Friday, July 8, 2011

Simba full shangwe

Image



Mlindalango wa timu ya Simba Juma Kaseja akishangilia kwa kuonesha flana yenye maandishi (There is only one Kaseja) yakimaanisha ‘Kuna Kaseja mmoja tu’ baada ya kudaka penati iliyopigwa na mchezaji wa timu ya El Mereikh ya Sudan kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Castle la Kagame uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Simba ilishinda kwa penalti 5-4.









MABINGWA
wa kihistoria wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame timu ya Simba jana ilifuzu kutinga kwenye fainali ya michuano hiyo baada ya kuinyuka timu ngumu ya El Mereikh ya Sudan kwa mikwaju ya penati 5-4 katika mchezo mgumu wa nusu fainali ya kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ambao ilibidi uende katika muda wa ziada hivyo kuchezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo El Mereikh ndio walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Simba katika dakika ya 12 kwa bao lililofungwa na Adiko Rime akiunganisha krosi ya Balla Gabir akiwa amezungukwa na mabeki wawili wa Simba .

Simba ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 24 kwa bao lililofungwa na Ulimbokwa Mwakingwe kwa kichwa baada ya mpira wa krosi ya Shija Mkina kuokolewa vibaya na kipa Isam Elhadary na kumfikia Mwakingwe aliyeutumbukiza kimiani.

Katika changamoto hiyo ya mikwaju ya penati shujaa wa Wekundu hao wa Msimbazi alikuwa ni kipa Juma Kaseja ambaye aliokoa mkwaju wa Jonas Sakwaha na kuwafanya mashabiki wa Simba waliofurika kwenye uwanja huo kulipuka kwa shangwe na kuimba ‘ Hatubebwi hatubebwi hatubebwi ikiwa ni katika kuwakejeli watani zao Yanga ambao juzi walitinga kwenye hatua hiyo ya nusu fainali kwa matuta dhidi ya Red Sea ya Eritrea ambapo mashabiki wa Simba wanahisi kuwa watani zao hao walipendelewa baada ya penati zao mbili kurudiwa baada ya kuzikosa awali.

Katika hatua hiyo ya upigaji penati tano tano Simba ndio walianza ambapo Jerry Santo aliongoza jahazi la Simba na kufunga penati ya kwanza lakini Faisal Agab Sido alisawazisha na kufanya iwe sare penati ya pili ya Simba ilipigwa na Salum Machaku na kwenda kugonga mwamba wa juu na hivyo kuzua hofu lakini El Mereikh nayo ilikosa penati yake baada ya Mnigeria Collin Kezechi kupaisha mkwaju wake.

Penati zilizofuatia zilipigwa na Salum Kanoni, Nassor Saidi ‘Chollo’ na Patrick Mafisango aliyepiga penati maridadi iliyomwacha kipa Isam El Hadary akichupa kulia na mpira kutinga kushoto kwa upande wa Mereikh Ahmed Elbasha, Bari Eldin Eldod na kipa Elhadary alifunga penati ya tano na hivyo kufanya ziongezwe moja moja.

Ndipo alikwenda kupiga Ulimboka Mwakingwe ambaye mbali ya kucheza kwa juhudi muda wote wa mchezo pia kiwango chake kilikuwa cha juu na kutumbukiza wavuni mkwaju wake na hivyo kazi ikawa kwa El Mereikh ambayo ilimpa jukumu Sakwaha ambaye penati yake iliokolewa na Kaseja na kumwacha ameduwaa uwanjani.

Kutokana na ushindi huo wa penati 5-4 ,Simba imefuzu kutinga fainali kwa jumla ya mabao 6-5 na sasa inamsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili inayofanyika leo kati ya mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Yanga dhidi Saint George ya Ethiopia.

No comments:

Post a Comment