Saturday, May 5, 2012

Yametimia

JK AWATUPA MKULO,NGELEJA,MAIGE,NUNDU NA DK MPONDA,ATEUA WATATU WAPYA,PROFESA MAGHEMBE,MKUCHIKA WAPONA MAKAMBA SIMBACHAWENE SASA MANAIBU. 

Neville Meena
RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua wapya watatu na manaibu 10 huku akiwaacha wanane.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amewapandisha manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wizara mawaziri wanane na manaibu waziri sita, huku mawaziri na manaibu waziri 22 wakibaki katika wizara zao za awali.

Kutokana na mabadiliko hayo, idadi ya mawaziri na manaibu wao sasa imeongezeka kutoka 50 katika baraza la awali hadi 55. Mawaziri kamili wameongezeka kutoka 29 hadi 30 huku manaibu waziri wakiongezeka kutoka 21 hadi 25.

Mawaziri ambao wameng’olewa na wizara walizokuwa wakiziongoza kwenye mabano ni Mustafa Mkulo (Fedha), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omar Nundu (Uchukuzi) na Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii).

Panga hilo la mabadiliko limewakumba pia Manaibu Waziri wawili, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athumani Mfutakamba (Uchukuzi).

Akitangaza baraza hilo Ikulu jana, Rais Kikwete alisema mabadiliko hayo yametokana na mjadala mkali ulioanzia bungeni baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba ametumia fursa hiyo kufanya marekebisho kadhaa ili kuimarisha utendaji wa Serikali.

“Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ile kulikuwa na mjadala mkali bungeni, lakini pia kwenye kikao cha wabunge wa chama na Waziri Mkuu (Mizengo Pinda), alinipa taarifa hiyo na wanasema mawaziri wote waliotajwa waondolewe,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Tumekaa kwa pamoja na kumwangalia kila mmoja na tuhuma zake, kwa Kiingereza tunasema ‘case by case’ na tukaona kwamba wawili kati yao tuwahamishie katika wizara nyingine lakini tukatumia fursa hiyo kufanya mabadiliko mengine kwa lengo la kuimarisha utendaji wa Serikali.”

Mawaziri wengine ambao walikuwa wakikabiliwa na shinikizo la kuondolewa madarakani ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe.

Mkuchika sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais – Utawala Bora wakati Maghembe amehamishiwa Wizara ya Maji akichukua nafasi ya Profesa Mark Mwandosya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, asiyekuwa na Wizara Maalumu.

Rais Kikwete alisema ameteua manaibu waziri wawili katika Wizara ya Nishati na Madini; mmoja atakayeshughulikia masuala ya nishati na mwingine madini.

“Kulikuwa na mjadala mkali kuhusu kutenganishwa kwa wizara hii ya nishati na madini, lakini tumeangalia kwamba kuunda wizara mpya katikati hivi halafu kuna masuala ya kibajeti, tukaona itatusumbua, hivyo tumeamua kuwe na manaibu waziri wawili halafu hayo mapendekezo mengine tukasema tuangalie mbele ya safari,” alisema.

Alisema uamuzi huo umezingatia ukubwa wa wizara hiyo na changamoto zake akisema nishati ni sekta inayokua hasa kutokana na kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi pia kuwapo kwa dalili za kupatikana kwa mafuta.

Alisema kwa upande wa madini, pia sekta hiyo imekuwa ikikuwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kwa miaka mitano mfululizo imekuwa ikishika nafasi ya pili katika kuliingizia taifa mapato, baada ya utalii.

Mbali na kuongezwa kwa naibu waziri katika wizara hiyo, Rais Kikwete pia ameteua manaibu waziri katika wizara ambazo awali hazikuwa na nafasi hizo.

Wizara hizo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Katiba na Sheria na Maliasili na Utalii.

Mawaziri wapya
Mawaziri wapya walioteuliwa na Wizara zao kwenye mabano ni Mbunge wa Handeni,  Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa Profesa  Sospeter Muhongo (Nishati na Madini).

