Wednesday, March 21, 2012

Kanisa Katoliki lamshukia Wassira kuhusu Dk Slaa


LASEMA KAMA ANAO USHAHIDI WA WIZI WA FEDHA ZA PAPA AUTOE, WANASIASA WANAOCHAFUA WENZAO WAMEFILISIKA, NEC YAVIONYA CCM, CHADEMA
Na Waandishi Wetu
KANISA Katoliki nchini limemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano wa Jamii), Stephen Wassira kutoa ushahidi kuthibitisha kama Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alifukuzwa upadre baada ya kuiba fedha za ujio wa Papa John Paul II, alipokuja nchini mwaka 1991.Akizungumza kwa simu jana, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), Yuda Thadeus Ruwaichi alimtaka Wassira athibitishe tuhuma zake akisema kanisa hilo halijawahi kumtuhumu  Dk Slaa kwa tuhuma za wizi.

Akizungumza katika kampeni za CCM Jimbo la Arumeru Machi 19, mwaka huu, Wassira alimtupia kombora Dk Slaa akidai si mwaminifu kwa kuwa alifukuzwa ukasisi wa kanisa hilo baada ya kufanya ufisadi kwenye fedha za mapokezi ya Papa huyo ambaye sasa ni marehemu.

Hata hivyo, Wassira jana alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Askofu Ruwaichi alijibu kwa kifupi: “Mimi nilishazungumza na yakaandikwa kwenye vyombo vya habari, hii leo siyo habari.”
Ruwaichi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza alisema madai hayo ya Wassira hayana msingi.

“Kanisa halijawahi kumshutumu Dk Slaa kuhusu madai hayo (ya Wassira). Kama Wassira ameyatoa kwenye mkutano wa hadhara, njia sahihi ya kupata ukweli ni yeye kutupa ushahidi wa vielelezo kuthibitisha madai yake,” alisema Ruwaichi.

Askofu Ruwaichi amewaonya wanasiasa wanaofanya kampeni za kuchafuana akiwataka waache na waanze kufanya siasa za kistaarabu.

“Ukiona mwanasiasa anakurupuka na kuanza kumchafua mwenzake ujue amefilisika, vitendo hivyo vinaonyesha udhaifu kwa nchi katika nyanja za siasa,” alisema.

Askofu Ruwaichi alisema wanasiasa waliokomaa hawapaswi kufanya kampeni za kuchafuana... “Watajishughulisha katika kujadili hoja zinazozingatia mahitaji ya jamii. Kitendo cha wanasiasa wetu kufanya kampeni za kuchafuana kinaonyesha dhahiri kuwa bado tuko dhaifu katika siasa na hatuna vipaumbele.”

Askofu Ruwaichi aliwataka wanasiasa hao kuachana na kampeni chafu na badala yake wajikite katika kujadili hoja zinazotoa vipaumbele katika matatizo yanayoikabili jamii na namna ya kuyatatua ili kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi bora.

Kauli hiyo ya Askofu Ruwaichi, imekuja siku chache baada ya Dk Slaa kuzungumza katika mkutano wa hadhara kwenye kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru na kusema Wassira ni mwongo na hajui asemalo.

“Kama tangu mwaka 1991 nipo, basi kitendo cha Serikali kushindwa kunifungulia mashtaka ya wizi wa hizo fedha basi ni Serikali dhaifu na ijiuzulu,” alisema Dk Slaa.

NEC yavionya CCM, Chadema

Katika hatua nyingine, Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeonya vyama vya CCM na Chadema kuacha kampeni chafu baada ya kuthibitika kuwa vimekiuka sheria na maadili ya uchaguzi kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinafanywa na wafuasi wao.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema vyama hivyo vimeandikiwa barua hizo baada ya kukamilika kwa kikao cha kamati ya maadili ambacho kilipokea barua za malalamiko matano kuhusu mwenendo usioridhisha katika kampeni.

Kagenzi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema CCM kimepewa barua ya onyo kutokana kitendo cha wafuasi wake kuchana picha na mgombea wa ubunge wa Chadema, Joshua Nassari siku ya uzinduzi wa kampeni zake katika Uwanja wa Ngaresero.

