Friday, May 18, 2012

CCM sasa yabariki mgombea binafsi


HALMASHAURI Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM imebariki rasmi kuwapo kwa mjadala wa mgombea binafsi katika mchakato wa kuandikwa Katiba mpya, ikiwa ni siku chache baada ya chama hicho tawala kuwataka wanachama wake kujiandaa kisaikolojia kukabaliana na wagombea hao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Uamuzi huo ni moja ya mambo yaliyoamuliwa katika kikao cha Nec, kilichomalizika juzi mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na shinikizo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wanaharakati na wanasheria wanaotaka kuruhusiwa kwa kwa mgombea binafsi jambo ambalo pia liliwahi kupigiwa debe na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu  maazimio ya kikao hicho cha Nec, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema, “ Hatuna tatizo na suala la mgombea binafsi, jambo hili linajadilika, ni mambo ambayo Nec imeona kuwa yanahitaji mjadala mpana zaidi.”

Alisema mbali na kuwa suala hilo linajadilika, pia mchakato wa kuandika Katiba mpya unawashikirisha wananchi wote hivyo ni vyema mwafaka ukapatikana kutokana na mjadala wa wananchi wote.

Nape alisema mawazo hayo ya CCM watayawasilisha kama maoni kwenye Tume ya Kuratibu maoni ya Katiba iliyoanza kazi Mei mosi mwaka huu.

Alisema mambo mengine ambayo Nec imependekeza yajadiliwe ni pamoja na kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, utaratibu wa uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya rais, uteuzi wa mawaziri na waziri mkuu na uteuzi wa Tume ya uchaguzi.

Mengine ni muundo wa Bunge na Baraza la Wawakilishi, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais, uwepo wa Baraza la pili la Kutunga Sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, mfumo wa Mahakama na nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano.

“Awali, Rais wa Zanzibar ndiye alikuwa Makamu wa Rais lakini mfumo huo uliondolewa na sasa Rais wa Zanzibar ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri,” alisema Nape.

Yabaki yalivyo
Alisema yale ambayo yalijadiliwa na kuonekana kuwa yabaki au yaingie katika Katiba mpya kama yalivyo, ni pamoja na kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kubaki kwa muundo wa Serikali mbili, kuendeleza mihimili mitatu ya dola na  kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Mambo mengine ni kuendeleza umoja wa kitaifa, kufanyika uchaguzi mara kwa mara katika vipindi maalumu kwa kuzingatia haki ya kupiga kura, kuendeleza haki za binadamu, dola kutokuwa na dini na Serikali kuwa mmiliki wa rasilimali kuu za nchi.

Katika orodha hiyo pia Nape alitaja mengine kuwa ni kusimamia maadili ya viongozi ikiwa ni pamoja na kuipa nguvu ya kikatiba Tume ya Maadili ya Viongozi, kuimarisha madaraka ya umma, kuhamasisha sera ya misingi ya kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine, kusimamia hifadhi ya mazingira na Rais kuendelea kuwa mtendaji.

CCM ipo imara
Katika hatua nyingine, Nape alisema CCM ni chama imara na kwamba wanaosema kinakimbiwa na wanachama wake wanatakiwa kufanya utafiti kwanza.

“Ukitizama kwa undani utaona kuwa viongozi waliokimbia ni sita tu na hata hao wanachama 5,000 mara 10,000 tunaosikia katika vyombo vya habari kuwa wamekihama CCM, ukifuatilia utaona si kweli,” alisema Nape.

Alifafanua kwamba, wingi wa watu katika mikutano mbalimbali ya vyama vya wapinzani haina maana kuwa watu hao ndio watamchagua mgombea wa chama husika.

Nape alimtolea mfano aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, mikutano yake ilijaa watu wengi, lakini kura alizopata hazikumwezesha kushinda kiti cha Urais.

Historia ya mgombea binafsi
Moto wa kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi wa kisiasa uliwashwa na Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma mwaka 1993, akiiomba Mahakama iruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi.

Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 24, 1994 na Jaji Kahwa Rugakingira, Mtikila  aliibuka mshindi.

Hata hivyo, Serikali ilikataka rufaa Mahakama ya Rufani lakini wakati rufaa hiyo ikisubiri kusikilizwa, ilipeleka muswada bungeni ambapo ilifanya marekebisho ya kikatiba na kuweka ibara inayotamka kuwa kila mgombea ni lazima awe amependekezwa na chama cha siasa.

Lakini, Februari 17 mwaka 2005, Mtikila alifungua kesi nyingine Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akipinga marekebisho hayo ya Katiba ya mwaka 1994. Katika kesi hiyo alikuwa akiiomba Mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru kuwepo kwa mgombe binafsi.

Katika hukumu iliyotolewa Mei 5 mwaka 2006, Mtikila aliibuka mshindi kwa mara nyingine tena baada ya Mahakama Kuu Dar es Salaam kukubaliana na hoja na maombi yake ya kuwepo kwa mgombea binafsi.

Hukumu hiyo ilitolewa na na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo, likiongozwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi,  Amir Manento pamoja na Salum Massati (Jaji Kiongozi Mstaafu pia na Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa) na Jaji mstaafu, Thomas Mihayo.

Lakini, Serikali ilikata rufaa tena Mahakama ya Rufani, ikipinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu Dar es Salaam na safari hii hukumu hiyo ilisikilizwa na jopo la Majaji Saba wa Mahakama ya Rufani Aprili  8, 2010.

Katika hukumu yake ya Juni 16,2010,  jopo la majaji hao saba wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan, lilitupilia mbali hoja ya Mtikila.

Jopo hilo lilimhusisha pia majaji Eusebio Munuo, Januari Msofe, Benard Luanda, Mbarouk Mbarouk, Nathalia Kimaro na Sauda Mjasiri

No comments:

Post a Comment