JESHI la Polisi Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, limewakamata watu watano akiwemo raia wa Iran, Ali Mirzael Pirbaksh, kwa tuhuma za kukutwa na kilo 97 za dawa hizo aina ya heroine zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.4.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na taarifa walizopewa na raia wema.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Said Mrisho (31) wa Tandale, Aziz Kizingiti (32) wa Magomeni Mapipa, Abdul Lukongo (36) wa Kariakoo na Hamidu Karimu (43), wa Tandale.
Nzowa alisema watuhumiwa hao waliokuwa wamepakia dawa hizo ndani ya magari mawili, Toyota Carina namba T 954 BGT na Caldina namba T 107 BAS, walikamatwa jana saa 9.30 alifajiri eneo la Afrikana Mbuyuni, Kinondoni.
“Baada ya mimi kupewa taarifa za watu hao, nilichukua vijana wangu na kuwafuatilia taratibu katika maeneo waliyokuwa wakienda na hatimaye kuwakamata eneo hilo,” alisema Nzowa.
Alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao, isipokuwa raia huyo wa Iran, ambaye ndiye anadaiwa kuingiza dawa hizo nchini, walidai kuwa zilikuwa mali ya Pirbaksh, ambaye hata hivyo hakuhojiwa baada ya kukosekana mkalimani.
Nzowa alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi wa tukio hilo utakapokamilika, huku akiwataka wananchi wanaojihusisha au kutumiwa kufanya biashara hiyo kuacha, ili kuepuka mkono wa sheria.
Aidha, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaolipa Jeshi hilo katika kupambana na biashara hiyo haramu, huku akiwataka kuendelea kudumisha uhusiano huo hadi mapambano hayo yatakapofanikiwa.
No comments:
Post a Comment