Tuesday, July 5, 2011

Mishahara mipya yatengewa fedha

* Watumishi wapya 64,024 kuajiriwa
* Wengine 80,050 kupandishwa vyeo


SERIKALI imeongeza sh. bilioni 938 katika fedha zilizotengwa kugharamia malipo kadhaa ya watumishi wa umma, ikiwemo mishahara mipya. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema hayo bungeni jana, alipowasilisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012. Alisema serikali itarekebisha mishahara ya watumishi kwa kuzingatia kasi ya mfumuko wa bei, uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.

Kwa mujibu wa Hawa, katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kutumia sh. trilioni 3.2 kugharamia malipo ya mishahara, upandishwaji vyeo na kulipia madai ya malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa serikali kuu, za mitaa, wakala na taasisi za serikali.
“Kiasi hiki kimeongezeka kwa sh. bilioni 938 sawa na ongezeko la asilimia 40.2 ya fedha zilizotengwa kugharamia malipo hayo katika mwaka wa fedha wa 2010/2011,” alisema.

Hawa alisema katika kuboresha maslahi, serikali itaendelea kutekeleza sera ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma ya mwaka 2010.

Alisema mkakati wa utekelezaji sera hiyo  umeandaliwa, ambapo bodi ya maslahi na tija katika utumishi wa umma iliyoanzishwa itaanza kutekeleza majukumu yake rasmi katika mwaka huu wa fedha.
Kuhusu ajira, alisema serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 64,024 na  kipaumbele kitakuwa katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo, huku watumishi 80,050 wa kada mbalimbali wanatarajia kupandishwa vyeo.

Hawa alisema katika mwaka huu wa fedha, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali watu na kuratibu ajira. Alisema hilo litatekelezwa kwa kusimamia mfumo wa mishahara serikalini, ambapo ukaguzi wa mara kwa mara wa orodha ya malipo ya mishahara utafanyika.

Waziri alisema ukaguzi wa rasilimali watu utafanyika ili kuhakikisha waliopo wanatumika kwa ukamilifu na wanalipwa mishahara kulingana na stahili zao.

Katika hatua nyingine, alisema ofisi yake kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imepanga kuchunguza tuhuma 2,456. Pia itafanya uchunguzi maalumu wa vocha za pembejeo za kilimo, kutokana na kupokewa  malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. Alisema taasisi hiyo itaendesha kesi 466 zilizopo mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa uchunguzi.
Hawa alisema serikali itaendelea kufanya utafiti na udhibiti katika maeneo ya ununuzi, elimu, ubora wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na zinazotoka nje.

Waziri alisema mchakato unatarajiwa kuanza ili kuingiza somo la maadili, mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora katika mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa wizara hiyo, Suzan Lyimo, akiwasilisha hotuba yake alilalamikia maslahi duni ya wafanyakazi. Suzan aliiomba serikali kufanya maboresho  ya mishahara ya watumishi wa umma kwa kupandisha kima cha chini cha mshahara kutoka sh. 135,000 za sasa hadi sh. 315,000.

No comments:

Post a Comment