Friday, September 9, 2011

Bosi utoroshaji twiga atoweka

Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi
  • Aliomba akale Idd Dar, ‘akachupa’
  • Wakubwa wahofu kuzungumza
MTUHUMIWA wa kwanza katika kesi ya utoroshaji nje ya nchi wanyama pori hai 136 wa aina 14 tofauti, wakiwemo twiga wanne, Kamran Ahmed (29), aliyekuwa nje kwa dhamana, ametoweka nchini na inasadikiwa amekwenda kwao Pakistan, Raia Mwema limefahamishwa.

Habari zinasema kuna mazingira tata ya kutoweka kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa nje kwa dhamana yenye masharti ya kutosafiri nje ya mikoa ya Kilimanjaro ilikofunguliwa kesi dhidi yake na watuhumiwa wengine, na Mkoa wa Arusha alikokuwa akiishi.

Taarifa zinasema, Kamran anaweza kuwa aliondoka nchini Agosti 31 kwa ndege ya Shirika la Emirates; huku akiacha nyuma maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuhusu hatma ya kesi iliyokuwa ikiwakabili yeye na washirika wake watano.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Makahama ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, Juni 11 mwaka huu, kwa tuhuma za kusafirisha na kutorosha nje ya nchi wanyamapori hai 136 wa aina 14 tofauti wenye thmani ya Shilingi 170,572,000.

Kamran na wenzake walifikishwa mahakamani baada ya kusuasua kwa upelelezi kuhusu kesi hiyo hadi taarifa za hujuma hiyo zilipofichuliwa kwa mara ya kwanza na Raia Mwema katika moja ya matoleo yake ya mwezi Mei kuhusu kutoroshwa nje ya nchi kwa wanyamapori hao.

Baada ya kufunguliwa kesi, Kamran alisomewa mashitaka sita tofauti yakiwamo ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha na kuuza nje nchi wanyamapori hao ambao ni nyara za Serikali.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jane Mbogo (33) ambaye ni raia wa Kenya, Hawa Hassan Mangunyuka (51), Mkurugenzi wa kampuni ya HAM Marketing ya Jijini Dar es Salaam, Afisa Mifugo katika uwanja wa ndege wa KIA, Martin Kimati (58), Veronica Benno (51) na Locken Kimaro (50) ambao wote ni maafisa usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mtuhumiwa huyo, hata hivyo, aliachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu, Kanda Moshi, kwa masharti ya kusalimisha hati yake ya kusafiria na pia asitoke nje ya Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro hiyo ikitokana na hatua ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi, Mkoa wa Kilimanjaro, kukataa kutoa dhamana kwa maelezo kuwa kesi za uhujumu uchumi hazina dhamana kisheria. Kamran alikuwa anatetewa na wakili wa kujitegemea wa mjini Arusha, Medium Mwale.

Mwale mwenyewe alifikishwa mahakamani mwanzoni mwa Agosti akituhumiwa kwa usafirishaji fedha haramu akiwa amekamatwa na kiasi cha shilingi bilioni 18 katika akaunti yake ambazo alishindwa kuzitolea maelezo. Mwale bado anashikiliwa katika Gereza la Kisongo, nje kidogo ya mji wa Arusha, akisubiri hatma ya kesi yake.

Taarifa zilizolifikia Raia Mwema, mwishoni mwa wiki, zilieleza kuwa Kamran aliondoka nchini Agosti 31 kwa ndege ya Shirika la Emirates na kurudi kwao Pakistan akipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere, Dar es Salaam akiambatana na kaka yake na mshirika wake wa biashara, Norman Ahmed, ama maarufu kama Nommy.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, wawili hao walitua Karachi, mji mkuu wa Pakistan, Septemba Mosi mchana, na taarifa kutoka kwa watu wao wa karibu zinadai kuwa hawatarajiwi kurejea nchini katika kipindi hiki ambacho kesi inayomkabili Kamran itatajwa tena Jumatatu (Septemba 12, 2011).

Taarifa za kuondoka nchini kwa mtuhumiwa huyo hadi sasa zinatatanisha kwani habari zisizothibitishwa zinaeleza ya kuwa aliondoka baada ya kupewa ruhusa na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro ama ruhusa maalumu ya mahakama baada ya hati yake ya kusafiria kushilikiliwa na kwamba ruhusa hiyo ilikuwa ni kwenda Dar es Salaam kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitr.

