Monday, June 11, 2012

Dk. Mgimwa ahaidi kutanzua kero ya kodi

WAZIRI wa Fedha na Uchumi wa Tanzania Bara, Dk. William Mgimwa, amesema suala la wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapopeleka bidhaa Tanzania bara litapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho.
Kauli hiyo alitoa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa.
Alisema kodi ni suala linalogusa maisha ya watu, hivyo manung’uniko ya wafanyabiashara kutozwa mara mbili yanapaswa kushughulikiwa.
Dk. Mgimwa alisema kuwa katika utaratibu wa kawaida wa kisheria duniani kote, ukilipia kodi upande mmoja wa Muungano hutakiwi kulipia tena upande mwingine, na kwamba si utaratibu wa kawaida, hivyo amewaagiza TRA kungalia juu ya hali hiyo.
Alisema kuwa baada ya kuangalia upya mfumo uliopo na kubaini dosari, watakaa na kujadiliana ili kutoa mapendekezo kwa viongozi na matatizo yaliyopo yaweze kupata ufumbuzi.
“Uamuzi wa kuupitia upya mfumo huo utatekelezwa na wizara zinazosimamia mambo ya fedha na sera, kwa sababu ndio wanaoguswa na masuala ya kodi kwa maana ya utendaji,” alisema.
Dk. Mgimwa aliongeza kuwa, lengo la kuupitia upya mfumo huo ni kupata muafaka juu ya mambo yanayolalamikiwa katika mfumo wa sasa wa kodi.
Akizungumzia suala la Zanzibar kulipwa asilimia 4.5 ya hisa zake katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Mgimwa alisema suala hilo pia linahitaji mabadiliko.
Alisema mabadiliko hayo yanaweza kufanyika baada ya kuangalia vigezo vilivyotumika kuweka kiwango hicho kama bado vina mantiki.
Dk. Mgimwa alisema lengo la serikali ni kupata mfumo unaotumika katika aina zote za mifumo ya muungano ili kupata utaratibu usiolalamikiwa na walipa kodi na wadau wa pande mbili za Muungano.
Alisema utekelezaji wa kazi hiyo pia utalenga kuijengea Tanzania mazingira bora ya kuingia katika ushirikiano wa masuala ya fedha na soko la pamoja la nchi wanachama wa Afrika Mshariki (EAC).

No comments:

Post a Comment