Monday, September 19, 2011
Mabalozi CCM wanaswa wakiandikisha wapigakura
Geofrey Nyangoro na Boniface Meena, Igunga
WAKATI joto la uchaguzi mdogo wa Jimbo a Igunga likiendelea kupanda, Chama cha Wananchi (CUF) kimekituhumu CCM kuwa kimeanza kukusanya na kuorodhesha kadi za wapiga kura na kwamba, kimemkamata mmoja wa mabalozi wa nyumba kumi wa CCM wakati akifanya kazi hiyo.Tuhuma hizo dhidi ya CCM zilitolewa jana na mgombea wa CUF, Leopold Mahona, ambazo tayari zimeshapingwa na Mratibu wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba.
Akiwa katika kijiji cha Imalilo, Kata ya Nguru, jimboni humo, Mahona alisema kazi kuorodhesha majina ya wapiga kura na kadi zao inaratibiwa na kusimamiwa na wajumbe wa nyumba kumi wa CCM.
Mahona aliwataka wakazi wa kijiji hicho kukataa mpango huo kwa kutotoa vitambulisho vyao vya kupigia kura, kwani wakikubali kufanya hivyo watashindwa kuchagua mwakilishi mwenye uwezo wa kuwasaidia.
Kauli ya Mahona imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba, kuwataka wakazi Igunga kujiandaa kukabiliana na hujuma zinazotarajiwa kufanywa na CCM kwa lengo la kulazimisha ushindi, kutokana na chama hicho kupoteza mvuto kwa wananchi.
"Wakija kuwaomba shahada kataeni, hata wakiwatisha msikubali, mkae kimya na msiwafanye chochote. Subirini siku ya kupiga kura na mnichague mimi nikaletee maendeleo,’’ alisema Mahona.
Mahona alidai kuwa, wajumbe hao wanawatisha wakazi wa jimbo hilo wanaounga mkono upinzani na kulaani kuwa, kitendo hicho kinakwamisha maendeleo na juhudi za mabadiliko ya kidemokrasia.
Hujuma sehemu mbalimbali
Wakati mgombea huyo wa CUF akilalamikia kitendo hicho, mwandishi wa habari hizi imeshuhudia tukio la uandikishaji kadi hizo ukiendelea katika maeneo mbalimbali.
Mwandishi alishuhudia kijana mmoja, mkazi wa kata ya Iborogero, nje kidogo ya mji wa Igunga akiorodhesha majina ya wenye vitambulisho vya mpiga kura pamoja na namba za vitambulisho vyao vya mpigakura.
Kijana huyo alipoulizwa na Mwananchi, huku akisita kutaja jina lake, alisema kazi hiyo amepewa na wakubwa wake ambao alikataa kuwataja na kusisitiza kuwa, anachofanya ni kuorodhesha majina ya wapiga kura na vitambulisho vyao kupigia kura kisha kuviwasilisha kwa wakubwa.
‘’Mimi kazi yangu kukusanya taarifa za watu wenye vitambulisho vya mpigakura. Ninaandika majina yao pamoja na namba ya kitambulisho nawasilisha kwa wakubwa, wao watatoa maelekezo na hatua za kuchukua,’’ alisema kijana huyo.
Mmoja watu waliotoa kadi zao, Chiristina Kaloli, mkazi wa Iborogero alipoulizwa na gazeti hili alikiri kuwa, kadi yake imeishaandikishwa mjumbe wa CCM huku kusisitiza kuwa hiki ni kipindi cha mavuno kwao.
Kadi hiyo ambayo mwananchi iliona kumbukumbu zake Ikiwa na namba 05262605 inaonyesha kuwa, ‘Chritina Kaloli alijiandikisha kuwa mpiga kura Desemba 26, 2004 katika Shule ya Msingi Mpogoro, Wilaya ya Igunga’.
CCM wakanusha
Mratibu wa kampeni wa CCM, Nchemba alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema ni kitu kisichoweza kufanywa na CCM.