Walioteuliwa kuwa Manaibu Waziri ni Mbunge wa Rufiji Dk Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (Nishati na Madini), Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Mbunge wa Mvomero, Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).

Wengine ni Mbunge wa Makete, Dk Binilith Mahenge (Maji), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Maselle (Nishati na Madini – Madini), Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (Katiba na Sheria) na Wabunge wa Kuteuliwa Janet Mbene na Saada Mkuya Salum  wote Fedha.

Naibu Mawaziri waliopandishwa na kuwa mawaziri kamili wamo, Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).

Kabla ya kuwa mawaziri kamili, Chiza na Dk Mukangara walikuwa Naibu mawaziri katika wizara walizopangiwa wakati Dk Mwakyembe alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Kaghasheki alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mawaziri wengine waliohamishwa kutoka wizara zao za awali ni, Celina Kombani kutoka Katiba na Sheria kwenda Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa Umma) ambako amechukua nafasi ya  Hawa Ghasia ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).

Shamsi Vuai Nahodha amehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambako amechukua nafasi ya Dk Hussein Mwinyi ambaye amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Dk Emmanuel Nchimbi amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuchukua nafasi ya Nahodha akitokea Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wakati Waziri wa Katiba na Sheria ni Mathias Chikawe ambaye alikuwa Ofisi ya Rais Utawala Bora.
Manaibu waziri waliohamishwa ni Charles Kitwanga ambaye amepelekwa Ofisi ya Makamu wa Rais akitokea Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Adam Malima ambaye amehamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika akitokea Nishati na Madini na Pereira Ame Silima ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha sasa anakuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Gregory Teu ambaye pia alikuwa Wizara ya Fedha amehamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara ambako anachukua nafasi ya Lazaro Nyalandu ambaye amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Gerson Lwenge, amehamishiwa Wizara ya Ujenzi, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Mwakyembe.

Waliobaki kwenye nafasi zao
Mawaziri waliobaki kwenye nafasi zao ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri  Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.

Pia wamo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka; Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Kwa upande wa Manaibu Waziri wamo Kassim Majaliwa (Ofisi  ya Waziri Mkuu, Tamisemi - Elimu), Aggrey Mwanry (Ofisi  ya Waziri Mkuu, Tamisemi), Dk Makongoro (Kazi na Ajira) na Benedict Ole-Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).

Wengine ni Mahadhi Juma Maalim ( Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa),  Goodluck J. Ole-Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Ummy Mwalimu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Dk Abdulla Juma Abdulla (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Uwajibikaji
Kuhusu uwajibikaji Rais Kikwete alisema baada mawaziri kuwajibika kisiasa, wanaofuta ni watendaji katika wizara na taasisi nyingine za umma ambao ndiyo chanzo cha mawaziri hao kuwajibika.

Alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa ambayo si yao na kwamba hivi sasa Serikali itaanza kuchukua hatua kwa watendaji wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika husika.

“Pamoja na kuwa na utaratibu huu mzuri wa kuwajibika kwa wanasiasa, sasa lazima tuwawajibishe hata hao wanaosababisha mawaziri hawa kujiuzulu, maana wakati mwingine wanawajibika kwa makosa ambayo si yao,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Kuna watu ambao kazi yao ni kupiga fitina tu … wao wana kazi ya kusema kaja hapa ataondoka kwani yeye ni nani bwana …… sasa watu wa aina hii hatuwezi kuendelea kuwavumilia hata kidogo, lazima hatua zichukuliwe kwa watendaji wakuu awe ni katibu mkuu wa wizara, ofisa mtendaji mkuu wa shrika la umma, mkurugenzi wizarani au hata bodi ambazo zinasimamia taasisi hizi.”

Mawaziri wapya na waliohamishwa wataapishwa keshokutwa Jumatatu kuanzia saa 5:00 asubuhi katika Viwanja vya Ikulu.

No comments:

Post a Comment