Wednesday, May 16, 2012

Mzee Makamba awarushia kombora Nape, Pinda


ASEMA NAPE ANAIGEUZA CCM MALI YAKE,PINDA YUKO MBALI NA WANANCHI, KINGUNGE PIA ACHARUKA
Midraji Ibrahim, Dodoma
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba ameibuka katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (Nec) na kumtuhumu Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kwamba amekigeuza chama kuwa mali yake binafsi.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zimesema kwamba Makamba alisema hatua ya Nape kugeuza chama hicho kama taasisi yake binafsi ndiyo ambayo imesababisha kikose mwelekeo.

Makamba licha ya kuelekeza mashambulizi yake kwa Nape, alimrushia pia kombora Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa ana uhusiano mdogo na wananchi.

“Mzee (Makamba) amesema hivi sasa CCM imekuwa kama jogoo anayepelekwa kwa mganga, kila anakoelekezwa ndo huko, hali hiyo ndiyo inakikumba CCM hivi sasa. Amemweleza Nape kuwa amegeuza chama kama mali yake binafsi, anafanya mambo nje ya utaratibu na anaangaliwa tu.”

Makamba alidai kuwa badala ya sekretarieti kushughulikia matatizo ya chama, imekuwa ikihangaika na watu kwa sababu ya kutofautiana nao misimamo na wakati huo wakijidai kuzika tofauti ili kukiimarisha.

Nape alipoulizwa kuhusu suala hilo alipuuza na kusema: “Si kweli, lakini ninyi andikeni tu maana tumewazoea.”

Alipotakiwa kueleza kama Kingunge na Makamba walisema nini dhidi yake katika kikao cha Nec alijibu: “Walikuwapo, lakini hakuna kati yao aliyenitaja hata kwa jina.”

Nape alitumia muda mwingi kulalamika kuwa taarifa nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa kutoka ndani ya mkutano huo uliomalizika jana zimetoka kwa watu aliowataja kuwa wana maslahi nazo binafsi na kuhoji,” Kwa nini msiwe mnasubiri taarifa rasmi (za chama) ili habari iwe ya ukweli zaidi?”

Mkongwe mwingine wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye anadaiwa kusikitishwa na vitendo vya rushwa na ugomvi vinavyoendelea ndani ya chama huku vikiangaliwa na viongozi kama vile vinakistawisha wakati vinakiporomosha.

Kingunge alidai kuwa hivi sasa chama hicho kimetawaliwa na matajiri ambao ndiyo wanaopata nafasi za uongozi na maskini wanawekwa kando.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja aliunga mkono suala la Pinda kuwa na uhusiano mdogo na wananchi na kwamba, amekuwa mkimya zaidi na hamsaidii Rais Jakaya Kikwete.

“Yule Mwenyekiti wa Shinyanga, amemweleza Pinda kuwa ng’ombe wakila mazao mtu wa kwanza kuchapwa viboko ni mchungaji, halafu mmiliki anatozwa faini baadaye. Hivyo, alitakiwa kuwajibika kwanza kabla ya mawaziri walioondolewa,” kilidokeza chanzo chetu.

Mgeja alidai kuwa uwajibishwaji wa mawaziri, haukuzingatia haki kwa sababu George Mkuchika, Profesa Jumanne Maghembe na Hawa Ghasia walilalamikiwa, lakini kilichofanywa ni kutoa kafara wengine na hao kubadilishiwa wizara.

Pia, inadaiwa kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwataka wajumbe kuzika tofauti zao ili kuweka msimamo wa pamoja kwa ajili ya ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015 na kwamba adui namba moja wa CCM hivi sasa ni Chadema.

Rushwa yakishtua chama

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema Nec imejadili changamoto zinazokikabili chama kwenye uchaguzi unaoendelea na kubaini kuwa rushwa imekithiri.

Nape alisema tishio la rushwa ni kubwa na mgombea atayakayethibitika kujihusisha na vitendo hivyo rushwa ataondolewa mara moja, huku viongozi na watendaji wakitahadharishwa kuchukuliwa hatua za nidhamu.

“Kwa kisingizio cha kuwasalimia wajumbe, kuwapa nauli au kujitambulisha. Mgombea atakayethibitika anazunguka au amezunguka ataondolewa bila kuchelewa katika orodha ya wagombea,” alisema na kuongeza:

“Kwa watendaji na viongozi wa chama ngazi zote kuanzia sasa ni marufuku kuwatembeza ndani ya maeneo yao, kwa nia ya kuwatambulisha kwa wapiga kura. Mtendaji au kiongozi atakayebainika anakiuka agizo hili, atachukuliwa hatua za nidhamu mara moja.”

Pia, Nape alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji na viongozi wa chama ngazi zote kuwaitia wagombea, wajumbe wa mikutano ya uchaguzi kwa lengo lolote, kwani vikao vya aina hiyo havimo katika katiba.

Alisema vikao vya aina hiyo ni haramu na vinapalilia rushwa na kuongeza kwamba wanachama wa CCM wanatakiwa kupiga vita rushwa na kutoa taarifa ya vitendo hivyo katika ofisi za chama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Aliitaka Takukuru kutomuonea aibu au kumuogopa mtu anayejihusisha na vitendo vya rushwa badala yake wamchukulie hatua.

Mishahara na chakula

Kuhusu mishahara ya watumishi wa umma na mfumuko wa bei ya chakula, Nape alisema Nec imeagiza Serikali kuhimiza waajiri kupandisha mishahara na malipo mengine kwa wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.

Alisema gharama za maisha zimepanda na mishahara inayolipwa haiendani na hali halisi. Alisema nayo Serikali inatakiwa nayo kupandisha mishahara kwa watumishi wake.

“Serikali idhibiti malipo ya huduma ya ndani kwa kutumia fedha za kigeni, hasa Dola ya Marekani. Pia, iongeze udhibiti wa maduka na hoteli zinazofanya biashara ya fedha za kigeni ili kuondoa hujuma kwa uchumi wa nchi inayofanywa kutokana na uhuru uliokithiri katika biashara hii,” alisema.

Nape alisema Serikali inatakiwa kuweka jitihada zaidi za kudhibiti ulanguzi wa bidhaa muhimu na upandishaji holela wa bei za vyakula, kodi za nyumba na usafiri.

Alisema Nec imeagiza Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na kati za kukabiliana na tatizo la mfumuko wa bei.

“CCM inaiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka na muda mfupi ikiwamo kuangalia upya baadhi ya kodi katika vyakula pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika sukari,” alisema Nape.

Pia, Nape alisema wameagiza Serikali kupitia upya utaratibu wa ruzuku ya mbegu na mbolea ili upanuliwe kunufaisha wakulima wengi.

Alisema Nec imeitaka Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mpango wake wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula nchini, hasa kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Nafaka ya Taifa (NFRA), ikiwamo kujenga maghala zaidi ya mazao ya chakula maeneo ya uzalishaji na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ununuzi wa mazao hayo.

“Wakati wa uhaba wa vyakula maeneo ya mijini, kasi ya kupeleka chakula maeneo hayo iongezwe na utaratibu mzuri zaidi wa usambazaji chakula utumike ili walaji na siyo wasafirishaji na wasindikaji, wanufaike,” alisema.

No comments:

Post a Comment