Wednesday, May 18, 2011

Polisi waua watano


POLISI wameua watu watano na kujeruhi wengine kadhaa katika mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold, Tarime mkoani Mara.

Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi zilisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri katika eneo la Nyabirama.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Constantine Massawe, alisema askari walilazimika kutumia risasi za moto baada ya kutumia mabomu ya machozi bila mafanikio kutawanya kundi la watu waliojaribu kuingia kwa jinai na kupora mawe yenye dhahabu mgodini.

“Askari walilazimika kutumia risasi kukabiliana na watu wanaokadiriwa kuwa kati ya 800 na 1,000 waliokuwa wamevamia mgodi huo ili kuokota mawe yenye dhahabu,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, watu watatu walikufa katika eneo la tukio na wengine wawili walifia katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime. Majina yao hayakufahamika mara moja.

Hata hivyo, Kamanda huyo alitaja baadhi ya majina ya majeruhi waliolazwa hospitalini hapo kuwa ni Francis Emmanuel (20) mkazi wa kijiji cha Kewanja, Chacha Mwasi (23) mkazi wa kijiji cha Bisarwi wilayani Tarime na Mwikwabe Marwa (30) mkazi wa Mugumu wilayani Serengeti.

Alidai kwamba polisi wawili waliofika eneo la tukio walijeruhiwa kwa mawe yaliyokuwa yakirushwa kwa kombeo.

Akizungumzia tukio hilo kwa simu kutoka Dar es Salaam, Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), alilaani mauaji hayo na kuahidi kuchukua hatua.

Alilaani matumizi ya nguvu kubwa yaliyofanywa na polisi kukabiliana na wananchi waliojaribu kuvamia mgodi.
“Ninalaani sana kitendo cha askari kutumia nguvu kubwa ya kuua na kujeruhi wananchi kwa tuhuma za kuvamia mgodi. Nitachukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika katika tukio hilo la kusikitisha,” alisema Nyangwine bila kutaja aina hiyo ya nguvu alizoahidi.

Kamanda Massawe alisema ofisi yake inakusudia kuitisha mkutano maalumu wa viongozi wa mgodi wa dhahabu wa North Mara na wakazi wa vijiji vilivyo jirani kutafuta ufumbuzi thabiti wa matukio ya uvamizi na mauaji ambayo yamekuwa yakitokea mgodi hapo.

Alitoa wito kwa wananchi kuepuka vitendo vya uvamizi na uporaji mali katika mgodi huo kwa vile unamilikiwa kihalali na kampuni ya African Barrick Gold.

Wimbi la matukio ya uvamizi, uporaji mawe yenye dhahabu na mauaji ya watu katika mgodi wa dhahabu wa North Mara limeendelea kuwepo, huku baadhi ya askari, walinzi na wafanyakazi wa mgodi huo wakituhumiwa kupokea rushwa ya fedha na kuruhusu watu kuingia kuokota mawe yenye dhahabu.

No comments:

Post a Comment