Friday, June 15, 2012

... Mbowe, Lipumba, Mbatia walia


WENYEVITI wa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF wameiponda Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakisema imeongeza mzigo kwa walipa kodi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo jana, wenyeviti hao walisema hakuna matumaini kwa Watanzania kupitia Bajeti hiyo kwani fedha nyingi zimerundikwa kuwanufaisha wachache huku umma ukiambulia patupu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Hakuna mkataba wa makusudi wa kupunguza matumizi ya Serikali, ahadi yake ya kupunguza matumizi kwa kupunguza posho zisizo na tija na matumizi mengine haikutekelezwa.”
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema ameshangazwa na kutokuwapo kwa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na badala yake fedha nyingi kurundikwa katika matumizi ya kawaida ya Serikali.
“Mfumo wa kodi kama mlivyosikia ni mbaya kabisa, hakuna kinachoashiria kwamba mkulima wa kawaida atapunguziwa mzigo na badala yake wanaendelea kuwanufaisha wafanyabiashara wa vyakula kwa kuwaruhusu kuagiza vyakula nje bila kodi, hiki naweza kusema ni kichekesho,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Hakuna ubunifu kwenye kupanua wigo wa kodi, tungeweza kusikia katika construction (sekta ya ujenzi) ambayo inakua haraka na inachukua asilimia 18 ya Pato la Taifa kwamba tungetoza kodi huko, lakini badala yake ni yaleyale ya siku zote, kodi kwenye sigara, vinywaji na bia.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema matatizo makubwa katika bajeti hiyo ni kutengwa kwa fedha kidogo za maendeleo na kwamba kinachoshangaza ni Serikali kushindwa hata kugharimia matumizi ya kawaida.
“Utawala unagharimiwa kwa Sh10 trilioni hali uwezo wa kukusanya mapato ya ndani ni Sh8 trilioni, hii inamaanisha kwamba Serikali yetu pia inatumia fedha za wahisani kugharimia matumizi ya kawaida,” alisema Profesa Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema Serikali lazima ijifunze kubadilika kwani kilichotangazwa jana kwenye Bajeti yake ni marudio ya miaka yote.
“Huwezi kuchukua fedha zote ukaurundikia utawala halafu ukawaacha wananchi bila kitu, hicho ndicho tulichokiona leo, Sh10 trilioni ni kwa ajili ya mishahara na watumishi na matumizi ya kawaida, maendeleo ambako ndiko wananchi waliko kumeachwa tena kutegemea fedha za wafadhili,” alisema Mbatia.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu alisema, Bajeti hiyo haitatekelezeka... “Mwaka jana wamekuja na Bajeti kama hii ya kutegemea fedha za wafadhili, zaidi ya asilimia 40 ya fedha zilizotengwa hazikupatikana na leo wanakuja na bajeti ya aina ileile,” alisema Lissu.
Mbunge wa Ngorongoro (CCM) Saning’o Ole Telele, alisema Bajeti hiyo ni pigo kubwa kwa wafugaji kwani wameshindwa kutengewa fedha kwa ajili ya kuboresha ufugaji hasa wale ambao wanahamahama.
Hoja hiyo ya Telele, iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili ambaye alisema  Bajeti ya mwaka huu, badala ya kuongeza fedha kusaidia wafugaji hasa wa asili ambao wanatangatanga, imeendelea kupunguza fedha za wizara hiyo.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alisema Bajeti hiyo kama zilivyo nyingine,  imeendelea kujikita katika kuongeza kodi katika bidhaa zilezile kila mwaka.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema Bajeti hiyo ni nzuri akipongeza mkakati wa ukarabati mkubwa wa Reli ya Kati.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso alisema, Bajeti ya mwaka 2012/13 kama alivyoisikiliza  imeendelea kukosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na hivyo kuongeza makusanyo ya ndani.

Wadau wengine
Rais Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema fedha zilizotengwa kwenye Wizara ya Elimu ni ndogo kiasi cha kutoweza kukidhi mahitaji ya walimu na kueleza kuwa hiyo itaendeleza migogoro.
“Kwa kweli ni kiasi kidogo sana, tena imetuvunja nguvu, kwa sababu tulitegemea wafanyakazi tutapewa kipaumbele kwenye Bajeti, lakini kilichotokea ni tofauti kabisa,” alisema Mukoba.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema Bajeti ya mwaka huu imeendelea kuwa yenye manufaa kwa viongozi wa Serikali na kuwaumiza wananchi wa hali ya chini.
Alisema haiwezekani Bajeti ya mwaka 2006/7 ikawa zaidi ya Sh4 trilioni halafu ya mwaka 2012/13 ikafika Sh15.2 trilioni na bado ikawa ina manufaa kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellein Kijo-Bisimba alisema Bajeti  imeegemea upande mmoja wa Serikali badala ya kuwa upande wa wananchi.
Dk Bisimba alisema haiwezekani kodi ya huduma ya simu ikapandishwa na kulingana na nchi za Afrika Mashariki bila kujali kwamba itawaumiza watumiaji wa hali ya chini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya alisema Bajeti haina kipaumbele kwa huduma za kijamii na imejikita kwenye masuala ya anasa.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema Bajeti ya mwaka huu haina tofauti na zilizowahi kutolewa.
Alisema kutokana na ukweli kuwa Bajeti ya mwaka jana haikuwa na ufanisi, ilitegemewa mwaka huu kusikia maelezo ya kina yakifafanua sababu za kutofanya vizuri kwa Bajeti ya mwaka jana, jambo ambalo halikufanyika.
Alisema hata ongezeko la trilioni mbili  kwa Bajeti ya 2012/13  ikilinganishwa na iliyopita, siyo jambo geni kwani limekuwa likifanyika mara kadhaa lakini ufanisi wake hauonekani.
Nyongeza na Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Ibrahim Yamola, Dar; Salim Mohammed, Tanga; Joseph Lyimo, Manyara na Peter Saramba, Arusha.

No comments:

Post a Comment