Thursday, July 21, 2011

Kikwete amweka kiporo Jairo

RAIS Jakaya Kikwete amemweka kiporo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo akisema ataona cha kufanya baada ya ziara yake ya Afrika Kusini.

Akizungumza jana nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu uvumi wa kujiuzulu kwa Jairo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hakuwa amepata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwake.

Lakini alisema kilichopo ni kuwa alimjulisha Rais Kikwete mambo yaliyotokea Jumatatu bungeni kuhusu mjadala wa Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo baadhi ya wabunge walitaka Jairo aondolewe.

“Amenijibu kuwa ‘sawa, nisubiri nitakaporudi Afrika Kusini tuone tunafanyaje’,” alisema Pinda akimnukuu Rais Kikwete.

Jumatatu wakati wa mjadala wa makadirio hayo, wabunge waliibua kashfa wakituhumu wizara hiyo kuchangisha Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa makadirio hayo.

Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), ndiye aliyeibua sakata hilo wakati akichangia hotuba ya Makadirio hayo kabla hayajaondolewa bungeni.

Katika kuthibitisha kashfa hiyo, Shelukindo aliwasilisha barua bungeni iliyoandikwa na Jairo ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo, kila moja ichangie Sh milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.

Mbunge huyo wa Kilindi pamoja na wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo, takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.

Pinda katika hoja yake bungeni, alikiri kwamba Jairo aliudhi na kutibua wabunge na akaahidi kuwasilisha suala hilo kwa Rais Kikwete aliyemteua ili achukuliwe hatua.

“Lazima nikiri hata mimi nilishtuka sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi hakuna namna ya kutetea,” alisema Pinda siku hiyo.

No comments:

Post a Comment