DK. Harrison Mwakyembe, waziri mpya wa uchukuzi, yuko kitanzini na aweza kulazimika kujiuzulu wakati wowote kutoka sasa.
Gazeti hili limeambiwa kuwa Dk. Mwakyembe aweza kujiuzulu au hata kufukuzwa kazi kwa kuwa “amebebeshwa bomu.”
Bomu ambalo Mwakyembe anadaiwa kubebeshwa ni wizara iliyosheheni kinachoitwa “kashfa na miradi ya wakubwa.”
Rais Jakaya Kikwete alimteua Dk. Mwakyembe kuwa waziri wa uchukuzi katika mabadilko ya baraza la mawaziri yaliyofanyika wiki iliyopita.
Mbunge huyo wa Kyela, mkoani Mbeya alijipatia umaarufu mkubwa baada ya kuongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa Richmond.
“Huyu bwana ni kama vile ametegwa. Amekabidhiwa wizara ambayo kwa vyovyote vile, hatafika nayo mbali,” ameeleza mtoa taarifa.
Amesema, “Katika wizara yake ndiko kuna kampuni ya reli (TRL). Kuna Kampuni ya Ndege (ATCL). Kuna mamlaka ya bandari (TPA). Kote huko kuna mikataba yenye utata na wakati mwingine inahusishwa na wakubwa.”
Taarifa zinasema waziri huyo atatakiwa kuchagua moja kati ya mawili: kuwa mkali kwa kufuta au kurekebisha mikataba hiyo; au kusubiri kuchafuka kisha afukuzwe kazi.
Taarifa zinasema Dk. Mwakyembe ana kibarua kigumu cha kulikwamua shirika la reli la taifa (TRL) ambalo linakabiliwa na ukata mkubwa.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuteuliwa kuwa waziri kwamba, ataweza kuongea juu ya mikakati yake pale atakapokuwa ameapishwa.
Tayari menejementi ya TRL imeeleza wazi kuwa haina fedha za kujiendesha na kwamba injini na mabehewa ya treni vinafanya kazi lakini hayafanyiwi matengenezo.
Kwa njia hii, menejimenti imekiri, kunaweza kutokea ajali zitakazosababisha maafa makubwa kwa taifa.
MwanaHALISI limeelezwa na vyanzo vyake vya ndani ya serikali kuwa TRL liko taabani kifedha na linaweza kusitisha usafiri wa reli wakati wowote kuanzia sasa.
Hayo yameelezwa kwenye waraka maalum wa Menejimenti ya Mpito ya TRL, kwenda kwa serikali. Waraka ulilenga kutoa “taarifa ya uwezekano wa TRL kushindwa kutoa huduma ya usafiri wa reli katika muda mfupi ujao.”
Katika waraka huo, menejementi ya mpito imeeleza tayari imeanza kuacha mizigo ya wateja katika stesheni mbalimbali nchini kutokana na ukosefu wa mafuta.
“…TRL imefikia hatua ambayo upo uwezekano mkubwa wa kushindwa kutoa huduma za usafiri wa reli wakati wowote kuanzia sasa endapo hatua za dharura hazitachukuliwa mara moja,” waraka umeeleza.
Waraka huo unatoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Kipallo Kisamfu kwenda kwa serikali.
Waraka huo wa 23 Aprili 2012, umepelekwa kwa katibu mkuu Wizara ya Uchukuzi, Omar Chambo.
Mhandisi Kisamfu katika waraka huo, amemweleza Chambo kuwa kwa miezi miwili iliyopita, TRL imekuwa ikitumia fedha kidogo inazopata kununua tu mafuta kwa ajili ya treni za abiria, na kuacha za mizigo.
“Sasa hivi kuna treni za mizigo takribani 18… ambazo zimesimama Korogwe, Morogoro, Dodoma kwa sababu ya kukosa fedha ya kununulia mafuta ya dizeli,” amesema.
