Tuesday, May 22, 2012

Vurugu kubwa zazuka Pwani


•  Wananchi wachoma moto nyumba ya polisi
 
VURUGU kubwa zimeibuka Ikwiriri wilayani hapa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za wafugaji ikiwemo kuchomwa moto kwa nyumba mbili, ikiwemo ya afisa wa polisi.
Habari zimedai kuwa wakulima wa eneo hilo, tangu jana asubuhi walianza kuwashambulia wafugaji wa kijiji hicho, na kuvamia nyumba zao, huku wakiharibu na kupora kila kitu walichokikuta, kwa kile kilichodaiwa kulipa kisasi cha kuuawa mwenzao, Shamte Tawangala(60) kunakodaiwa kufanywa na jamii ya wafugaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, amethibitisha kutokea kwa vurugu hizi na kudai kuwa, amelazimika kuongeza nguvu kwa kutuma askari wengi wa kikosi cha kutuliza ghasia, ili kuzima ghasia hizo.
Kamanda Mangu hata hivyo, alisema hadi sasa hawajajua idadi kamili ya watu waliojeruhiwa ama kuwepo na taarifa za waliopoteza maisha katika mapigano hayo, kwa vile hadi jana mchana walikuwa katika jitihadi za kuzima vurugu hizo.
Imedaiwa kuwa, awali polisi waliojaribu kutuliza ghasia walikumbana na mashambulizi ya mawe toka kwa wananchi, kiasi cha kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Habari zimedai kuwa, wakulima na wakazi wa kawaida wa kijiji hicho, walichukizwa na kitendo cha polisi kupuuzia tukio la kuuawa kwa Tawangala, anayedaiwa kushambuliwa vibaya hadi kufa kwa fimbo na vijana wawili wanaodaiwa kuwa ni wafugaji.
Imedaiwa kuwa, nyumba mbili pamoja na duka la afisa mifugo wa Kata ya Umwe, aliyejitambulisha kama Elikabu Lameck, vimevunjwa na kuchomwa moto na wananchi hao waliopora bidhaa zote zilizokuwemo.
Lameck alidai hatua ya kumshambulia Tawangala, inatokana na kile kilichodaiwa na wananchi hao kuwa, ni uhusiano wake wa karibu na mmoja wa wafugaji, aliyetajwa kwa jina la Masanja Mabala.
Vurugu hizo zimemlazimisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza pamoja na viongozi mbalimbali wa vyombo vya usalama kwenda Ikwiriri kutuliza.
Akizungumzia tukio la mauaji ya mkulima huyo, Mangu alidai kuwa vijana wawili wa jamii ya wafugaji wanadaiwa kuhusika na tukio hilo lililotokea Mei 19, mwaka huu katika kitongoji cha Njogoro, Kijiji cha Umwe Kusini, Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji.
Kamanda huyo aliongeza kuwa, chanzo cha mauaji hayo kinaelezwa kuwa ni vijana hao wachungaji kutaka kulisha mifugo yao kwenye shamba la mahindi la Tawangala, na alipojaribu kuwakataza, walianza kumshambulia kwa fimbo hadi kufariki dunia.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa zahanati ya Ikwiriri kwa uchunguzi wa daktari, na hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, ambapo polisi wanaendesha msako mkali kuwatia mbaroni waliohusika.
 

No comments:

Post a Comment