Wednesday, May 25, 2011

Polisi 'wapora' maiti mochwari

*Tundu Lisu akamatwa, afikishwa kortini Tarime

JESHI la Polisi limewakamata na kuwafikisha mahakamani Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na maofisa wengine wa chama hicho baada ya kudaiwa kufanya mkusanyiko usio halali na kuzuia watu kuzika ndugu zao.

Sambamba na hatua hiyo jeshi hilo limedaiwa kuingia mochwari ya Hospitali ya Wilaya ya Tarime na kuchukua kwa nguvu maiti nne za watu waliouawa na polisi hivi karibuni na kwenda kuzitelekeza maeneo mbalimbali ili kuzuia mkusanyiko wa kuaga maiti hizo kwa pamoja, kwa kile wanachoeleza ni kuzuia uvunjifu wa amani.

Bw. Lisu na wenzake wanadaiwa kukutwa katika Hosptali ya Wilaya ya mjini hapo wakilinda miili hiyo baada ya kusikia tetesi kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuichukua na kuisafirisha kusikojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Casmil Kria alisema watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, yaliyosomwa mbele ya Hakimu wa Wilaya, Bw. Yusto Ruboroga.

Mashtaka hayo ni kuingia eneo la hospitali bila kibali, kufanya mkusanyiko usio halali na kuzuia watu kuchukua miili ya ndugu zao.

Watuhumiwa hao ambao wanadaiwa kukutwa eneo hilo saa 4:00 usiku baada ya kusomewa mashtaka na kuyakana, walirudishwa rumande kwa 'sababu za kiusalama', na kesho watafikishwa tena mahakamani kwa ajili ya kupewa dhamana, endapo miili ya waliouawa itakuwa imeshazikwa.

Walioshtakiwa ni Mbunge wa Singida Magharibi, Bw. Tundu Lissu (43), Bw. Mwita Mwikwabe (36), Bw. Stancelaus Nyembea (33), Anderson Deogratias (35), Bw. Andrew Andaru (63), Bw. Mwita Marwa (48) Bw. Bashiri Abdallah Seremani (35) pamoja na Ibrahimu Juma Kimi (27) ambaye ni dereva wa Bw. Lissu.

Wakati huo huo, waandishi wanne wa habari pamoja na Mbunge Viti Maalumu, Bi. Ester Matiko (CHADEMA) nao walishikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Kidogo cha Nyamwaga na baadaye kuachiwa huru baada ya mahojiano.

Wandishi hao ni Bi. Beldina Nyakeke wa The Citizen, Anna Mroso (Nipashe), Bw. Anthony Mayunga (Mwananchi) pamoja na Mabere Makubi wa Chanel Ten ambao walikuwa kwenye msafara wa Bi. Matiko.

Waandishi wengine wa habari waliofika katika mahakama ya wilaya kufuatilia tukio hilo walizuiliwa kuingia na kutishiwa kupigwa
risasi na ofisa mmoja wa polisi.

Ofisa huyo ambaye hakufahamika jina aliwatimua waandishi hao, huku akiomba bunduki kutoka kwa askari mwenzake na kuiandaa mithili ya kupambana na adui.

“Toka! Toka! Naombeni bunduki yangu hapa naona nyinyi hamjui kufanya kazi, hatukuja kufanya mchezo hapa waondoe na wale watu upesi mahali hapa wasongee mbali huko hatutaki mtu hapa!” alisema.

Askari hao wakiwa wameziba njia huku ofisa huyo akiendelea kuelekeza bunduki yake kwa raia waliokuwa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment