Wednesday, June 8, 2011

LEO NI BAJETI

Mawaziri wapigia debe bajeti 

MACHO na masikio ya mamilioni ya Watanzania na wadau wa nje, leo yanaelekezwa Dodoma ambako Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12 itasomwa. Wananchi wengi wamekuwa na shauku ya kujua mwelekeo wa bajeti hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha iliyotokana na kupanda kwa bei vyakula na bidhaa za mafuta.

Kwa takriban wiki nzima iliyopita, baadhi ya wananchi wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu katika vyombo vya habari, wakiisihi serikali kuhakikisha kuwa bajeti ya mwaka huu inawaondoa katika hali ngumu ya maisha.

Bajeti hiyo itakayosomwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo itatangazwa kwa wakati mmoja na bajeti za serikali za nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika mtazamo wa kuimarisha mshimakano na umoja wa nchi hizo.

Kwa kawaida na mazoea ya muda mrefu, bajeti ya serikali imekuwa ikisomwa siku za Alhamisi ya wiki ya kwanza ya Juni, lakini mwaka huu imebadilika ikielezwa kwamba hiyo ni kutokana na siku hiyo kuangukia siku ya Uhuru wa Uganda.

Akizungumza bungeni jana asubuhi, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema bajeti hiyo itatanguliwa na hotuba ya hali ya uchumi itakayosomwa pia na Waziri Mkulo. Alisema hotuba hiyo itasomwa asubuhi, wakati ile ya bajeti itasomwa jioni.

Baadhi ya mawaziri akiwamo Mkulo wameifagilia bajeti hiyo huku Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) likitoa mapendekezo na matumaini yake.

CTI: Tunataka bajeti ya uchumi wa viwanda

Shirikisho hilo limesema kuwa linaisubiri kwa hamu bajeti hiyo likitaka iwe ya kukuza uchumi na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Kauli ya CTI huku likilalamikia kupanda kwa gharama za uzalishaji zilizotokana na mgawo wa umeme wa Tanesco.

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Christine Kilindu alisema jana kwamba serikali inapaswa kutoa bajeti ambayo pia itaondoa kodi zinazoumiza uzalishaji mkubwa. Alisema kodi kubwa zisizo za msingi zinachangia kupanda kwa gharama za uzalishaji ambao mwishowe husababisha kupanda kwa gharama za maisha kwa mwananchi wa kawaida. 

"Tunataka bajeti ambayo itaondoa kodi zinazokwamisha uzalishaji mkubwa na ukuaji uchumi, tunataka bajeti itakayopunguza makali ya maisha kwa mwananchi kwa kumwezesha kupata bidhaa kwa urahisi," alisema Kilindu.

Alisema bajeti hiyo inapaswa pia kuweka mazingira mazuri na yanavyovutia kibiashara ili kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha uwekezaji. Alisema kwamba anategemea kuona umeme ukiwekewa mazingira ya kukuza uchumi na uwekezaji nchini, akisema bila kufanya hivyo hakuna kitu kitakachofanyika.

"Bila umeme hakuna kitu chochote, serikali inapaswa kuongeza nguvu na msukumo kuona umeme siyo tu unamulika maisha ya watu kwa kutoa mwanga, bali iwe ni nguvu ya kusukuma ukuaji wa uchumi wa nchi."

Mawaziri wapigia debe bajeti

Katika kujiwekea mazingira mazuri na kuzuia kubanwa na wabunge, baadhi ya mawaziri wamepigia debe bajeti za wizara zao huku Mkulo, akiahidi kuwa malimbikizo ya vyombo vya usalama yatalipwa mwezi huu.

Mara kwa mara baadhi ya wabunge wamekuwa wakitishia kukwamisha baadhi ya bajeti za wizara, kutokana na kukosa majibu ya msingi kwa mambo mbalimbali ya msingi. Jana asubuhi baadhi ya mawaziri walipokuwa wakijibu maswali bungeni walisisitiza kuwa mambo mengi waliyokuwa wakiulizwa yamezingatiwa katika bajeti.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamis Kagasheki, akijibu swali kuhusu malipo ya malimbikizo ya posho za polisi ikiwamo za wakati wa uhamisho, alisema wizara yake imeandaa mwongozo wa kisera wa namna ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.Alisema katika mwongozo huo ambao tayari ulikubaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi, wizara yake imejipangia utaratibu wa kutatua kero hiyo kuanzia kwenye bajeti ya mwaka huu.

Balozi Kagasheki alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Mohammed Sanya, ambaye alitaka kujua mkakati huo ukoje kutokana na tatizo hilo kuwa ni la muda mrefu. Baada ya majibu hayo, Waziri Mkulo alisimama na kukuongeza kuwa siyo malimbikizo ya polisi pekee, bali ya vyombo vyote vya usalama na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha yanalipwa kabla ya mwezi huu kumalizika.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe naye alipigia debe bajeti ya wizara yake ambayo tayari ilisifiwa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu, kutokana na kugusa kila eneo huku ikitajwa kuandaliwa kwa weledi wa hali ya juu.

Akijibu maswali likiwamo lililohusu ujenzi wa Barabara ya Babati, Dareda hadi Minjingu na kuhusu kero za barabara katika Jimbo la Ludewa linaloongozwa na Profesa Raphael Mwalyosi, Naibu Waziri huyo alisisitiza kuwa wizara yake ni sikivu na mambo mengi yatazingatiwa ndani ya bajeti.

Alisema wizara iko makini na Bajeti ya Ujenzi imezingatia mambo mengi ya msingi huku akitupa kete ya kuomba uungwaji mkono kwa wabunge ili waipitishe.

No comments:

Post a Comment