Monday, May 28, 2012
Kisumo: Ngeleja, Maige wanamdhalilisha rais
MWANASIASA mkongwe nchini, Peter Kisumo amehoji hatua ya mawaziri wawili waliong'olewa na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kuhusishwa na tuhuma za rushwa, kupokelewa majimboni kwao kama mashujaa.
Kauli hiyo ya Kisumo ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa CCM, imekuja kipindi ambacho kumekuwa na utaratibu kwa baadhi ya watu kufanya sherehe na kupokelewa kama mashujaa baada ya kujiuzulu au kung'olewa.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Kisumo alisema kitendo kilichofanywa na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Ezekiel Maige wa Maliasili na Utalii, kupokelewa kama mashujaa ni kumdhalilisha rais.
Kisumo alisema kama CCM kingekuwa na Kamati ya Maadili iliyo hai ilipaswa kuwaita wabunge hao na kuwahoji juu ya kitendo hicho.
"Siamini kama mapokezi yao hayakuwa na mkono wao, siamini hata kidogo..., kama kamati yetu ya maadili ingekuwa hai lazima ingewaita wajieleze," alisema Kisumo.
Alisema kama CCM na Serikali yake itaacha utamaduni huo uanze kujengeka katika jamii wa kuwapokea kishujaa viongozi waliondolewa madarakani kwa kuhusishwa na vitendo viovu, itakuwa ni jambo la hatari kwa mustakabali wa nchi.
Kisumo alisema hata mapokezi ya kishujaa waliyopewa Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa zamani wa Miundombinu, Andrew Chenge yalikuwa si sahihi na ni kumweka rais na serikali katika majaribu makubwa.
"Yeye rais anasimamia suala la maadili, watu wengine wanaona ni kero, hapa kuna tatizo kubwa la kimaadili... tukifika mahali wananchi hawaoni rushwa na ufisadi kama ni dhambi na wanawapokea kama mashujaa, ni jambo la hatari," alionya.
Alisema kuondolewa kwa mawaziri hao kuliridhiwa na vikao vya juu ndani ya CCM na serikali, hivyo wananchi katika majimbo yao kuwapokea kishujaa kunatia mashaka kama viongozi hao hawakushiriki kuwahamasisha kufanya hivyo.
"Haiwezekani kijana mdogo kama Ngeleja umepata uwaziri katika umri mdogo unaondoshwa unaanza kufanya wana CCM jimboni wanung'unike kana kwamba umeonewa, kwani rais alipokuchagua aliwaconsult (aliwaomba ushauri) wananchi waliokupokea kishujaa? "alihoji Kusumo.
Kwa mujibu wa Kisumo, kwa hali inayoendelea sasa ni kama CCM imenyimwa haki yake kukabiliana na ukiukwaji wa maadili kwa wanachama wake, na hata jitihada inazozifanya hazionekani waziwazi kwa wananchi.
"Suala la kufikiri usimamiaji wa maadili ya viongozi ni lazima kuwe na ushahidi kama wa kimahakama, ni udhaifu na lazima viongozi wetu sasa wajue chama kinahitaji dhamira ya kweli katika hili," alisema.
Kudhibiti fedha chafu
Katika hatua nyingine, CCM kimetangaza rasmi kuanzisha kampuni za biashara na kuimarisha mapato kwenye miradi yake ili kuwa na nguvu ya kifedha na hivyo kujiepusha na fedha chafu zinazoweza kutoka kwa wafadhili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisi ndogo za CCM Lumumba, Kisumo alitangaza mpango huo ambao sasa chama kitajikita katika kufufua vitega uchumi vyake.
“Kuna wafadhili ambao wamekuwa wakiichangia CCM na Chadema hadharani kama akina Sabodo, lakini wako wengine wanachangia kwa siri, sasa kuna hatari ya kupokea fedha chafu kutoka kwao,” alionya Kisumo.
Alisema chama hicho kinahitaji fedha lakini siyo fedha chafu ambazo zimepatikana kwa kukwepa kodi.
Hata hivyo, alisema, “Tunawashukuru watu marafiki ambao wamekuwa wakikisaidia chama.”
Kisumo aliongeza kusema,"Tunahitjai fedha lakini hatuhitaji fedha chafu tunataka fedha zitakazopatikana kwa uwazi na sio kama kampuni fulani (anaitaja) inakupa fedha ili uipe upendeleo."
Alisema ili kuondokana na utegemezi, chama hicho kitafungua kampuni zake na kuingia ubia na kampuni nyingine za kitaifa na kimataifa.
“Kampuni hizo zitakuwa huru kufanya biashara kwa kufuata sheria na kanuni huku zikiwa chini ya wadhanimi, lakini utendaji wake hautaingiliwa na chama,” alisema.
Alisema pia chama hicho kinataka kuimarisha usimamizi wa mapato kwenye miradi yake iliyoko kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Kisumo alisema kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa mwaka 2007, chama hicho kina miradi yenye thamani ya Sh 57 bilioni lakini mapato yake ni madogo ilikinganishwa na thamani ya miradi.
“Tunataka kuimarisha usimamizi kwenye miradi ya chama ili kuongeza mapato,” alisema Kisumo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema miradi ina thamani kubwa lakini, inashindwa hata kulipa mishahara badala yake baadhi ya mikoa inapelekewa ruzuku.
Kisumo alisema chama hicho hakiwezi kuendelea kuwategemea wafadhili kwani, kuna uwezekano mkubwa wa kupokea fedha chafu.
“Wako marafiki wanaoweza kutupatia fedha walizozipata kihalali, lakini wakataka upendeleo fulani, pia wapo wengine ambao wanaweza kutupatia fedha ambazo zimepatikana kwa njia zisizo halali, hizo zote ni chafu hatuzihitaji,” alisema Kisumo.
Alisema utaratibu huo wa kuanzisha miradi badala ya kutegemea ada za wanachama na wafadhili, wamejifunza kutoka Msumbiji, Afrika Kusini na Namibia.
“Chama cha Swapo Namibia, ANC cha Afrika Kusini na Frelimo cha Msumbiji vyote vinamiliki kampuni na kuendesha biashara. Hawategemei ada za wanachama wala wafadhili kama sisi, ingawa sisi ni wakongwe kwao imebidi tujifunze kutoka kwao,” alisema Kisumo.
Mwenyekiti huyo alisema michango ya wanachama bado ni midogo ambayo haiwezi kukiendesha chama hicho.
Alisema kwa siasa za hivi sasa, chama hakiwezi kujiendesha kwa kutegemea ada za uanachama pekee yake.
Alipoulizwa CCM itawezaje kuendesha miradi wakati ilishindwa kuendesha shirika lake la uchumi (Sukita), Kisumo alisema katika kipindi hicho mashirika mengi yalikufa kwa sababu ‘yalidekezwa’ na serikali.
“Mashirika yale yakitetereka kidogo yalikuwa yanapata fedha kutoka hazina, sasa hivi utapata wapi, ndiyo maana tukianzisha tunaweka waendeshaji wenye sifa kibiashara,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment