Thursday, July 28, 2011

Watendaji wa Kata sasa kuwa na shahada

SERIKALI imesema itahakikisha kuwa watendaji wa Kata wanaoajiriwa ni waliohitimu chuo kikuu na si wenye elimu ya msingi.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) aliliambia Bunge jana kwamba itahakikisha watendaji hao wanapatiwa pia elimu ya uongozi kabla ya kupelekwa kuongoza kata yoyote.

Mwanri aliwataka wabunge wenye kata zisizo na watendaji wapeleke orodha kwake ili pengo hilo lizibwe kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba tatizo la ukosefu wa watendaji katika kata linatatuliwa.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu maswali ya wabunge mbalimbali akiwemo Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM) ambaye katika swali la nyongeza alisema baadhi ya kata na vijiji jimboni mwake havina watendaji. “Je Serikali haioni lengo la kupeleka madaraka na huduma vijijini halijatimia,” alihoji Laizer.

“Tumejaribu kuzibaziba. Kama kuna kata ambazo hazina watendaji wa Kata, hatupeleki waliomaliza darasa la saba, bali wahitimu wa chuo kikuu, kama kuna wabunge wenye kati zisizo na watendaji, walete orodha, tayari tuna maelekezo kutoka kwa Waziri Mkuu tuhakikishe tatizo linamalizwa," alisema na kuongeza kuwa watahakikisha wanapelekwa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, wanolewe kabla ya kuajiriwa.

Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay (CHADEMA) alishutumu kuwa uundaji wa vijiji unafanywa kienyeji na wakati huo huo akasema wakati wa uchaguzi vijiji vimekuwa vikiundwa na kutengeneza kata kisiasa.

Akijibu hoja hiyo, “kusema kuunda uunda ni kufanya kienyeji. Hakuna kijiji kimeundwa kienyeji. Habari kwamba tunaundaunda hapa hakuna.”

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Biharamulo, Dk. Anthony Mbassa (CHADEMA) alitaka aelezwe ni lini Serikali itatenga tarafa mbili zilizokuwepo na kuwa angalau nne ili kufanikisha suala zima la kiutawala na kiutendaji katika Wilaya ya Biharamulo.

Alitaka pia kufahamu ni lini Serikali itatoa miliki za vijiji hivyo. Mwanri alisema Serikali imegawa maeneo mapya ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya nchi ambapo kupitia tangazo la Serikali Namba 173 la Mei 7, 2010, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilipatiwa maeneo mapya kutoka kata saba na kuwa kata 15.

Vijiji viliongezwa kutoka 25 hadi 74, vitongoji vipya vikaongezwa kutoka 85 hadi 384. Hata hivyo alisema halmashauri imeendelea kuwa na tarafa mbili za Nyarubungo na Lusahunga.

No comments:

Post a Comment