Thursday, June 30, 2011

Ukweli wa vifo vya wapenzi 2 Dar wajulikana

POLISI Jijini Dar es Salaam wamepata ujumbe wa maandishi wa marehemu Nicholaus Maleko (43) aliyeelezwa kujiua pamoja na mpenzi wake, Catherine George (25) Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa Polisi, Maleko ameandika kuwa, yeye amejiua lakini kifo cha mpenzi wake ni bahati mbaya.

Maleko amedai katika barua hiyo kuwa, amejiua kwa makusudi kukwepa usumbufu wa kuhojiwa baada ya kubaini kifo cha mpenzi wake alichodai kilitokea Catherine alipojisahau na kunywa pombe, wakati akiwa katika dozi ya dawa za ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.

Akizungumza na HABARILEO jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela
alisema, barua hiyo ya Nicholaus imeeleza namna vifo hivyo vilivyotokea na itatumika kama sehemu ya ushahidi.

“Pamoja na kuwataja wadai na wadaiwa wake, ameandika namna mali zake zitakavyogawanywa kwa warithi na kufafanua kwa kina jinsi tukio zima lilivyotokea, ambalo kwa ufupi limehusisha uzembe wa mwanamke na makusudi ya Nicholaus,” alisema Kamanda Kenyela.

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, barua hiyo imemtetea Catherine na kueleza kuwa hakujiua kwa makusudi, ila bahati mbaya kwa kunywa bia aina ya Serengeti wakati akiwa katika dozi ya dawa za binadamu kutibu ugonjwa ambao hata hivyo, Nicholaus hakuutaja.

“Nicholaus, pamoja na kuwapa pole ndugu wa marehemu Catherine na kutuma salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa katika barua hiyo, pia ameeleza namna alivyojaribu kuokoa maisha ya dada huyo ambaye katika barua amemtaja kama mkewe,” alisema.

Kwa maelezo ya Kenyela, sehemu ya barua ya Nicholaus ilisomeka, “mke wangu amejiua kwa bahati mbaya lakini mimi nimejiua kwa makusudi kwa kunywa sumu ya panya kwa sababu sikuona sababu ya kuendelea kuishi na kusumbuliwa kwa yaliyotokea.

“Nilipoona hali yake imebadilika na kukumbuka alikuwa amekunywa dawa, nilimnywesha maziwa lakini hayakusaidia na baada ya hapo niliamua kumpa redbull kwa kudhani ninamsaidia kwa sababu kinywaji hicho ni energizer (cha kuongeza nguvu) lakini kwa bahati mbaya hali ilibadilika na kuzidi kuwa mbaya, akafariki dunia,” Kenyela alisoma barua hiyo.

Tukio hilo lilitokea Boko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kugunduliwa saa 12 asubuhi na mtoto wa marehemu Nicholaus aliyekuwa akienda bafuni kuoga, Masanje Maleko (20) baada ya kusikia baba yao akikoroma kwa sauti ya ajabu.

Mtoto mkubwa, Alexandre Kwilima (21) na ndugu yake Masanje walisema walilazimika kuvunja mlango wa chumbani kwa wawili hao na kukuta mama yao mdogo akiwa amefariki huku baba yao akiwa hajitambui.

“Tuliwafikisha katika hospitali ya MICO iliyoko Tegeta lakini baba alifariki muda mfupi baadaye. Hawakuwa na ugomvi na siku zote walizokuwa pamoja walizoea kunywa pombe huko chumbani kwao,” alisema Kwilima na kufafanua kuwa Catherine waliyeanza kumuona na Nicholaus Januari mwaka huu, alikuwa mama wa kwenda na kuondoka nyumbani hapo. Mtoto huyo alisema muda mrefu aliokaa nyumbani hapo kwa mfululizo ni wiki moja.

Hata hivyo, polisi imechukua sampuli ya maini, damu, utumbo na figo za marehemu hao na kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.

“Majibu ya Mkemia Mkuu ndio yatakayo tueleza ukweli kuhusu chanzo cha vifo hivyo kama ni sumu ya dawa ya panya, kuchanganywa dawa na pombe au kitu kingine lakini matapishi ya Nicholaus tuliyoyachukua hospitalini MICO, yana rangi ile ile ya sumu tuliyoipata pale na tumeyakabidhi kwa Mkemia Mkuu pia kwa uchunguzi wa kitaalamu,” alisema.

Katika hatua nyingine, msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, Jezza Waziri alisema uchunguzi wa awali wa marehemu hao umekamilika na kupeleka ripoti Polisi na miili yote miwili bado imehifadhiwa hospitalini hapo.

Watoto wa marehemu walisema kuwa, baba yao atasafirishwa Ijumaa kwenda Marangu, mkoani Kilimanjaro kwa maziko na hawakuwa na taarifa kuhusu mipango ya mazishi ya Catherine.

No comments:

Post a Comment