• Mgeja ataka ang’olewe kama mawaziri wengine
BAADA ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kunusurika kung’olewa Bungeni, jinamizi hilo limeendelea kumwandama ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), mjini Dodoma, Tanzania Daima limebaini.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichomalizika jana mjini Dodoma zilidai kuwa baadhi ya wajumbe wa NEC waliibua hoja ya kumtaka Pinda apime uzito wa tuhuma zinazomwandama Bungeni na achuke hatua za kuwajibika.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa Pinda kwa kuibua hoja ya kumtaka naye ang’atuke.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mgeja akichangia ajenda ya hali ya kisiasa ndani ya chama hicho, alisema haoni sababu ya Waziri Mkuu kutowajibika wakati mawaziri wake wamewajibika, tena wengine si kwa makosa yao bali ya uzembe uliosababisha na watendaji wao.
Mgeja ambaye mara kwa mara amekuwa akiwashambulia viongozi wake wa juu bila woga, alisema Pinda anapaswa kuwajibika kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali ulioainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Huku akiungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa NEC kwa kupiga makofi, mwenyekiti huyo alisema CCM inapakwa matope kwa makosa ya viongozi wa serikali kutowajibika na kusisitiza kuwa Pinda anapaswa kupima uzito wa hoja kwani ndiye kiranja wa mawaziri waliong’olewa kwa tuhuma za ufisadi.
Alihoji kuwa kama mawaziri nane wameng’olewa kutokana na ripoti ya CAG na shinikizo la wabunge wakiwemo wa CCM kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Pinda, Waziri Mkuu huyo hana uhalali wa kubaki madarakani akaendelea kuaminika.
Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya kikao hicho, alisema Mgeja alitoa mfano wa ufisadi wa mamilioni ya fedha unaofanywa na watendaji katika wilaya za mkoa wake kupitia vocha ya pembejeo kwamba ni wa kutisha, na alishatoa taarifa kwa waziri mkuu ambaye hakuzifanyia kazi hadi sasa.
Hoja hiyo iliungwa mkono Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye alimlipua Waziri Mkuu Pinda kwamba hana mawasiliano mazuri na serikali.
Alisema haridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo kwani ni rahisi kumpata Rais kuliko waziri mkuu, jambo ambalo alisema halileti tija kwa serikali.
Mjumbe mwingine aliyekosoa utendaji wa Pinda ni mkongwe Kingune Kombare Mwiru ambaye alimtaka mtendaji huyo kufanya kazi kwa kujiamini ili kurejesha imani ya wananchi kwa CCM iliyoanza kupotea.
Habari zinasema kuwa wakati Pinda akishambuliwa na kutakiwa kujiuzulu, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete, na Pinda mwenyewe, hawakujibu chochote.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua wapya watatu na manaibu 10 huku akiwaacha wanane.
Rais Kikwete alisema mabadiliko hayo yametokana na mjadala mkali ulioanzia bungeni baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba ametumia fursa hiyo kufanya marekebisho kadhaa ili kuimarisha utendaji wa serikali.
Katika mjadala huo Bungeni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alikusanya saini za wabunge 76 kwa lengo la kuwasilisha hoja ya kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Pinda endapo mawaziri waliotuhumiwa na CAG, wasingejiuzulu nyadhifa zao.
Mawaziri waliong’olewa na wizara walizokuwa wakiziongoza kwenye mabano ni Mustafa Mkulo (Fedha), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omar Nundu (Uchukuzi) na Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii).
Panga hilo la mabadiliko limewakumba pia Manaibu Waziri wawili, Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk. Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).
Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwapandisha manaibu waziri wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wizara mawaziri wanane na manaibu waziri sita, huku mawaziri na manaibu waziri 22 wakibaki katika wizara zao za awali.
Mawaziri wengine ambao walikuwa wakikabiliwa na shinikizo la kuondolewa madarakani ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika, na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe.
Mkuchika sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais Utawala Bora wakati Maghembe amehamishiwa Wizara ya Maji akichukua nafasi ya Profesa Mark Mwandosya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais, asiyekuwa na Wizara Maalumu.
Kutokana na mabadiliko hayo, idadi ya mawaziri na manaibu wao sasa imeongezeka kutoka 50 katika baraza la awali hadi 55. Mawaziri kamili wameongezeka kutoka 29 hadi 30 huku manaibu waziri wakiongezeka kutoka 21 hadi 25.
Katika hatua nyingine, NEC imekiri kukithiri kwa vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM taifa Nape Nnauye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Nape alisema imebainika kuwa vitendo vya rushwa ndani ya CCM vimeota mizizi hususan wakati wa uchaguzi, jambo ambalo limesababisha kupatikana viongozi wabovu.
“Tishio la rushwa ndani ya chama siyo ndogo, rushwa inaonekana kuchukua kasi kubwa na kutokana na hali hiyo, NEC imechukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo,” alisema Nape.
Alisema NEC imeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuhakikisha inapambana na watoa au kupokea rushwa.
“TAKUKURU tumeitaka kuhakikisha inapambana na vigogo wote ndani ya CCM ambao wanatoa au kupokea rushwa wakati wa kipindi cha uchaguzi, chama kinaagiza kuwa asionewe aibu mtu yeyote kwa kuangalia cheo, urefu rangi au fedha zake…..,” alisema.
Msemaji huyo wa chama alitoa angalizo kuwa endapo CCM itaendelea kuwakumbatia viongozi wanaotaka madaraka kwa kutoa rushwa, kitaiweka nchi rehani.
Kwa mujibu wa Nape, kuanzia sasa ni marufuku kwa mgombea wa ngazi yoyote kuzunguka matawini, kwenye kata, wilaya na mikoa kwa lengo la kukutana na wa mkutano wa uchaguzi kwa kisingizio cha kuwasalimia.
Pia chama hicho kimezuia viongozi wao wa ngazi zote kuwatembeza wagombea ndani ya maeneo yao kwa nia ya kuwatambulisha kwa wapiga kura.
NEC pia imeiagiza serikali kuhakikisha inachukua hatua za haraka kudhibiti mfumko wa bei ya vyakula pamoja ununuzi holela wa huduma kwa dola ili kuwapunguzia ukali wa gharama za maisha wananchi.
Alisema kutokana na kuwepo kwa mfumko wa bei ya vyakula, NEC imeiagiza serikali kuhakikisha inafanya juhudi za haraka kutatua tatizo hilo.
Nape alisema kutokana na hali mbaya ya maisha kwa Watanzania, NEC imetoa maagizo kwa serikali ambayo yakitekelezwa yatarejesha imani na matumaini kwa Watanzania waliopoteza imani na chama hicho.
Aidha chama hicho kimeitaka serikali kuongeza uthibiti wa maduka na mahoteli yanayofanya biashara za fedha ya kigeni ili kuondoa hujuma kwa uchumi wa nchi inayofanywa kutokana na uhuru uliokithiri katika biashara hiyo.
Alisema pia waajiri wahimizwe kupandisha mishahara na malipo mengineyo kwa wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.
No comments:
Post a Comment