Saturday, July 16, 2011

Umeme kwa kaya mpaka mwakani

MPANGO wa dharura wa kupunguza makali ya mgawo wa umeme ifikapo Desemba mwaka huu, huenda ukagonga mwamba hata kama itapatikana mitambo mipya ya kufua umeme kutokana na utata wa upatikanaji wa gesi na mafuta mazito.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM),January Makamba, amebainisha jana kuwa, itachukua miezi 18 kupata gesi ya kutosha kuzalisha umeme wa dharura.

Awali Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja katika hotuba yake ya bajeti ya wizara hiyo, alisema ili kukabiliana na mgawo uliopo, Serikali imejipanga kuleta mtambo wa kutumia gesi asilia wa kuzalisha umeme wa Megawati 100 utakaofungwa Ubungo Desemba mwaka huu.

Mbali na mtambo huo, pia Ngeleja alisema ifikapo Juni mwakani, Serikali itafunga mtambo mwingine wa kutumia mafuta mazito kuzalisha umeme wa megawati 60 katika eneo la Nyakato, Mwanza.

Lakini January katika hotuba ya kamati yake, alisema kwa sasa mtambo wa kufua umeme unaotumia gesi asilia wa Symbion uliopo Ubungo, hauzalishi kwa kiwango chake cha megawati 112 kutokana na kukosekana kwa gesi.

Akafafanua kuwa, Kamati hiyo imejulishwa kwamba kiwango cha gesi hakiwezi kuongezeka katika muda mfupi kwa sababu mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirishia gesi, vimefikia ukomo wake wa juu.

January alisema mtambo huo mpya wa kupunguza makali ya umeme, utahitaji gesi iongezwe lakini ili hilo litekelezwe, kunahitajika upanuzi wa miundombinu hiyo ambao ukamilikaji wake utachukua miezi 18.

"Kwa maana hiyo, Kamati inapendekeza Serikali iuhakikishie umma kwamba mtambo huu (wa Ubungo) utapata gesi mara utakapofungwa Desemba na hautakuwa tembo mweupe.

"Kamati pia inapendekeza Serikali ieleze, ilikuwaje Tanesco (Shirika la Umeme), ikanunua mtambo mkubwa wa gharama kama huo bila kupanga kuwepo kwa gesi ya kuuendesha," alisema January.

Kuhusu mtambo ya mafuta mazito, January alisema ulipaswa kukamilika mwaka jana, lakini jana Ngeleja alisema utakamilika Juni mwaka 2012. Hata hivyo January alisema Kamati haijapata maelezo ya kuridhisha kuhusu upatikanaji wa mafuta mazito na gharama za kuyasafirisha hadi Mwanza.

Alielezea histori ya mtambo kama huo wa kutumia mafuta mazito uliofungwa Mwanza mwaka 2006/2007 wa Alstom Power Rentals ambao Serikali iliwekeza dola za Marekani milioni 21, zaidi ya Sh. bilioni 25, lakini mpaka leo haujawahi kutoa hata Megawati moja ya umeme.

Hata hivyo, Ngeleja katika hotuba hiyo, alikiri ugumu wa kutekeleza miradi ya umeme, na kubainisha wazi kuwa kati ya mwaka 2005-2010, Serikali ilikusudia kuongeza megawati za umeme 645, lakini walifanikisha miradi ya megawati 145 tu.

Katika bajeti hiyo, Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 402, kati ya hizo bajeti ya maendeleo ni Sh. bilioni 325 na Sh. bilioni 76.9 za matumizi ya kawaida.

Wakati huo huo Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela (CCM), amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kumuomba radhi kwa kumdanganya kuwa angepeleka umeme katika jimbo lake na badala yake akapeleka kwingine.

Katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, miradi ya umeme mkoani Kilimanjaro imepangwa katika majimbo matatu likiwemo la Same Mashariki, lakini vijiji vilivyoandikwa ni vya Same Magharibi, jimbo la Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David.

Mbali na kutaka kuombwa radhi, Kilango pia amebainisha bungeni jana kuwa ugawaji wa miradi ya umeme, umekuwa na upendeleo na kutoka mfano wa Mkoa wa Kilimanjaro ambako miradi hiyo iko katika majimbo matatu tu na yote ya mawaziri.

"Waziri sitakuunga mkono, umenitupia changa la macho, sikuachi leo, kila siku unaninunulia chai na unajua naweza kununua mwenyewe, mimi sitaki chai nataka umeme, haiwezekani watu wa jimbo langu wafanywe wateja wa tochi.

"Wewe mtu wa ajabu sana, umeendika jina la jimbo langu na kuweka miradi katika vijiji vya rafiki yako Mathayo," alisema Kilango.

Alisema mafundi wa umeme walitumwa katika jimbo hilo kufanya upimaji na yeye alishirikiana nao kila siku kuzungukia maeneo ambayo yanatarajia kupelekewa umeme.

Mbunge huyo alibainisha kuwa wakati wote wakifanya upimaji huo, yeye alikuwa akiwasiliana na Waziri Ngeleja kwa simu na kuhakikishiwa kuwa hayo ndiyo maandalizi ya kupeleka umeme.

"Lakini nimeangalia miradi ya umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro, sikilizeni wa kwanza Same Mashariki, lakini vijiji vya Same Magharibi (kwa Mathayo), Mwanga (Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe) na Siha ( Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawaza za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri,"alisema.

Mbunge huyo pia aliishauri Serikali kuchukua mradi mmoja wa umeme wa Stieglers Gorge wa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100 badala ya kuwa na miradi mingi midogo ambayo hawana uhakika itakamilika lini.

Alisema, ni bora Serikali iwaambie Watanzania wafunge mkanda ili watekeleze mradi. Huo kwa kuwa wamezoea na haijulikani kama wameshawahi kuifungua tangu wakati wa vita dhidi ya Nduli, Idd Amini walipotangaziwa kufanya hivyo na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kuhusu madini, Kilango alisema hana uhakika kama Tanzania inanufaika na utajiri wa madini yake na kuhoji kama Waziri Ngeleja ana undugu na nchi za nje zinazonufaika nayo.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM) alisimama mara baada ya Ngeleja kumaliza kusoma bajeti na kuomba mwongozo na kufafanua kuwa waziri huyo kadanganya Bunge.

Alifafanua kuwa, kuna mradi katika jimbo hilo la Nkasi Kaskazini ambo Ngeleja kasema umekamilika kwa karibu asilimia 60, lakini Mbunge huyo akasema kuwa hakuna hata nguzo moja katika eneo la mradi huo.

Akichangia bajeti hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema January amefanya kazi nzuri na kumkejeli ahame Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na Chadema ili wasaidiane kazi.

Mbowe alisema Serikali imepoteza uhalali was kushughulikia tatizo la umeme la muda mrefu na kinachohitajika ni kuundwa kwa kikosikazi kitakachokuwa na wadau mbalimbali wa asasi za kiraia, sekta binafsi na hata wabunge kishughulikie aibu ya mgawo.

Pia alitaka Rais Jakaya Kikwete atumie nafasi kumi alizonazo bungeni, kuteua wataalamu ili wapewe wizara hiyo na Ngeleja apelekwe Wizara ya Sheria na Katiba na Naibu wake, Adam Malima apelekwe Mipango.

Lakini baada ya kumaliza, Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uratibu, Sera na Bunge), William Lukuvi, aliomba kutoa taarifa na kufafanua kwamba Serikali inayo uhalali kwa kuwa CCM ilishindana na Chadema na kukishinda kwa kura.

No comments:

Post a Comment