Wednesday, May 23, 2012

jalada la Mkulo latua kwa Hoseah


ASEMA ALIANZA KULISHUGHULIKIA JANA, LINAHUSU TUHUMA ZA UUZWAJI WA KIWANJA KWA MOHAMMED ENTERPRISES
Patricia Kimelemeta na Raymond Kamnyoge
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah jana alikuwa akichambua majalada ya baadhi ya mawaziri waliong’olewa baada ya wizara zao kutajwa kuhusika na ufisadi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Tayari Dk Hoseah alikwishatangaza kwamba Takukuru imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma za mawaziri hao kabla hata ya Rais Jakaya Kikwete hajawang’oa katika mabadiliko yake ya Baraza la Mawaziri aliyofanya mapema mwezi huu huku Ikulu nayo ikiagiza uchunguzi kwa watendaji wa wizara husika.

Mawaziri walioondolewa ni pamoja na aliyekuwa wa Fedha, Mustafa Mkulo, Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Omary Nundu (Uchukuzi).

Jana, akizungumza na gazeti hili, Dar es Salaam, Dk Hoseah alisema tangu CAG alipowalisha ripoti hiyo serikalini walianza uchunguzi wa tuhuma hizo ili kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria.
Alisema jana hiyo alikuwa akipitia tuhuma za Mkulo kuhusu na uuzaji wa Kiwanja Namba 10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MTeL).

“Tangu CAG alipowasisha ripoti yake Serikalini tulianza mchakato wa kuwachunguza kulingana na tuhuma zinazowakabili kwa kila mmoja kwa nafasi yake ili tutakapomaliza zoezi hilo tuwasilishe kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Dk Hoseah.

Mkulo aishangaa Takukuru

Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya kuchunguzwa, Mkulo alisema anachojua ni kwamba uchunguzi au mahojiano ya Takukuru na mawaziri ni wa kimaadili na ni jambo la siri.

“Huwezi kusimama sokoni Kariakoo kwenye watu wengi na kutangaza kwamba tunamchunguza au tunamhoji Mkulo ni kwenda kinyume na maadili ya Takukuru,” alisema Mkulo.

Alisema uchunguzi unaweza kuvurugika kama unawekwa hadharani ukiwa katika hatua za mwanzo.

“Ndiyo maana nasema hata kama ninachunguzwa au nimehojiwa kuna umuhimu gani kutangaza? Kwa nini Takukuru wasisubiri ili kupata uhakika katika uchunguzi wao?”

Mkulo alikuwa akirejea Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007, Kifungu cha 37 ambacho kinazuia mtu yeyote kueleza kwa kina mchakato wa uchunguzi unaofanywa na Takukuru dhidi ya mtuhumiwa.

Watendaji nao

Dk Hoseah alisema uchunguzi unaoendelea hivi sasa siyo kwa mawaziri hao pekee, bali unagusa pia baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali ambao wamehusishwa kwa namna moja au nyingine kwenye Ripoti ya CAG hivyo kusababisha kuwajibishwa kwa mawaziri.

Alisema ripoti zilizopo kwenye ofisi yake ni za viongozi mbalimbali ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara.

Katika Mkutano wa Saba wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, wabunge wa upinzani pamoja na wa CCM walifikia uamuzi wa kusaini fomu ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda lengo likiwa kumshinikiza kuwawakijibisha mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo vinginevyo, ajiuzulu.

Hatua hiyo iliibua mvutano mkali ndani ya CCM huku wabunge wa chama hicho wakishikilia msimamo wa kuitaka Serikali kuwawajibisha mawaziri hao hali iliyomfanya Rais Kikwete kupangua Baraza lake la Mawaziri na kulipanga upya huku akiwatosa mawaziri sita kati ya wanane waliotajwa katika ripoti hiyo.

Ripoti ya CAG

Katika shinikizo hilo la wabunge, Mkulo alikuwa wa kwanza kutakiwa ajiuzulu, kutokana na kashfa ya kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa Kiwanja hicho Na.10 kwa MeTL.

Kilichomponza Dk Mponda ni kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD) ambako ukaguzi maalumu katika bohari hiyo ulibaini kuwapo tofauti ya Sh658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokewa na kuripotiwa wizarani kwenda MSD, bila ya ushahidi wa kuzipokea.

Pia, uchunguzi unaonyesha kuwapo Sh100 milioni zilizopelekwa MSD kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kutumiwa na Bohari hiyo bila kuwepo kwa mchanganuo wa matumizi.

Ukaguzi pia ulibaini kuwepo kwa kiasi cha Sh4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh4.344 bilioni ndicho kilichopelekwa MSD  ukiondoa Sh196 milioni ambazo zilitumika bila kuwapo kwa ushahidi wa kupokewa MSD kutoka wizarani.

Kwa upande wa Maige, pamoja na mambo mengine, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitaka awajibishwe kwa madai ya kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kampuni ambazo hazina sifa na kusafirishwa nje kwa wanyama wakiwamo twiga na tembo kinyume cha sheria.

Nundu alidaiwa kuipigia kifua kampuni ya China Merchant ili apate zabuni ya ujenzi wa magati mawili katika Bandari ya Dar es Salaam huku Ngeleja akidaiwa kukaa kimya wakati Tanesco ikifanya ununuzi wa Sh300 hadi 600bilioni kwa mwaka mmoja.

Profesa Jumanne Maghembe ambaye alihamishiwa Wizara ya Maji akitokea Kilimo, Chakula na Ushirika, alituhimiwa kwa kuchelewa kwa mikopo ya pembejeo kwa wakulima huku George Mkuchika ambaye sasa yuko Ofisi ya Rais (Utawala bora), akituhimiwa kuwa akiwa Waziri wa Nchi Ofidi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), halmashauri nyingi zilifanya ufisadi wa kutisha ukitolewa mfano wa Kishapu ambayo inadaiwa kufuja fedha za umma kiasi cha Sh6bilioni.

No comments:

Post a Comment