Kisamfu amemweleza Chambo kuwa TRL haina uwezo tena wa kununua mafuta ya kuendeshea treni wala kununua vipuri mbalimbali; hivyo kuna uwezekano wa kusimamisha huduma za usafiri wa treni wakati wowote.
Kwa mujibu wa waraka huo, Menejimenti ya Mpito TRL imeshafikisha suala hili serikalini lakini halijapatiwa ufumbuzi.
Badala yake, TRL imekuwa ikielekezwa kwenda kukopa au kutafuta mtaji wa biashara nje ya serikali ambako haikopesheki tena kutokana na wingi wa madeni.
Hadi sasa TRL inadaiwa Sh. 11 bilioni na baadhi ya wadai wameipeleka mahakamani, wakati waliobaki hawako tayari kuikopesha tena.
Menejimenti ya mpito ilikabidhiwa TRL, 26 Julai 2011 ikiwa haina fedha. Iliachwa katika hali hiyo na menejimenti ya RITES kutoka India ambayo ilikuwa imeingia ubia na serikali.
TRL iliyoanza kazi 1 Oktoba 2007, chini ya menejimenti ya RITES ilishindwa kujiendesha licha ya kuwa na mtaji wa wanahisa (serikali ya Tanzania na RITES) wa Sh. 20 bilioni na mkopo wa IFC wa dola za Marekani 44 milioni (Sh. 70 bilioni).
Mwezi Juni 2009, RITES iliwasilisha kwa serikali mpango wa miaka 10 wa kuiboresha TRL, wakiitaka iwatafutie mtaji wa dola za Marekani bilioni moja (Sh.1.6 trilioni).
Kwa mujibu wa Kisamfu, katika mpango huo TRL ingepata hasara ya dola za Marekani milioni 515 (Sh. 824 bilioni). Serikali ilikataa mpango huo na kuamua kuanza utaratibu wa kuirejesha TRL mikononi mwake.
Waraka huo umeonyesha kuwa hadi 30 Aprili 2010, wakati serikali inajadiliana na RITES jinsi ya kuachana katika ubia wa TRL, mtaji wa wanahisa ulikwishatumika wote na kuwaachia nakisi ya Sh. 78.4 bilioni.
Kutokana na utendaji huo usioridhisha, serikali iliamua kurudisha TRL mikononi mwake kwa kuchukua hisa zote asilimia 51 za RITES.
Kukwama kwa TRL kiuendeshaji, kunasababishwa na serikali kushindwa kutoa fedha hata zilizopitishwa na bunge katika bajeti ya shirika.
Mbali na miradi ya maendeleo, Menejimenti ya Mpito iliomba katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011-12, Sh. 63.7 bilioni kwa ajili ya mtaji wa kufanyia biashara (working capital), lakini serikali ilitoa Sh. 900 milioni tu.
Mhandisi Kisamfu amesema, “Kampuni hii hivi sasa inatembeza treni mbili tu za abiria kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na kusafirisha wastani wa tani 20,400 za mizigo kwa mwezi.
“Mapato ni madogo kwa wastani wa Sh. 2.53 bilioni kwa mwezi wakati matumizi yasiyoepukika ni Sh. 4.05 bilioni kwa mwezi. Hii ina maana kuwa TRL inazalisha madeni ya wastani wa Sh. 1.52 bilioni kwa mwezi,” umesema waraka huo.
Taarifa za ndani za kampuni hiyo zinaeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2012/13, matumizi ya kawaida yaliyopendekezwa kwa ajili ya TRL ni Sh. 76 bilioni badala ya Sh. 231 bilioni zilizoombwa. Hii ni pungufu kwa Sh. 208 bilioni.
TRL imetengewa Sh. 146 bilioni kwa ajili ya maendeleo, badala ya Sh. 318 bilioni zilizoombwa. Hii ni pungufu kwa Sh. 233 bilioni.
MwanaHALISI limeelezwa kuwa hali iliyoko TRL ni ileile iliyoko ATCL na bandarini; na kwamba “inatosha kuletea presha kwa Dk. Mwakyembe.”
No comments:
Post a Comment