Wednesday, May 16, 2012

Kitimtim JWTZ, Jeshi la Polisi

SIKU moja baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Nchini (NIDA) kuwalipua askari polisi 700 na askari 248 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi, (JWTZ) kutumia vyeti vya kughushi, taasisi hizo zimetangaza vita vya kuwasaka waliohusika na tuhuma hizo ili wachukuliwe hatua.
Katika kushughulikia suala hilo, taasisi hizo za ulinzi zimeunda timu maalumu kufanya uchunguzi wa kina juu ya suala hilo, huku JWTZ ikisisitiza kuwa haitasita kumwajibisha askari yeyote atakayenaswa na kashfa hiyo bila kujali wadhifa alionao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe, alisema jeshi hilo limeanza uchunguzi dhidi ya madai hayo ili kubaini ukweli na kisha kuchukua hatua.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za Majeshi ya Ulinzi hususan aya ya 8.26.(1)(c), mwanajeshi anayegundulika kudanganya katika taarifa anazotoa wakati wa kujiunga na jeshi, atashtakiwa katika mahakama za kijeshi na akipatikana na hatia atapewa adhabu kali zinazoambatana na kufukuzwa kazi.
“…Hilo sasa kwa mujibu wa kanuni hii ya 8.26.(1)(c) hakuna mzaha hata kama ulikuwa na PhD lazima ujibu hoja, lazima ujibu hoja kwa sababu ulidanganya. Kwa hiyo sisi hatujali hata kama utakuwa ulisonga mbele, hata kama umefikia kama mimi, lazima ushtakiwe na mahakama za kijeshi.
“Ukipatikana na hatia adhabu kali lakini inayoendana na kuachishwa kazi na pengine haki zote uzikose ambazo zilipatikana pengine katika kipindi chote ulichoingia jeshi. Hiyo haijalishi kwamba ulijiendeleza na kufikia hivi…,” alisema Kanali Mgawe.
Hata hivyo msemaji huyo alisema kwamba ni mapema mno kwa sasa kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo.
Alisema jeshi hilo litashiriki na NIDA kufuatilia waliotuhumiwa kughushi vyeti hivyo na nyaraka mbalimbali na kwamba utaratibu huo ni endelevu kutokana na unyeti wa taasisi hiyo.
Alikiri kwamba taarifa hizo za Nida ambazo alisema kwa mara ya kwanza wamezisikia kupitia vyombo vya habari jana, zimewashtua na kwamba wameanza kulishughulikia suala hilo ingawa wamekuwa wakifuatilia mambo hayo mara kwa mara.
Alikiri pia kwamba mambo hayo yamekuwa yakijitokeza mara nyingi na alipoulizwa hadi sasa jeshi hilo limewawajibisha askari wangapi, alisema ni vigumu kufahamu idadi kamili lakini kifungo hicho kiliwekwa kwa madhumuni mengi.
“Sina idadi kamili pengine katika utumishi wangu sijawahi kushuhudia mtu akifanyiwa hivyo lakini naamini siku za nyuma pengine hayo yalikuwepo,” alisema Kanali Mgawe.
Alipoulizwa utaratibu wanaoutumia kuajiri watu alisema awali walikuwa wakitumia vyeti lakini hivi sasa wamekuwa wakiwatumia wadau mbalimbali ikiwemo Tume vya Vyuo Vikuu (TCU)na wengine.
“Tumekuwa tukichukua hatua kadiri teknolojia inavyokua… Hata hivyo kadiri teknolojia inavyobadilika na vitu pia vinabadilika na vijana wa kileo wanakuwa na uelewa wa haraka kuhusu mambo mbalimbali,” alisema msemaji huyo wa JWTZ.
Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Advera Senso alisema jana kuwa timu inayochunguza kashfa hiyo kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo, inawahusisha maofisa mbalimbali kutoka Kamisheni ya Utawala na Operesheni na Upelelezi.
Alisema kwamba kutokana na suala hilo kulihusisha jeshi hilo, miiko na taratibu za kijeshi zitafuatwa katika kulipatia ufumbuzi.
Alipoulizwa timu hiyo inaanza kazi lini, Senso alisema tayari kazi imeshaanza tangu jana na watatoa taarifa kwa umma baada ya kuikamilisha.
Juzi Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ilitangaza kubaini zaidi ya polisi 700 na wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) 248 wakiwa wameghushi vyeti vya shule.
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu, alisema sababu hiyo na nyingine ndizo zilizochangia kuchelewa kutoa vitambulisho hivyo vilivyotarajiwa kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwezi huu.
Kutokana na udanganyifu huo, Maimu alipendekeza kiundwe chombo maalumu cha kuchunguza hali hiyo.
Maimu alitaja sababu nyingine ya kuchelewa kwa vitambulisho hivyo kuwa kulitokana na mabadiliko makubwa katika mfumo wa daftari la kielektroni la anuani za makazi na simbo za posta na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kutokana na changamoto hizo, alisema mamlaka hiyo imeona ni busara kuzindua mradi ukiwa tayari umetatua changamoto hizo jambo ambalo litachukua zaidi ya miezi miwili au pungufu.
Alisema serikali imeamua kuwa vitambulisho vya taifa vitolewe sambamba na uandikishaji wa wapigakura ili kupunguza gharama kwa serikali na usumbufu unaoweza kutokea kwa kuita watu walewale kujiandikisha mara nyingi ndani ya kipindi kifupi.

No comments:

Post a Comment