Mwenyekiti huyo alisema Chadema nacho kimepewa onyo kutokana na wafuasi wake kuwakashifu viongozi wa CCM katika eneo la Meru Garden ambako viongozi hao na mgombea wao, Sioi Sumari walisimama kupata chakula.

Alisema malalamiko yaliyojadiliwa ni ya Chadema na CCM na kwamba vyama hivyo viwili vinatuhumiana kwa ukiukwaji wa sheria na maadili ya uchaguzi.

Alisema Chadema katika barua yao ya Machi 12 mwaka huu, kililalamikia wafuasi wa CCM kung’oa picha za mgombea wao wakati wa uzinduzi wa kampeni zao ambazo zilikuwa zimebandikwa katika kontena lilipo jirani na uwanja kulipozinduliwa kampeni.

Alisema malalamiko mengine ya Chadema yaliwasilishwa Machi 14, mwaka huu kuhusu kukashifiwa kwa mgombea wao na CCM kwa matusi mbalimbali na Machi 19 walilalamika kutekwa kwa Mwenyekiti wao wa Kitongoji cha Magadirisho, Nuru Maeda na wafuasi wa CCM na kupigwa.

Kwa upande wa CCM, Kagenzi alisema kiliwasilisha barua ya malalamiko kwamba Machi 12 wafuasi wa Chadema walikaa njia panda kutoka eneo palipofanyika uzinduzi wa kampeni za CCM na kuanza kuwazomea viongozi wa chama hicho na kung’oa bendera za chama hicho kwenye magari na kuonyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema.

Alisema pia Machi 18 wafuasi wa Chadema waliufanyia vurugu
msafara wa mgombea ubunge wa CCM, katika eneo la Meru Garden na kushambulia magari kwa mawe na gari moja la CCM lilivunjwa vioo.

Kagenzi alisema ni busara vyama vyenye wagombea katika
uchaguzi huo kufanya kampeni kwa kunadi sera za kutoa ahadi wagombea wao wakichaguliwa watafanya nini, badala ya kutoa matusi wakati wote na kashfa dhidi ya wengine.

Pia amepiga marufuku machapisho yote kusambazwa katika jimbo hilo bila ridhaa yake... “Napenda kukumbusha kuwa ni marufuku kwa chama au mtu kusambaza machapisho katika kampeni bila kuwasilisha chapisho hilo ofisi yake ili yaidhinishwe.”

Tamko hilo limekuja wakati Chadema wakiwa wanalalamikia kusambazwa kwa nyaraka za uchochezi na kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk Slaa wamekuwa wakilalamikia polisi kusambaza vipeperushi kwenye mikutano yake ambavyo alisema vinalenga kuwatisha raia.

CCM wamgomea msimamizi
Akizungumza na gazeti Dada la The Citizen jana, Mratibu wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema chama chake hakiwezi kuacha kujibu mapigo ya Chadema na kuongeza kuwa kitaacha kufanya hivyo endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakiandikia Chadema kukanusha kashfa kilizozitoa dhidi ya mgombea wa CCM Sioi.

“Tunachokifanya sisi ni kuwaeleza wananchi ukweli dhidi ya wapinzani wetu hatutukani watu hapa… hatuwezi kubadili staili hii ya kampeni mpaka tume iwaambie Chadema wafute matusi hadharani dhidi ya mgombea wetu,” alisema Nchemba.

Alisema tume inatakiwa kutenda haki kwa vyama vyote huku pia akiwataka wapinzani kutolia katika harakati za mashambulizi ambazo wamezianzisha wenyewe.

Meneja wa Kampeni wa Chadema, Vincent Nyerere alisema chama chake hakijapokea barua yoyote kutoka tume huku akionya kwamba hata kama kutakuwa na barua hiyo, basi walengwa wake ni CCM na siyo chama chake.

Alisema amekuwa mmoja kati ya watu waliokashifiwa na viongozi wa CCM huku akiitaka Tume kuacha upendeleo na badala yake itoe adhabu stahiki kwa chama hicho tawala.

“Hebu tuwaache Sioi na Nassari wapambane katika majukwaa na sio mzee Wassira, Mkapa na Ole Sendeka kutushambulia badala ya kutangaza sera za chama chao, sisi tunaendelea na kampeni za kistaarabu,” alisema Nyerere.
Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang'oro Dar, Neville Meena na Mussa Juma, Arumeru.

No comments:

Post a Comment