Thursday, May 26, 2011

Lissu na wenzake marufuku Nyamongo

Maiti wazikwa, wananchi wataka kurejesha majeneza polisi



 
















MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, na wenzake saba ambao juzi walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime na kusomewa mashtaka matatu ya kuingia eneo la hospitali bila kibali, kufanya mkutano na kuzuia watu kufanya kazi, wamepata dhamana lakini wamezuiwa kutembelea maeneo ya Nyamongo hadi kesi inayowakabili itakapokwisha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Yusto Roboroga alitoa uamuzi huo akisema ni kwa mujibu wa kifungu cha Sheria Namba 148 cha Makosa ya Jinai, kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambacho kinatoa haki kwa watuhumiwa kupata dhamana. Alitoa uamuzi huo baada ya kupitia pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka kutaka wasipewe dhamana. Hata hivyo, alisema: “Washtakiwa wanazuiwa kutembelea maeneo ya Nyamongo mpaka kesi hiyo itakapokuwa imekwisha."

Hakimu huyo alisema kwa kuwa washtakiwa hao ni viongozi wakubwa wa chama walizuiwa ili kupunguza shinikizo la wanachama kutokana na tukio lililojitokeza, lakini kwa kuwa mazishi yameshafanyika, alisema wanaweza kudhaminiwa kama watakidhi masharti.

Hakimu Ruboroga alitaja masharti  ya dhamana hiyo kuwa ni kusaini mkataba wa dhamana wa Sh5 milioni kwa wadhamini wawili wanaoaminika.

Kwa wasio wakazi wa Tarime, alisema watatakiwa kupeleka mahakamani hati za mali isiyohamishika. Washtakiwa wote walikidhi masharti na kuachiwa kwa dhamana hadi Juni 26, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Juzi, Lissu na wenzake, Waitara Mwita Mwikwabe, Stanslaus Nyembea, Anderson Deogratias Chacha, Andrew Andalu Nyandu, Mwita Marwa Maswi, Bashiri Abdalllah Selemani na Ibrahimu Juma Kimu walifikishwa mbele ya mahakama hiyo na kusomewa mashtaka hayo matatu na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Casmir Kiria ambaye alisema, waliyatenda Mei 23, majira ya saa nne usiku. Wote walikana mashtaka hayo.

Wakati huo huo maiti wote waliokuwa wametelekezwa barabarani wamezikwa na ndugu zao huku baadhi ya familia zikikataa kuwazika kwa majeneza ya polisi na kutumia yale yaliyokuwa yameandaliwa huku wengine wakipanga kuyarudisha kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime, Constantine Massawe.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kewanja, Om’tima Tanzania alisema kuwa mmoja wa marehemu hao, Chacha Ngoka alizikwa na jamii. Hata hivyo, alisema polisi waliweka mwili wake ndani ya jeneza bila kuweka sanda hali ambayo iliwalazimu kumweka ndani ya jeneza lao na kumvika sanda. Hilo lilifanyika pia katika eneo la Nyakunguru alikozikwa marehemu Emmanuel Magige.

Katika Kijiji cha Bonchugu, Serengeti, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Mwikwabe Makena alidai kwamba walilazimika kuzika mwili wa marehemu Chawali Bhoke uliotelekezwa na polisi.


Alidai kwamba kabla ya kuutelekeza, walifyatua mabomu ya machozi na risasi hewani baada ya wananchi waliokuwa wamebeba pinde, mishale, mikuki na mapanga kujaribu kuzuia gari la polisi. Alisema walilazimika kuzika bila kuwapo kwa ndugu wa marehemu waliokuwa wameachwa Tarime.Hata hivyo, Kamanda Massawe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz hakuwa tayari kuzungumzia madai hayo.

No comments:

Post a Comment