Friday, May 20, 2011

OCD mbaroni kwa kumpiga risasi makalioni mhadhiri wa SUA



MKUU wa Polisi wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Onesmo Lianga ameshikiliwa na polisi mkoani Morogoro kwa muda na baadaye kuachiwa kwa
tuhuma za kumpiga risasi sehemu ya makalio mwalimu wa kikundi cha sanaa cha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dadie Kitururu (42).

Ndugu wa karibu na marafiki wa Bw. Kitururu alipigwa risasi Mei 11, mwaka huu majira ya jioni katika eneo la Forest wakati akiwa njiani kurejea nyumbani kwake, huku wakishangaa kwa nini polisi amtwange mtuhumiwa risasi badala ya kumtia mbaroni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Bi. Adolphina Chialo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema kuwa siku ya tukio majira ya jioni Bw. Kitururu akiendesha gari alimgonga mpanda baiskeli Salumu Chiga (58), mfanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mkazi wa Kichangani karibu na ofisi za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Kilakala na kukimbia.

Alisema kuwa OCD huyo ambaye alikuwa nyuma ya Bw. Kitururu aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 320 ANQ Suzuki Samurai, naye akiwa na gari lenye namba T 630 BFZ aina ya Rav 4 alimkimbiza Kitururu hadi eneo hilo la Forest.

Kwa mujibu wa RPC, baada ya OCD kuona Kitururu anakimbia zaidi, alifyatua risasi kwa bastola yenye namba PA06897 aina ya Chinese na kupasua taili la mbele na risasi ikapenya hadi kumfikia Kitururu kwenye makalio.

Kamanda Chialo alisema, baada ya tukio hilo OCD alimkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Morogoro na kuwekwa rumande na baadaye polisi waligundua kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na majeraha baada ya kuona akivuja damu, ndipo alipopelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.

"Baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mtuhumiwa huyo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kutokana na hali yake kuwa mbaya na aligundulika kuwa na kipande cha risasi katika makalio na hivyo kupatiwa matibabu," alisema.

Baada ya kugundua hivyo, ndipo polisi walipoamua kumshikilia OCD huyo kwa kwa mahojiano juu ya tukio hilo na kubaini kuwa alipiga tairi risasi likapenya na kumfikia Kitururu.

No comments:

Post a Comment