Saturday, July 23, 2011

Jairo awekwa benchi


SERIKALI imemsimamisha kazi Katibu Mkuu  wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.  Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya   ufanyika uchunguzi dhidi ya tuhuma  zinazomkabili zilizoibuliwa bungeni. Jairo anadaiwa kuziandikia barua idara na  taasisi zilizo chini ya wizara ili kila moja itoe  sh. milioni 50 kwa ajili ya kufanikisha  uwasilishaji wa makadirio ya matumizi ya  wizara kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012. Anadaiwa pia kuwalipa posho za safari  watumishi wa wizara waliofuatana na  viongozi wa juu licha ya kuwa walishalipwa  na idara na taasisi zao. 
Wabunge Beatrice Shellukindo (Kilindi-CCM)  na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro  -CCM), ndio walioibua tuhuma hizo  walipojadili makadirio ya wizara, kabla ya  serikali kuyaondoa bungeni.  Serikali iliyaondoa makadirio hayo bungeni  kutokana na hoja za wabunge kuwa  haijajipanga kukabiliana na tatizo la umeme.  Bunge limetoa wiki tatu kwa serikali  kujipanga na kuyarejesha. 
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo,  akizungumza na waandishi wa habari jana  mjini hapa, alisema amemwagiza Mdhibiti  na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  (CAG), kufanya uchunguzi wa kina, ambao  anatakiwa kuukamilisha ndani ya siku 10  kuanzia alipopewa kazi hiyo. "Wakati uchunguzi ukiendelea, Jairo   amesimamishwa kazi.
Hatua nyingine  zitafanyika baadaye kulingana na matokeo  ya uchunguzi," alisema. Luhanjo alisema anatarajia kufanya uteuzi  wa mtu atakayekaimu nafasi hiyo katika  kipindi kisichozidi siku tatu. Luhanjo alisema baada ya uchunguzi  kukamilika na endapo tuhuma dhidi ya Jairo  zitathibitika, uamuzi dhidi yake utachukuliwa  na rais kwa kuwa ndiye mamlaka yake ya  uteuzi.

Alisema amechukua uamuzi huo dhidi ya  Jairo kwa kuwa sheria ya  utumishi wa  umma inampa uwezo wa kushughulikia  nidhamu serikalini. "Kwa sababu suala hili ni zito nimeamua  aende likizo, lakini baada ya uchunguzi na  nikipata matokeo ya uchunguzi huo nitampa  taarifa itakayoambatana na hati ya  mashitaka," alisema.
Akizungumzia utaratibu alisema baada ya  matokeo ya uchunguzi kupatikana, Jairo  atapatiwa taarifa itakayoambatana na hati  ya mashitaka, itakayoeleza kwa kifupi kosa  alilotenda na namna alivyolitenda ili atoe  majibu.  Luhanjo alisema katika kipindi hicho,  atakuwa amesimamishwa kazi na kuanza  kulipwa nusu mshahara.  Kwa mujibu wa Luhanjo, katika majibu,  anaweza kukubali au kukana tuhuma dhidi  yake, ambapo mamlaka ya nidhamu  itaendelea kutoa adhabu kulingana na uzito  na kwamba, kwa kuwa Jairo ni mteule wa  rais, ndiye atakayeamua hatima dhidi yake.

Awali, kabla Luhanjo hajatangaza uamuzi  huo, wabunge waliibua hoja hiyo wakitaka  kufahamu hatua zilizochukuliwa dhidi ya  Jairo. Hoja hiyo iliibuliwa wakati wa kipindi cha   maswali ya papo kwa hapo kwa waziri mkuu  bungeni, ambapo Rashid Ali Abdalah  (Tumbe -CUF), alihoji hatua ya Waziri Mkuu  Mizengo Pinda, kudai hana mamlaka ya  kumwadhibu Jairo. Katika swali la msingi Rashid alitaka  kufahamu ni kwa nini waziri mkuu alitoa  kauli kuwa hawezi kumwajibisha Jairo hadi  Rais Jakaya Kikwete atakaporudi wakati  makamu wake na yeye wapo.
Akiwasilisha hoja ya kuondoa bungeni  makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini,  Waziri Mkuu Pinda alisema Rais Kikwete  ndiye atakayeamua kuhusu hatima ya Jairo  kwa kuwa ndiye aliyemteua. Waziri Mkuu Pinda akijibu swali la Rashid,  alisema makamu wa rais au waziri mkuu  hawana mamlaka kikatiba ya kumwajibisha  Jairo, kwani mwenye uamuzi wa mwisho ni  rais wa nchi.
"Naomba niwaambie waheshimiwa wabunge  kwamba, si kila jambo linalotokea wakati  rais anapokuwa hayupo au yupo nje ya nchi  linaweza kutolewa uamuzi na makamu wa  rais au waziri mkuu," alisema. Alisema ni kweli kwa mujibu wa Katiba ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu  cha 47 (1) (c), rais anapokuwa nje ya nchi  makamu wake ndiye anayeshika madaraka  ya kuongoza taifa. Pinda alisema kuna wakati hata waziri mkuu  hupewa nafasi hiyo, kama na makamu wa  rais hayupo, lakini wote wawili wana ukomo  katika utekelezaji wa majukumu yao,  ikiwemo kuamua mambo ambayo ni rais  pekee anayepasa kuyaamua.

No comments:

Post a Comment