Monday, June 25, 2012
Mgomo wa madaktari waanza rasmi
HUDUMA ZA KAWAIDA ZAZOROTA
Waandishi Wetu, Dar na Mikoani
MADAKTARI nchini wameanza mgomo katika baadhi ya hospitali nchini baada ya Serikali kushindwa kutekeleza madai yao waliyowasilisha katika Kamati ya Majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Mgomo huo umetangazwa na Jumuiya ya Madaktari nchini huku ikifafanua kwamba kati ya madai kumi waliyotaka yatekelezwe na Serikali, hakuna hata moja lililofanyiwa kazi. Hata hivyo, jana madaktari hao ambao walikaa vikao vya majadiliano na Serikali kwa siku 90 baada ya kusitisha mgomo wao wa pili, wamesema katika madai yao kumi, hakuna hata moja lililotekelezwa na Serikali. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Stephen Ulimboka jana aliwaeleza waandishi wa habari kwamba ili warejee kazini, Serikali inatakiwa kutekeleza madai yao yote na kusisitiza kwamba dai lao la kwanza ni kuitaka Serikali kuboresha huduma za msingi kwa wagonjwa.
“Mgomo umeanza leo na hauna kikomo, lengo ni kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yetu, hata zile huduma za dharura nazo kuanzia kesho (leo) zinaweza kusitishwa,” alisema Dk Ulimboka. Wakati Ulimboka akieleza hayo, huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (Moi) ilikuwa ikitolewa kwa kusuasua huku baadhi ya wafanyakazi wakisisitiza kuwa mgomo huo upo.
Licha ya wafanyakazi hao kukiri kuwa siku za mwisho wa wiki idadi ya wagonjwa katika hospitali hizo huwa ndogo, lakini walisisitiza kuwapo kwa mgomo huo na kufafanua kuwa kwa mtu mgeni katika eneo hilo si rahisi kutambua hali hiyo. Mwananchi Jumapili lilifika katika hospitali hiyo na kukuta huduma zikitolewa ‘kiaina’ huku baadhi ya wagonjwa wakieleza kwamba zimezorota, sio kama siku zilizopita.
Tamko la Jumuiya Akieleza kwa kina sababu za mgomo huo, Dk Ulimboka alisema katika madai waliyoyawasilisha, hakuna hata moja lililotekelezwa na kufafanua kwamba Serikali imeongeza dai ambalo wao hawakuliwasilisha. Madai hayo ni pamoja na kupandishwa kwa ongezeko la mishahara, posho ya kuitwa kazini, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, bima ya afya, nyumba za kuishi, kukopeshwa magari kwa ajili ya usafiri, kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi kwa kupeleka vifaa vya kazi, dawa na kuboresha miundombinu.
“Serikali imesema imerekebisha viwango vinavyotumika kulipa posho ya uchunguzi wa maiti kwa Sh 100,000 kwa uchunguzi wa madaktari na Sh50,000 kwa watumishi wengine, lakini hili halikuwa dai letu!” alisema Dk Ulimboka. Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi aliwatahadharisha madaktari hao kuacha mgomo, akieleza kuwa ni batili na ni kinyume cha viapo vyao vya kazi. Dk Mwinyi aliainisha mambo 10 ambayo madaktari walikuwa wamepanga kutekelezewa na kusema kuwa kwa sehemu, yametekelezwa na baadhi ya mambo yaliyobakia wanaweza kuyazungumza.
Mwanza
Madaktari zaidi ya 200 waliopo katika Hosptali ya Rufaa ya Bugando jana walianza mgomo rasmi baada ya Serikali kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu madai yao mbalimbali yaliyosababisha madaktari hao kugoma mapema mwaka huu. Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Mwakilishi wa Kamati ndogo ya kufuatilia madai madaktari hao, Dk Richard Kirita alisema kwamba madaktari wa kada zote katika hospitali hiyo wapo kwenye mgomo isipokuwa baadhi ya madaktari bingwa pamoja na wakuu wa idara.
“Kwa kuwa leo sio siku ya kazi unaweza kudhani hakuna mgomo, lakini njoo Jumatatu (kesho) ndo utapata picha halisi ya mgomo kwa sababu wagonjwa watakuwa wengi, lakini hakutakuwa na huduma,”alisema
Moshi
Hali ya utendaji wa madaktari mkoani Kilimanjaro imeonekana ya kusuasua huku baadhi ya madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC wakisema hawaingii kazini na wengine wakisema bado wanasikilizia.
Katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, madaktari waliokuwa zamu walisema kwa leo huwezi kujua aliyeko kwenye mgomo na ambaye hayupo, kwani wengi hawako kazini leo hadi kesho. B
aadhi ya wagonjwa waliolazwa Hospitali ya KCMC katika wodi ya wanawake, walisema kuwa walitangaziwa kuwa kutakuwa na mgomo wa madaktari na kila mmoja aangalie cha kufanya na kuwa walifika wodini hapo asubuhi na hawakuzungumza na mgonjwa na kutoka. Wagonjwa hao wamesema Ijumaa jioni wagonjwa wengi waliruhusiwa kuondoka hata kama hali zao hazijatengemaa ambapo walisema wanahofia afya zao kama madaktari watatekeleza msimamo wao. Mbeya Katika Hospitali ya Rufaa Mbeya madaktari 10 kati ya 80 ndiyo waliokubali jana kuendelea na huduma ya kutibu wagonjwa ambapo wengine wameanza mgomo rasmi.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eliuter Samky amethibitisha kuwapo na hali ya mgomo na kwamba ana uhakika wa madaktari 10 waliopo zamu kuendelea kazi.
Awali Mwandishi wa gazeti hili alipofika katika hospitali hiyo hakukuta daktari yeyote na ofisi za utawala zikiwa zimefungwa huku katika eneo la mapokezi likiwa na wagonjwa ambao wamekaa wakisubiria kupata huduma. Katika kitengo cha wazazi Meta wanawake wanaokwenda kupata huduma wamesema wameingiwa na hofu kubwa kwa kukosa huduma hiyo baada ya kuona matangazo yanayosema hakuna mgojwa atakayepatiwa matibabu.
Wakizungumza hospitalini hapo wanawake hao ambao hawakutaka kuandikwa majina yao, walisema kuwa mbali na kuona tangazo hilo lakini pia waliambiwa na baadhi ya madaktari kuwa ni bora wakaenda sehemu nyingine kwa ajili ya matibabu kwa kile kilichoelezwa kuwa kuwa na wao wapo katika mgomo huo hivyo hakuta kuwa na huduma yeyote kwa mgonjwa.
Arusha
Hali ya mgomo wa madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, haikuonekana jana asubuhi ingawa katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya madaktari na manesi hawakufika wodimi kuwaona wagonjwa kama wananvyofanya siku nyingine.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo,Dk Mlay alipoulizwa na gazeti hili alisema hali hiyo isihusishwe na mgomo uliotangazwa na chama cha madaktari kwa kuwa kimetona na sababu kwamba leo na kesho ni siku za mapumziko .
Baadhi ya wagonjwa na ndugu wanaowauguza walihojiwa na gazeti hili walionyeshwa kushangazwa na hali ya madaktari na manesi kushindwa kuwatembelea leo katika wodi zao kinyume na siku zote.
Mganga Mkuu wa hospitali alisema kwamba hospitalini kwake hakuna mgomo wowote wa madaktari kwa kuwa wanafanya kazi kama kawaida na wala hawatambui suala la mgomo wa madaktari uliotangazwa na Chama cha Madaktari nchini(MAT).
Tanga Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo pamoja hospitali nyingine za wilayani jana ziliendelea na huduma ya kutoa matibabu kwa wagonjwa kama kawaida. Katika Hospitali ya Bombo ambayo ni ya Mkoa wa Tanga, Mwandishi wa habari hizi jana alikuta madaktari pamoja na wauguzi waliokuwa zamu wakiendelea na kutoa matibabu kwa wagonjwa waliolazwa pamoja na wale wa kutoka nje.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili madaktari wa Hospitali ya Bombo walisema wameshindwa kufanya mgomo kwa kuwa hawana taarifa za kuwataka kufanya hivyo bali wamekuwa wakisikia na kusoma kupitia vyombo vya habari.
Haruna Juma ambaye ni mkazi wa Barabara ya 10 Jijini Tanga, aliwashukuru madaktari wa Hospitali ya Bombo kwa kutogoma kwa kuwa mdogo wake anayesumbuliwa na Apendex alipangiwa kufanyiwa upasuaji jana ambapo waganga walimfanyia kama kawaida.
Waziri
Serikali imesema kuwa itaendelea na msimamo wake ilioutoa bungeni mjini Dodoma wa kuwataka madaktari nchini kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wakati ambapo madai yao ya msingi yakiwa yanashughulikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro jana baada ya kufanya ziara yake katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, alisema kuwa kimsingi yako mambo ambayo katika mazungumzo na madaktari hao walikubaliana lakini pia yako mambo ambayo hawakukubalina.
Dk Rashid alisema kuwa mambo ambayo walikubalina na madaktari hao yanaendelea kushughulikiwa lakini mambo ambayo walishindwa kukubalina katika baraza la usuluhishi madaktari hao walikimbilia mahakamani ili kutafuta suluhu.
“Na sisi tunasubiri maamuzi ya mahakama kwa hivyo kitendo cha wao kugoma kinakwenda kinyume na sheria kwa kuwa jambo hilo bado halijapatiwa ufumbuzi na mahakama,” alisisitiza.
Katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro hakukuwa na dalili zozote za madaktari na wauguzi kugoma, huduma za matibabu kwa wagonjwa zilikuwa zikiendelea kama kawaida huku baadhi ya wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo wakidai kutokuwa tayari kuingia katika mgomo huo.
Amana, Temeke Katika hospitali ya Amana na Temeke za jijini Dar es Salaam wameendelea kutoa huduma kama kawaida, isipokuwa Hospitali ya Mwananyamala ambayo kulikuwa na madaktari na waguzi wachache. Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Meshack Shemwela aliiambia Mwananchi Jumapili jana kwamba huduma ya afya zinaendelea kutolewa kama kawaida na kwamba wanafanya tathmini ilikutambua kama kuna madaktari waliogoma.
Akizungumzia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick alisema kuanzia jana saa 6 usiku walifanya uchunguzi na kubaini kwamba kuna watu waliokuwa wanapita katika kila hosptali kuhamasisha kufanyika lakini madaktari hawajagoma.
Imeandaliwa na Rehema Matowo,Moshi, Venance George, Morogoro, Burhani Yakub,Tanga, Brandy Nelson, Godfrey Kahango,Mbeya, Moses Mashalla,Arusha,Sheilla Sezzy,Mwanza Aidan Mhando, Ibrahim Yamola, Geofrey Nyang'oro na Fidelis Butahe,Fidelis Butahe na Geofrey Nyang’oro
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment