• Wamkabidhi orodha Waziri Muhongo
WAFANYAKAZI wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) wameibua hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wasio waaminifu na kukabidhi majina hayo kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wafanyakazi hao walifikia hatua hiyo jana katika mkutano wao na waziri huyo alipotembelea shirika hilo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Baada ya kuibua madai hayo na kupitishwa na makaratasi, wafanyakazi hao waliandika majina ya mafisadi hao na kumkabidhi waziri ambaye aliondoka nayo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Katika mkutano huo, baada ya wafanyakazi hao kuibua madai hayo na kudai kuwa wanawafahamu watu hao kwa majina, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakimu Maswi, aliwataka wawataje kwa majina watu hao, ili waweze kushughulikiwa.
Maswi alisema haiwezekani miaka 50 ya Uhuru bado nchi inakabiliwa na tatizo la umeme na wananchi wanaendelea kulalamika, hivyo ni wakati wa kuwashughulikia wale wote ambao ni wazembe na wala rushwa ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya shirika hilo.
“Mkiona ni vigumu kusema hadharani andikeni muweke kwenye boksi ili waziri aondoke nayo. Wajibu wangu ni kutekeleza majukumu yangu, sitamwonea mtu yeyote aibu,” alisema katibu mkuu huyo.
Aliwatahadharisha watumishi hao kuwa na uhakika na ushahidi kwa majina watakayoandika, ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa walengwa.
Katibu mkuu huyo alisema hataki kuona mgawo wa umeme ukiendelea nchini na kuongeza kuwa baadhi wa watumishi hawana nidhamu wala heshima kwa kuwa miongoni mwao kuna vishoka.
“Wezi wa mafuta ya transfoma mnao humu na mnawajua. Uhujumu hauwezi kuwa wizarani tu, hata hapa upo,” alisema.
Katibu mkuu huyo alitoa agizo hilo, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano wa TANESCO, Abdul Mkama, kueleza kuna watu wachache wanaoharibu taswira ya shirika hilo ambao wanawajua kwa majina na wapo tayari kuwataja.
Mkama alikiri mbele ya watendaji wakuu wizarani kuwa, kwa makusudi wanaamini viongozi wa shirika hilo, wana nia ya kuliua ili wawaweke wawekezaji wa kufua umeme.
“Uwezo tunao lakini biashara na siasa haviendi pamoja ni sawasawa na kupenga kamasi huku unataka kupiga mluzi,” alisema Mkama.
Naye mfanyakazi Kamuri Malangwa wa Kituo cha Ufuaji Umeme megawati 100, alisema wawekezaji wanathaminiwa zaidi na serikali kuliko TANESCO kwa kuwa katika kutumia gesi, TANESCO inakuwa ya mwisho kuipata hadi Kampuni ya Symbion ipate ya kutosha na wengine.
“Mara nyingi tunaambiwa tuzime mitambo gesi haitoshi, ili wenye gesi wauze kwa makampuni mengine, matokeo yake kituo hiki kila siku kinatengeneza chini ya kiwango cha ufuaji wa umeme. Inafikia mahala sisi wenyewe tunavutana mashati, ili wengine watengeneze pesa,” alisema.
Alisema hivi sasa shirika hilo limekuwa machinga wa umeme, pamoja na kuwakaribisha wawekezaji, linanunua umeme senti 27 na kuuza kwa senti 11, lakini wengine wananufaika kwa kuwa wao ndio wanajua kutengeneza fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo kituo hicho kitafungwa muda si mrefu kwa kuwa hakuna fedha za kukarabati injini.
Naye Raison Mwambage, alisema IPTL imelalamikiwa kwa mikataba mibovu, mawaziri mbalimbali wameshapita katika wizara husika bila kurekebisha tatizo hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Muhongo alisema hivi sasa ni wakati wa vitendo, si wakati wa kusikiliza hotuba, risala wala sera kwa kuwa vimekuwa vikitolewa siku zote, lakini hakuna mabadiliko.
Waziri huyo alikiri wananchi kukabiliwa na maisha magumu baada ya kuletwa mitambo ya kuzalisha umeme, kwani dunia ni ya ushindani na hivyo anafahamu kuna watu wanaotengeneza fedha ambao wanakwamisha masuala ya umeme yasisonge mbele.
Waziri huyo alikiri kuwa mikataba mibovu huiyumbisha nchi na kwamba kinachofanyika sasa ni kuipitia na kuhakikisha mikataba mingine haitakuwa na tatizo.
Alisema mikataba yote itakayosainiwa sasa itakuwa ni ya wazi, na kusema kuwa hatasaini mikataba mibovu.
Alisema tatizo la umeme nchini linatokana na kutegemea chanzo kimoja cha maji na kusema kuwa ili TANESCO iendelee alishauri vyanzo vitakuwa makaa ya mawe, gesi asilia, umeme wa maji, jua, upepo na ule unaotoka ardhini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri anayeshughulikia Nishati, George Simbachawene alisema atatumia akili, uwezo na ujuzi alionao, ili nchi itoke kwenye tatizo hilo.
Naye Naibu Waziri anayeshughulikia Madini, Stephen Masele, alisema hawatasita kuwaondoa wote watakaokwamisha safari hiyo kwa kuwachukulia hatua.
No comments:
Post a Comment