Thursday, June 14, 2012

Zanzibar yaongeza kodi ya mafuta, bandari


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza Bajeti yake kwa mwaka 2012/13 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza kodi katika maeneo manane ikiwamo mafuta, ada ya bandari na ushuru wa stempu huku ikiwa na maeneo sita ya kipaumbele.

Maeneo hayo ya vipaumbele ni afya, ajira kwa vijana, ustawi wa wazee, elimu, kuimarisha uchumi na kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

SMZ katika bajeti yake hiyo, imepanga kutumia Sh307.8 bilioni kwa kazi za kawaida na Sh341.1bilioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo huku makusanyo yakitarajiwa kuwa 648.9 bilioni.

Akiwasilisha Bajeti hiyo jana kwenye Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo), Omar Yussuf Mzee alisema kwa kuzingatia dhamira ya Serikali katika kukuza mpango wa maendeleo, imependekeza marekebisho ya viwango vya tozo ya kodi.

Mzee alitaja mabadiliko hayo kwamba yamegusa  Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 6 ya mwaka 1996, Sheria ya Kodi za Hoteli namba 1 ya mwaka 1995, Sheria ya Ada za Bandari namba 2 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ushuru wa Petroli namba 7 ya mwaka 2001.

Sheria nyingine ni ile ya Usimamizi na Utaratibu wa kodi namba 7 ya mwaka 2009, Sheria ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) namba 4 ya mwaka 1998, Sheria ya Bodi ya Mapato Zanzibar namba 7 ya mwaka 1996 na Sheria ya Mafunzo ya Amali namba 8, ya mwaka 2006.

Waziri huyo alisema kutokana na mabadiliko hayo, ada ya bandari imependekezwa kuongezwa kutoka Sh1,000 ya sasa hadi Sh2,000 kwa abiria wanaosafiri kati ya Zanzibar na Tanzania bara.
Mzee alisema abiria wanaosafiri kati ya Unguja na Pemba watatozwa Sh1,000.

Eneo jingine ni kuongeza ushuru wa mafuta kwa Sh50 kwa lita inayoingia visiwani humo kwa mafuta ya petroli na dizeli tu, hatua ambayo alisema inatarajiwa kuiingizia SMZ mapato ya Sh3.3bilioni.
Akizungumzia ongezeko la ushuru wa stempu, waziri huyo alisema Serikali inapendekeza kuongeza kutoka asilimia moja na nusu ya sasa hadi asilimia tatu, hatua ambayo itaongeza mapato kwa Serikali ya Sh2.10 bilioni.

Waziri Mzee alitaja eneo jingine ambalo limefanyiwa marekebisho kwamba ni Sheria ya Usafiri Barabarani, ambako Serikali imependekeza kurekebisha kiwango cha leseni za njia ili kiendane na uzito gari au ukubwa wa injini yake.

Alisema kiwango cha sasa cha ada ya leseni ya njia Sh24,000 kwa gari kwa mwaka, hakizingatii matumizi ya njia tofauti za gari.

Waziri huyo alisema kutokana hali hiyo, Serikali inapendekeza tozo la Sh15,000 kwa kila gari kwa mwaka na Sh3,000 kwa chombo cha moto cha magurudumu mawili au matatu.
Alisema hiyo inatokana na ongezeko la idadi ya magari nchini kila mwaka na hivyo, kuathiri mazingira kutokana na moshi unaotokana na magari hayo.

Marekebisho mengine ni yale ya viwango vya ada za huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali na taasisi zake baada ya kubainika kuwa zimepitwa na wakati.

Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha, Serikali inakusudia kufanya marekebisho kiwango cha kodi huduma za mahoteli, migahawa na kutembeza wageni.

Alisema Serikali imependekeza kuongeza kiwango cha kodi kwa hoteli, migahawa na watembeza wageni wasiosajiliwa VAT kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 18.

Ukuaji uchumi
Kuhusu ukuaji wa uchumi, Mzee alisema uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.5 kutoka  asilimia 6.8 mwaka 2011.

Alisema mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 8.7 kwa mwaka huo wa 2012  ukilinganishwa na mwaka jana, ambao ulikuwa ni asilimia 14.7.

Alisema uchumi wa Zanzibar kwa mwaka huu unatarajiwa kuimarika zaidi kutokana na mipango mbalimbali ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato, kutoka vyanzo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment