Kwirinus Mapunda, Songea
MKANDARASI mmoja wa Manispaa ya Songea,
Ruvuma (jina tunalihifadhi) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa
tuhuma ya kumpiga risasi askari polisi na kumvunja miguu yote miwili.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Ruvuma, George Chipos alimtaja askari
aliyepigwa risasi kuwa ni Lucas Komba ambaye kituo chake cha kazi ni
Mkoa wa Tabora. Alikuwa hapa kwa mapumziko na kwamba tukio hilo
lilitokea Mei, 20 mwaka huu saa 2.45 usiku katika grosari iliyopo
Seedefarm Barabara ya Namtumbo.
Chipos alisema mkandarasi huyo
aliyepewa kazi ya kutengeneza Barabara za vijijini, alimpiga risasi
askari Komba mwenye No.E 9507 PC kutokana na kile kinachodaiwa ni
mtuhumiwa kulewa kupita kiasi hivyo kuanza kufyatua risasi hewani bila
utaratibu.
Alisema askari Komba alishambuliwa baada ya kujaribu
kumzuia. Alimfyatulia risasi miguuni na kumpiga sehemu ya paja la mguu
wa kushoto.
Kaimu kamanda huyo alisema askari Komba amelezwa
katika Hospitali ya Mkoa Ruvuma akipatiwa matibabu na mtuhumiwa
atapandishwa kizimbani baada ya upelelezi kukamilika.
Katika
tukio jingine: Watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji
ya mtu mmoja, Esau Kapinga yaliyotokea katika Kijiji cha Mkumbi Wilaya
ya Mbinga, Ruvuma. Marehemu aliuawa kwa kukatwakatwa kwenye goti la
kulia na kupigwa na kitu kizito mgongoni.
Kamanda Chipos alisema
tukio hilo lilitokea Mei 21, mwaka huu saa 7:00 usiku na kuwa chanzo
chake ni ugomvi wa kifamilia wa kugombea mashamba ya kahawa. Alisema
watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment