Wednesday, September 7, 2011

Marufuku sukari sasa kuuzwa nje

SERIKALI imesimamisha leseni na vibali vyote vya uuzaji wa sukari nje ya nchi na kusimamia mipaka ili kudhibiti upitishwaji holela wa bidhaa hiyo.

“Kuanzia sasa mfanyabiashara atakayekamatwa amehodhi bidhaa hiyo kwa ajili ya kulangua au kuuza nje ya nchi kinyume na maagizo ya Serikali, ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na adhabu ni faini ya Sh milioni 30 au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote,” amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohammed Muya.

Hata hivyo akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusu matatizo ya kupanda kwa bei ya sukari nchini, Muya alisema hatua hiyo inachukuliwa ingawa upo ugumu kutokana na mazingira ya soko la pamoja la Afrika Mashariki.

Lakini pia alisema Serikali imeamua kutoa leseni kwa wingi kwa wafanyabiashara wa sukari kuingiza bidhaa hiyo kwa wingi kutoka nje ya nchi, huku Serikali nayo ikiagiza tani 120,000 za bidhaa hiyo kwa lengo la kukabiliana na upungufu uliopo.

Alisema kiasi hicho cha sukari kinajumuisha tani 20,000 zilizoingizwa kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na tani 100,000 zilizobaki zitaagizwa kutoka kwingine.

Halikadhalika kwa upande wa hatua za muda mrefu za kudhibiti upungufu wa sukari nchini, Serikali inapitia maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari nchini, itahakikisha hatua zinachukuliwa ili kupata wawekezaji katika eneo hilo.

Hata hivyo, Muya alisema kiwango cha uzalishaji sukari nchini kinatosheleza mahitaji, lakini tatizo kubwa ni bidhaa hiyo kuuzwa kwa magendo Kenya na Uganda.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa hatua za kudhibiti hali hiyo alizozitangaza jana ulianza mara moja.

Muya alisema tathmini iliyofanywa na wizara yake, ilibaini kuwa bei ya sukari Uganda na Kenya iko juu ikilinganishwa na bei ya bidhaa hiyo nchini.

Alisema Kenya sukari inauzwa Sh 4,000 za Tanzania kwa kilo na Uganda ni Sh 3,500 hali inayosababisha wafanyabiashara wengi nchini kuivusha kimagendo na kuiuza katika nchi hizo.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hali ya sasa ya upatikanaji wa sukari nchini si nzuri kwa kuwa imepungua na kusababisha bei kupanda kutoka bei elekezi ya Sh 1,700 iliyokubaliwa na wadau katika kikao kilichosimamiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Machi.

Alisema pamoja na hayo pia imefahamika sukari katika soko la dunia inauzwa kwa dola kati ya 700 na 900 za Marekani kwa tani na ikiingizwa nchini bila kodi bei yake inafikia Sh 1,300 kwa kilo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Mathew Kombe, alisema kiasi cha sukari kilichozalishwa nchini mwaka huu ni tani 306,000 ambacho ni sawa na kilichozalishwa mwaka jana. “Kwa sasa kila kiwanda kinazalisha tani 44,000 wakati mahitaji ya nchi ni tani 31,000.”

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Ashwin Rana, alisema uzalishaji wa bidhaa hiyo unaendelea kama kawaida na hakuna upungufu, tatizo ni uuzwaji kwa magendo nje ya nchi na kuitaka Serikali idhibiti tatizo hilo na si kuagiza sukari zaidi kutoka nje.

Viwanda vingine vinavyozalisha sukari pamoja na Kagera, ni Mtibwa, Kilombero na TPC, ambavyo vyote vilianza uzalishaji wa bidhaa hiyo Juni hadi Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment