Wednesday, June 1, 2011

Kiapo cha Mkapa chazua mjadala


     
Rais mstaafu Benjamin Willianm Mkapa

















 HATI ya kiapo ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, jana ilizua malumbano makali ya kisheria mahakamani na kusababisha washtakiwa, aliyekuwa Balozi wa Tanzania huko Italia, Profesa Costa Mahalu na mwenzake Grace Martin kushindwa kuanza kutoa utetezi wao katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili. Profesa Mahalu  na Grace aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi, walitarajiwa kuanza kujitetea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa wana kesi ya kujibu tuhuma zinazowakabili.

Watuhumiwa hao walikwama kuanza kujitetea baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Elvin Mugeta anayesikiliza kesi hiyo kukataa maombi ya mawakili wanaowatetea kutaka hati hiyo ya Mkapa iingizwe kwenye kumbukumbu za ushahidi za mahakama.Kukataliwa kwa ombi hilo lililowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa washtakiwa hao, Mabere Marando kulionekana kutaka kuzua mvutano, lakini Hakimu Mugeta alisema ameipokea hati hiyo ya kiapo cha Mkapa iliyowasilishwa mahakamani hapo, lakini wakati wa kuizungumzia bado haujafika.

Hakimu Mugeta alifafanua kuwa hati hiyo itazungumziwa baada ya washtakiwa kueleza namna watakavyojitetea, kama ni kwa mdomo au kwa viapo, ikiwa ni pamoja na kueleza idadi na kutaja mashahidi wao pamoja na vielelezo watakavyoviwasilisha.

Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi aliushutumu upande wa utetezi katika kesi hiyo baada ya kiapo cha Mkapa kuanza kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kabla ya kufika mahamani.

Wakili Lukosi alitoa mfano wa Gazeti la Mwanahalisi toleo la 239 la Aprili 27, mwaka huu kwa kuchapisha kiapo hicho, kukichambua kipengele kwa kipengele na kukitolea uamuzi kuwa upande wa mashtaka sharti ukunje jamvi kwa kuwa hauna kesi kutokana na kiapo hicho cha Mkapa.

Pia alizungumzia habari iliyoandikwa na gazeti la Mwananchi katika toleo la jana iliyomkariri Marando akithibitisha kuwa barua waliyomwandikia Rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo akiomba akubali kuwatetea washtakiwa hao, bado haijajibiwa.

Pia Marando alifafanua kuwa kutokana na umuhimu wa Rais Kikwete katika kesi hiyo, iwapo wateja wake watamaliza kujitetea pamoja na mashahidi wengine wataiomba mahakama imkumbushe.

Aliongeza kwamba kama hataridhia wataiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi mwaka 2016 atakapomaliza kipindi chake cha urais ili mahakama imlazimishe kufika mahakamani kutoa ushahidi huo.
Akijibu shutuma hizo, Wakili Marando alisema ndiye aliyeandaa waraka huo, lakini naye akautupia lawama upande wa mashtaka kuwa ndiyo unaopaswa kueleza zilifikaje kwenye vyombo vya habari.

“Mimi ndiye niliyeiandaa document (hati) hii kwa mkono wangu na nilikuwa nimeifungia mahali ambapo mtu yeyote hafiki. Kutokana na 'sensivity' (unyeti) wake niliikabidhi Serikali waraka huo kabla ya Aprili 27 (siku ambayo ilianza kuripotiwa kwenye vyombo vya habari),”
“Lakini wiki moja baadaye, nilishtuka kuiona kwenye gazeti, kwani hata mteja wangu hakuwa na nyaraka hiyo. Hivyo mimi ndiye niliyestahili kuwalaumu. Hata barua niliyomwandikia Katibu Mkuu Kiongozi nayo nilishtukia iko kwenye magazeti,” alidai Marando.

Kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti la Mwananchi alisema: “Mwananchi walinipigia simu wakiuliza utaratibu wa kisheria wa kumwita Rais, nami nikawaeleza kwa mujibu wa Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Mambo ya Rais aliye madarakani na hicho ndicho walichokiripoti.“Mimi naona halijaharibika jambo na tusikubali kuziba midomo magazeti pasipo lazima,” alisema Marando.

Wakili mwingine wa utetezi, Cuthbert Tenga aliiomba mahakama iwapatie mwenendo mzima wa kesi hiyo ili waweze kuandaa utetezi akidai kuwa hati walizo nazo hazikidhi kwa kuwa zina makosa.Kutokana na ombi hilo, mahakama ilikubali na kuahidi kuwapatia mwenendo huo keshokutwa na kwamba kesi hiyo itatajwa Juni 24, mwaka huu na ushahidi wa utetezi kuanza kusikilizwa Julai 8 na 11.

Profesa Mahalu na mwenzake wanadaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, wakati wa utumishi wao.Wanadaiwa kula njama na kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko nchini Italia, likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.

Wanadaiwa kuwa Septemba 23, 2002 jijini Rome, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58, maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.


No comments:

Post a Comment