"Hivyo vyama vingine vinatapatapa, sisi ndio wenye wanachama wengi Igunga, tukifanya hivyo tutakuwa tunapunguza wapiga kura wetu, hatuwezi kufanya hivyo bali wao,’’ alisema.
Alisema kitambulisho ni mali ya mwenye nacho na kwa mujibu wa sheria za nchi, hakuna mtu anayeruhusiwa kuchukua kitambulisho cha mtu mwingine.
Nchemba alisisitiza kuwa, suala la kukusanya vitambulisho vya wapiga kura linaweza kufanywa na vyama vingine visivyo katika jimbo hilo kikiwamo CUF kwa lengo la kupunguza wapiga kura.
Kafumu alipuliwa
Katika hatua nyingine, Mahona alimrushia kombora mgombea Ubunge kupitia CCM, Dk Dalaly Kafumu akidai alihusika katika mpango wa kuwahamisha wakazi wa kijiji cha Ihomelo chenye utajiri wa madini.
Alisema lengo la mpango huo uliobuniwa na Serikali ulikuwa kuwaondoa wakazi wote wa kijiji hicho kwa kuwalipa fidia ya Sh500,000 na kutoa eneo hilo kwa mwekezaji ili aweze kuchimba madini ya dhahabu.
Wabunge Chadema
wapelekwa Tabora
Katika tukio lingine. wabunge wa Chadema wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa, jana wamehamishiwa Tabora mjini kwa ajili ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi leo, kujibu mashtaka ya shambulio la aibu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.
Wabunge hao, Susan Kimwanga (Viti Maalumu) na Sylvester Kasulubai (Maswa Mashariki) ambao Ijumaa walihojiwa na polisi na kuachiwa huru, walikamatwa juzi walipoenda kituo cha polisi kuripoti na kutupwa korokoroni hadi leo watakapofikishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema hicho, Tundu Lissu alilaani kitendo hicho cha polisi kuwapeleka Tabora wakati wanajua kuwa, mahakama ya Wilaya ya Igunga ina uwezo wa kusikiliza mashtaka ya wabunge hao.
Lissu alisema kuwa, atakuwepo katika Mahakama ya Tabora kuwatetea wabunge hao ambao anaamini kuwa hawakutenda kosa lolote na wana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa Sheria inatambua hilo.
“Kama polisi wanadhani kuwa wanaweza kuitetea CCM, wajifunze kwa wenzao Kenya walivyoshindwa kuitetea Serikali. Jana polisi walijawa hofu baada ya kusikia nipo hapa na wamewapeleka Tabora Mjini ili wasipate msaada wa kisheria hapa Igunga,” alisema Lissu na kuongeza:
“Kesho (leo) nitakuwepo Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora na nitahakikisha wanatoka.”
Alisema kuwa kinachotokea kwa viongozi wa chama hicho si jambo geni kwa watetea ukombozi wa nchi, kwani hata Julius Nyerere na Bhoke Munanka walionja joto ya jiwe kwa dola ya kikoloni wakati wakitafuta ukombozi.
“Ningependa Mkuu wa Wilaya afike mahakamani ili aeleze jinsi alivyovuliwa nguo katika tukio hilo,” alisema Lissu.
Alisema kuwa walichokifanya wabunge hao walikuwa na mamlaka ya kisheria kukamata mhalifu kama wahalifu wengine wowote kwa sababu polisi hawakuwepo.
“DC alikuwa kwenye eneo ambalo Chadema walipaswa kuwepo, huo ulikuwa ni uhalifu, ndiyo maana raia walitumia nguvu zao kumkamata,” alisisitiza Lissu.
Uthibitisho wa polisi
Akizungumzia tukio suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Tathimini (Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu, alisema kuwa ni kweli waliwahamisha wabunge hao jana kuwapeleka Tabora.
Alisema kuwa wamewahamisha kwa sababu za kiusalama na kwa kuwa mjini hapa siyo mahali panapofaa kushughulikia suala hilo.
“Ni sehemu ya utaratibu wa polisi, itatumika mahakama ya hakimu mkazi pale Tabora,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment