Thursday, July 28, 2011

Wabunge wataka ukweli kuhusu samaki wa Japan

SAKATA la samaki wanaodaiwa kuwa na sumu kutoka Japan walioingizwa nchini, limefikishwa bungeni na wabunge wameitaka Serikali ifafanue ukweli wa jambo hilo ikiwa ni pamoja na kueleza ni namna gani waliingizwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Kambi ya Upinzani pamoja na wabunge waliochangia jana bungeni kwa nyakati tofauti, walieleza kushitushwa na taarifa hizo na wakataka Serikali itoe tamko bungeni.

“Kuna taarifa kwamba samaki wenye sumu wameingizwa nchini, pamoja na uzito wa jambo hili, Serikali haijatoa tamko. Kwa mamlaka niliyo nayo, naitaka Serikali itoe tamko ieleze ukweli wa suala hili na hatua zinazochukuliwa,” alisema Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati, Profesa David Mwakyusa.

Mbunge huyo alikuwa akisoma taarifa ya Kamati ya Bunge kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Makadirio ya Matumizi ya mwaka 2011/12.

Kambi ya upinzani kupitia kwa Msemaji wake Mkuu kwa Wizara ya Maendeleo na Mifugo, Silvester Kasulumbayi, ikitumia taarifa za vyombo vya habari vya Julai 26, ilihoji ni namna gani kampuni ya Alphakrust Limited ya Dar es Salaam, iliruhusiwa kuingiza samaki hao.

“Kama TDFA ndiyo waliotoa kibali cha kuingizwa kwa samaki hao baada ya kufanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa hawana madhara, ni nani na wa mamlaka gani aliyegundua kuwa wana madhara? Ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya maofisa waliohusika kutoa kibali husika?” alihoji Kasulumbayi.

Wabunge hao wa upinzani walihoji sababu ya Tanzania yenye maziwa na bahari kuagiza samaki kutoka nje ya nchi. “Kwa rasilimali hii yote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu iliyojaa samaki wengi wa kila aina, kama Taifa tuna haja kweli ya kuagiza samaki kutoka nje ya nchi?
“Kwa nini fedha zetu za kigeni zisitumike kununua mahitaji mengine ambayo hayapatikani nchini?” aliendelea kuhoji.

Naye Amir Mhando, anaripoti kwamba Mbunge wa Nyamagana Ezekia Wenje na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wote wa Chadema jana ‘walichafua hewa’ kwa muda kwenye ukumbi wa Bunge kutokana na hoja zao tofauti.

Hatua hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, ambaye pia ni Mbunge wa Dole, Sylivester Mabumba (CCM), kumtoa nje ya ukumbi Wenje na pia kumtaka Lissu athibitishe kauli yake, kwamba Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Kassim Majaliwa, amesema uongo bungeni.

Zogo lilianza muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu saa nne asubuhi, wakati Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliposimama na kuomba kutoa taarifa kuhusu tukio lililotokea mapema wakati wa kipindi cha maswali na majibu likimhusisha Lissu.

Machali alisema isingekuwa busara kwa Lissu kuambiwa apeleke uthibitisho wake kwa Mwenyekiti kuhusu kauli kwamba Naibu Waziri kasema uongo.

Alisema badala yake Lissu alitakiwa afanye hivyo saa tano asubuhi, wakati muda huo ilikuwa saa nne, huku shughuli zikiendelea, hivyo angepewa nafasi mpaka saa saba mchana wakati shughuli za Bunge zinapokuwa zimesitishwa kwa muda.

Lakini akizungumzia jambo hilo, Mwenyekiti Mabumba alisema kwa vile Lissu wakati anatoa kauli hiyo alisema ana ushahidi ambao angeweza kuuwasilisha hata wakati anazungumza, hilo si tatizo na kuongeza kuwa wakati anatoa kauli yake pia alishaanza kugusia uthibitisho wake.

Kutokana na majibizano hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama na kusema hakuna haja ya wabunge kuvimbiana na kwa vile Lissu aliahidi mwenyewe apeleke na kama ataona muda hautoshi amwambie Mwenyekiti amwongeze muda.

Baada ya kauli ya Lukuvi, Wenje alisimama na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti, lakini hakuruhusiwa na kusikika akiita mara kadhaa: “Mwenyekiti hoja ya dharura… hoja ya dharura Mheshimiwa Mwenyekiti ”.

Mwenyekiti alijibu kuwa hakuna haja ya hoja ya dharura, kwani hoja hiyo inawasilishwa kama kuna vita na nchi sasa haina vita, hivyo kumtaka Katibu aendelee na ratiba nyingine, ambayo ilikuwa ni hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Lakini Wenje aliendelea kumwita Mwenyekiti na kutaka Mwongozo, huku Mwenyekiti naye akimtaka akae chini, lakini waliendelea kubishana kwa dakika kadhaa na Mwenyekiti kutishia kumtoa nje ya kikao.

Hata hivyo bado Wenje hakutii agizo la Mwenyekiti, ndipo alipoagiza askari wamtoe ukumbini na hatua hiyo kutekelezwa mara moja, huku baadhi ya wabunge wakilalamika chini chini hasa wa upinzani, wakati wa CCM wakipiga meza zao kuunga mkono.

Akizungumza nje, Wenje alisema Mwenyekiti hakumtendea haki kwani hoja yake ya dharura aliyokuwa anataka izungumzwe ni kuhusu taarifa ya kuingizwa nchini kwa samaki wenye sumu kutoka Japan.

Alisema taarifa alizonazo ni kuwa kuna tani 1,600 za samaki hao mitaani hazijakamatwa na Polisi na wananchi wanawatumia na hali hiyo ni hatari na jambo linalohitaji udharura.

No comments:

Post a Comment