Friday, June 17, 2011

Mbowe: Kesi zimeniletea msongo wa mawazo

  • Kapteni Komba adai jina lake limekatwa


MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe, ameliambia Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa, ameshindwa kujaza fomu za kutangaza mali zake kutokana na msongo wa mawazo.

Akihojiwa kwenye baraza hilo jana, Mbowe alisema tangu umalizike Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, amekumbwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kesi mbalimbali ambazo zimemsababishia msongo wa mawazo na kumwathiri kifamilia. Alisema alifikishwa katika mahakama tatu tofauti, zikiwamo Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hai kwa tuhuma mbalimbali ambazo zimemsababishia msongo wa mawazo.

“Katika kipindi chote hicho nimekuwa kwenye mahakama tatu tofauti nikituhumiwa kwa mambo mbambali ambayo ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na matokeo ya kazi yangu,”alisema Mbowe na kuongeza:
“Siilaumu Tume kwa lolote, naiheshimu sana na naheshimu kazi yao, niliona kuliko kujaza kwa makosa ni bora nichelewe kuileta,”alisema.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema pia kutokana na mali na biashara alizonazo alishindwa kujaza fomu hizo kwa wakati kwa sababu ana makazi sehemu tatu na kote huko kuna mali zake.
“Naliomba radhi Baraza, ratiba yangu imekumbwa na mambo mengi sana. Mimi ni mbunge na ni kiongozi wa chama cha siasa hivyo, nilikosa utulivu wa kujaza fomu kwa wakati,”alisema.

Kapteni Komba adai jina lake limekatwa

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba amesema ameshangazwa kuitwa katika baraza hilo wakati yeye alijaza fomu na kuirejesha kwenye Ofisi ya Bunge.

“Sina mali za kutisha hadi niogope kujaza fomu, mimi nina vijihela tu kidogo kama Mtanzania mwingine wa kawaida,”alisema Komba na kuongeza kuwa:
“Nina marafiki wengi kama kina Bakili Muluzi wamenipa mahela sasa ningeyafanyia nini,”:
Komba pia alilalamikia jina lake kukatwa katika orodha ya wabunge wengine ambao walikuwa wamerejesha fomu na kudai kuwa hiyo ni hujuma.

“Wana lao jambo haiwezekani jina langu liwemo kwenye orodha ya wabunge waliorejesha fomu halafu lionekane limekatwa,”alisema.
Mbunge huyo aliitaka tume hiyo iwasiliane na viongozi husika moja kwa moja badala ya kupitia kwa spika kwa sababu katika suala la kutangaza mali hawawajibiki kwa spika. Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Damian Lubuva alisema baada ya kusikiliza utetezi wa viongozi hao watatoa uamuzi na mapendekezo yao kwenye mamlaka zinazohusika.

No comments:

Post a Comment