Tuesday, June 14, 2011

Askofu Mdegela awasamehe waliohusika kumzushia kashfa


Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa Dk. Owdenbug Mdegela, amesema anawasamehe wote waliohusika katika kumzushia tuhuma ambazo zimethibitika kuwa za uongo.
Ametoa kauli hiyo baada ya Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo na jopo la wachungaji wa kanisa hilo kumsafisha.

Taarifa ya askofu Mdegela aliyoitoa kwa waumini wa kanisa hilo jana inaeleza kuwa tuhuma hizo zilizochapishwa na kusambazwa kwa makusudi na watu aliowaita ‘waumini wasio raia’ zina lengo la kulivuruga kanisa na kuichafua dayosisi hiyo mbele ya jamii na waumini.

Mdegela alitoa tamko hilo jana kwa waumini wa KKKT Dayosisi ya Iringa ambao walihudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa kuu la Cathedral.
“Natangaza rasmi uamuzi wangu wa kuwasamehe baadhi ya viongozi wakiwemo maaskofu na wachungaji wenzangu waliotumika kuasisi mpango huo wenye lengo la kulivuruga kanisa, dayosisi pamoja na kunichonganisha na waumini pasipo kutathmini madhara ya matamko yasiyolenga kuwajenga waumini wao kiroho,” alisema Mdegela.

Alisema wiki iliyopita kanisa liliitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi na wachungaji wote na kujadili kilichojitokeza baada ya maaskofu watatu kufika katika dayosisi hiyo kwa nia ya kuchunguza habari ambazo wanadai zinasikika mara kwa mara.

Alisema kuwa Halmashauri Kuu na wachungaji hao walikaa Juni 8, mwaka huu ili kuangalia mfululizo wa matukio hayo na baadaye kuyapuuza.

1 comment:

  1. Ni vema kuyapuuza na ni vema kuwasamehe hao anaowaita WALIOMZUSHIA, lakini nashindwa kuelewa mambo machache:
    1) Kwa nini awe mbogo anapoombwa kuchunguzwa madai hayo kama yeye yu safi maana hii ingemsafisha na kuonekana kuwa kuna wazushi.
    2) Mbona Mheshimiwa Askofu ana maneno yasiyohusiana na kazi yake? Anaposema maneno kama nitawafanyizia ana maana gani? na atawafanyizia akina nani? Maaskofu wenzake au nani?
    3) Maaskofu waliotumwa kwake wanaonekana ni watu wazima na wenye Busara na walio na ufahamu wa kutosha kuona majungu na yasiyo majungu. Je haikuwa busara kuwasikiliza badala la kuwafukuza? Je Huyo mchungaji wa kondoo anayewafukuza wachungaji wenzake au alifikiri watamnyanganya kondoo wake?
    4) Huyu Baba Askofu mwenye Kitanda Ofisini kwake mbona ni kama amechoka sana si astaafu tu au ana magonjwa yanayomfanya apende kujipumzisha? Baba ukichoka si uende tu Nyumbani upumzike au huko kuna kiti moto? kwa kuwa nyumbani kwako siyo mbali na unapofanyia kazi, na wala Iringa hakuna foleni kubwa ya magari kuhitaji kupata kitanda ofisini.
    Neno la Bwana lasema, Mwenye kutamani kazi ya Uaskofu atamani kazi iliyonjema, lakini pia linasema sifa za kutamani kazi hiyo ni pamoja na upole, kiasi na kuwa na uwezo wa kukemea. Jer kukemea ni huko kwa kutoheshimu mamlaka? Pamoja na kuwa Dayosisi ina mamlaka makubwa, hata hivyo KKKT agreement lazima inamtaka member atii mamlaka. Hawamgoi lakini wanataka kumsafisha kama Halmashauri yake ilivyolazimika kumsafisha akiwa mbele yake.

    Ahsante - Msharika Mtiifu wa KKKT

    ReplyDelete