Taarifa zinadai kuwa, mara ya mwisho mtuhumiwa Kamran na ndugu yake walionekana katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) Obadia Jonas Nselu, kati ya Agosti 25 na 26, na inadaiwa kuwa baada ya majadiliano marefu waliweza kuwashawishi kurudishwa kwa hati ya kusafiria.
“Kuna uwezekano kuwa waliofanikisha mpango wa mtuhumiwa huyo kurudishiwa hati yake ya kusafiria walikuwa wamepewa malipo “rushwa” maana haiwezekani kama mtuhumiwa alikuwa anasafiri kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya sikukuu ya Idd basi apewe hati hiyo….hati za kusafiria ni kwa safari za nje ya nchi tu,” alieleza mtoa taarifa wetu.

Habari zaidi kutoka kwa watu walio karibu na mtuhumiwa huyo zinadai kuwa Kamran alifikia uamuzi wa kuondoka nchini baada ya kuona kuwa mwelekeo wa kesi ni mbaya kwake; hasa baada ya taarifa kwamba Serikali ilikuwa imeunda timu mpya ya wapelelezi kukusanya ushahidi zaidi wa kesi hiyo.

Raia Mwema imefahamishwa ya kuwa timu hiyo ilifanya kazi kwa umakini na kufichua mtandao uliokuwa ukifanya biashara hiyo haramu kwa muda mrefu, ukiwahusisha baadhi ya maafisa wa juu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na ushahidi huo ulikuwa msingi mkuu wa kesi iliyokuwa inamkabili mtuhumiwa huyo.
Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo pia alikuwa ametishwa sana na ‘moto’ uliowaka Bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa wabunge wote waliotoa michango yao kumbana Waziri wa Wizara hiyo, Ezekiel Maige, kutoa majibu kuhusu wanyama hao waliotoroshwa nje ya nchi.

Wabunge pia walifikia uamuzi wa kutaka iundwe kamati maalumu ya kufuatilia wanyama hao ambao wanadaiwa kutoroshwa kwenda Doha nchini Qatar kwa kutumia ndege ya jeshi la anga la nchi hiyo.
Katika kujibu hoja za wabunge Waziri Maige aliwaeleza kuwa pamoja na kuwafungulia watuhumiwa wote kesi ya uhujumu uchumi Serikali pia ilimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Obeid Mbangwa na watumishi wengine wawili, kupisha uchunguzi unaofanyika.

“Ni mlolongo wa matukio hayo makubwa yaliyotokea ndani ya mwezi Agosti ndiyo yanayotajwa kuwa yalimtisha sana Kamran kiasi akahisi ya kuwa kesi iliyokuwa inamkabili ni ngumu, hali iliyomfanya afikie uamuzi wa kuondoka nchini lakini kwa kutumia ushawishi wa kurudishiwa hati yake ya kusafiria,”anaeleza mtoa habari wetu.

Anaongeza mtoa habari wetu: “ Kuna uwezekano pia mpango wa kuondoka kwa Kamran uliratibiwa na baadhi ya maafisa wa juu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambao tuhuma za usafirishaji wanyama zimewagusa, lengo likiwa ni kuvuruga kesi iliyoko mahakamani kwa kuwa upande wa mashitaka utakuwa umeyumbishwa na kuondoka kwa mtuhumiwa namba moja.”

Akizungumzia yaliyojitokeza katika sakata hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuf Ilembo alieleza kuwa hana taarifa za kuondoka nchini kwa mtuhumiwa huyo wala hawajawahi kutoa ruhusa kwake ya kuondoka kwenda popote.

“Unajua suala hilo lilikuwa chini ya Kamanda wa Polisi (Absolom Mwakyoma), lakini sina taarifa zozote za suala hilo. Ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako,”alisema Kaimu Kamanda huyo.

Mara ya mwisho, Raia Mwema ilipowasiliana na Kamanda wa Upelelezi, Obadia Jonas Nselu, mwanzoni mwa wiki hii, hakuwa tayari kulizungumza akisema, hata hivyo, ya kuwa alikuwa kwenye kikao.
Hali ilikuwa ni hiyohiyo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi ambaye alieleza ya kuwa hafahamu habari za kuondoka kwa mtuhumiwa huyo na kumwomba mwandishi ampigie baadaye.
Hatua ya kuondoka kwa mtuhumiwa huyo kwa vyovyote vile itawasha upya moto mkali kuhusu sakata la kutoroshwa kwa wanyama hao hai nje ya nchi, na itakuwa pigo kubwa kwa upande wa Serikali na waendesha mashitaka wake.

No comments:

Post a Comment