Tuesday, May 22, 2012

Lema ataja ‘wazito’ wanaoenda CHADEMA

•  Yumo Waziri Mkuu wa zamani 
 
WAZIRI mkuu mmoja wa zamani na mawaziri wawili walioko madarakani, wametajwa kuwa miongoni mwa wazito walioko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Aidha, mawaziri hao wanasubiri muda muafaka ufike waweze kutangaza rasmi kujiunga na chama hicho, kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa na mwenendo mzima wa uongozi na utendaji wa mambo unavyokwenda serikalini na ndani ya CCM, hususan suala la kuwalinda watu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu.
Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbelss Lema aliwataja ‘wazito’ hao, kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika mjini Sengerema juzi, ambapo alisema hatua hiyo ni ishara wazi ya kuanguka kwa chama hicho.
Katika mkutano huo, uliofanyika katika viwanja vya Mnadani vilivyobatizwa jina la Uwanja wa Wenje, Lema pamoja na mbunge wa Nyamagana, Wenje walisema wananchi wengi wakiwemo baadhi ya viongozi wenye uchungu na taifa hili ndani ya CCM, hawafurahishwi na ubadhilifu wa mali za nchi, na kwamba hatua hiyo imewadidimiza Watanzania katika lindi kubwa la umasikini, kutokana na kubariki madini, wanyama, misitu, samaki na rasilimali nyinginezo kuuzwa nje ya nchi kwa maslahi ya vigogo wachache.
Katika mkutano huo ambao zaidi ya wanachama 100 wa CCM walijiunga na CHADEMA, wabunge hao waliishambulia serikali wakidai imekuwa kinara wa ombaomba duniani, wakati taifa lina rasilimali nyingi zinazotumiwa na wachache kufanya ziara za mara kwa mara ughaibuni.
Lema aliuambia umati huo wa watu kuwa kama walivyoamua kuchukua maamuzi mawaziri hao, nao wanatakiwa kuihukumu sasa CCM na serikali yake kwa kujiunga na CHADEMA, kwani kufanya hivyo ni kujiandaa na kile alichokisema ukombozi wa taifa mwaka 2015.
“CHADEMA tumejiandaa kuingia madarakani kwa kutumia nguvu ya umma. Ndiyo maana (akawataja mawaziri) wameomba kujiunga na CHADEMA ili tulisongeshe pamoja kwenda kuingia madarakani mwaka 2015.
“Lakini (akamtaja waziri mwingine) tumemkataa. Tunataka wachapa kazi na wenye mioyo ya kweli katika mapambano ya kupigania haki na kuondoa dhuluma kwa Watanzania,” alisema Lema.
Awali, aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Nyampulukano, Hamisi Mwagao Tabasamu, ambaye hivi karibuni alihamia CHADEMA, aliwaambia wananchi hao wa Sengerema kwamba, halmashauri ya wilaya hiyo imegubikwa na tuhuma za ufisadi, hivyo viongozi wawili waandamizi wanastahili kushtakiwa mahakamani.
“Halmashauri hii ya Sengerema kuna ufisadi mkubwa. Kuna fedha nyingi sana za miradi zimeliwa na ushahidi ninao, TAKUKURU kama mpo hapa na Usalama wa Taifa njooni mnikamate Jumatatu kama mnadhani ni uongo,” alisema Tabasamu ambaye anadaiwa kuivuruga kabisa CCM wilayani Sengerema.
Alisema, anao ushahidi wa mamilioni ya fedha za miradi katika eneo la Bukala, zinazodaiwa kutafunwa kwa mgongo wa mafunzo jijini Mwanza, na kwamba wananchi wa Sengerema waanze kubadilika na kuikataa CCM kwani viongozi wake hawawasaidii katika kutatua kero zao za maji, afya, barabara na miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Wenje aliwataka wananchi wa Sengerema kuhakikisha wanaanza kuikataa CCM mapema, kwani bila kufanya hivyo miaka michache watakuwa watumwa wa kupelekwa Ughaibuni kulima mashamba ya wakoloni.
“Wananchi wa Sengerema nawaambieni leo kwamba, viongozi wenu wa serikali wanauza kila kitu sasa. Twiga wanauzwa, tembo wanauzwa, misitu, madini navyo vinapigwa mnada kwa Wazungu,” alisema.
Alisema, ufisadi, kukumbatia wawekezaji wa nje pamoja na mikataba mibovu ndiyo inayoiweka Tanzania katika hali ya umasikini kiasi kikubwa, huku akimtaja mbunge mmoja wa CCM (jina linahifadhiwa), kwamba amepata utajiri mkubwa kuliko wa marais wawili wa zamani, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Aliwaomba wananchi hao kushinikiza katiba mpya ijayo Tanzania iongozwe kwa mfumo wa majimbo kama ilivyo huko Bara la Ulaya, kwa madai kuwa utarudisha mamlaka na utawala kwa wananchi, kuliko ilivyo sasa ambapo viongozi wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wanawajibika kwa rais.
 

No comments:

Post a Comment