungamani na dini wala kabila kwani daraja hilo limejaa roho ya huruma na upendo hivyo jamii ya jimbo la Ifakara ni wakati wa kutoa ushirikiano ili kumpa nafasi mhashamu Askofu Salutari Libena ya kuwahudumia katika nyanja mbalimbali za elimu, afya na tabia njema,” alisema Mwinyi.

Kadinali Pengo
Katika mahubiri yake, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alisema uamuzi wa kugawanya Jimbo la Mahenge ni mchakato wa muda mrefu uliotokana na ukubwa wa Jimbo la Mahenge.

“Mchakato huo uliridhiwa na Papa Benedict wa 16 Januari 14, 2012 kwa kukubali Ifakara kuwa jimbo jipya na makao makuu katika Kanisa la St Andrew lililopo mji mdogo wa Ifakara.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na taasisi wakiwemo maaskofu wa majimbo 34.

Wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na Kilombero, Francis Miti.

No comments:

Post a Comment