Tuesday, June 14, 2011

Polisi yapiga wanafunzi mabomu



Jeshi la Polisi limetumia mabomu kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom). Milio ya mabomu ilisikika katika eneo la Bunge mjini Dodoma, baada ya polisi kuwatawanya wanafunzi wa Chuo cha Sayansi ya Jamii cha Udom, kuandamana hadi bungeni wakitaka kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kushinikiza kulipwa posho za mafunzo kwa vitendo.

Mapema asubuhi, wanafunzi hao walikusanyika katika viwanja vya Nyerere Square mjini hapo na ilipofika saa 4.00 asubuhi walianza kuandamana hadi bungeni wakishinikiza kumuona Pinda na Kawambwa. Hata hivyo, jitihada zao zilishindikana baada ya polisi kuwaamuru kuondoka katika eneo hilo na walipokaidi amri hiyo ndipo walipopigwa kwa mabomu ya machozi yaliyofanya wanafunzi hao kukimbia ovyo.

Katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma hususan bungeni kulikuwa na ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU), waliokuwa wamebeba bunduki na mabomu ya kurusha kwa mkono.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi Kitivo cha Sanaa ya Lugha na Sayansi za Jamii, Mwakabinga Philipo, alisema wameamua kuandamana kutokana na kutotekelezewa madai yao ambayo ni kupatiwa fedha za mafunzo kwa vitendo ambazo wamekuwa wakiahidiwa, lakini hawapatiwi.

Alisema Seneti ya Udom Juni 8, mwaka huu ilitoa taarifa kuwa tatizo la madai ya fedha za mafunzo kwa vitendo halitatokea tena. Alifafanua kuwa licha ya ahadi hiyo, wanashangazwa kuona mpaka sasa haitekelezeki ndio maana waliamua kwenda bungeni kuonana na viongozi hao.

Mwakabinga alisema kutokana na ahadi zilizotolewa na viongozi hao ndio maana waliamua kwenda kuonana na Pinda na Kawambwa ili kupata ufumbuzi wa fedha hizo. Baada ya kutawanywa na polisi, ilipofika majira ya saa 6:00 mchana, wanafunzi hao walikusanyika tena katika viwanja vya Nyerere wakidai kuwa Waziri Kawambwa angekwenda kuzungumza nao.

Baada ya wanafunzi hao kukusanyika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Msekela, alifika katika eneo hilo kwa lengo la kuwatuliza, lakini jitihada zake ziligonga mwamba baada ya kumzomea na kumwambia “hatukutaki wewe, tunamtaka Waziri.” Baada ya Dk. Msekela kuzomewa, askari wa FFU walianza kuwatawanya wanafunzi hao na kukimbizana nao katika mitaa mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata baadhi yao.

No comments:

Post a Comment