Wednesday, September 7, 2011

CUF, Chadema watunishiana misuli

CCM WAREJESHA FOMU KIMYAKIMYA, KIVUMBI CHA KAMPENI KUANZA LEO

Boniface Meena na Geofrey Nyang'oro, Igunga
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeingia vitani katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga baada ya kutunishiana misuli wakati wa kurejesha fomu za wagombea wao.Vyama hivyo ambavyo ofisi zao mjini hapa ziko karibu, vilianza kufanya maandalizi majira ya saa nne asubuhi kwa ajili ya kuwasindikiza wagombea wao kurudisha fomu, maandalizi ambayo yalikuwa ya ushindani mkubwa.

Ubabe ulianza pale CUF walipoanza kupiga muziki kwenye magari yao mawili aina ya Mitsubishi Fuso huku wakiitambia Chadema. Baadaye Chadema nao walijibu mapigo kwa kufungua muziki kwa sauti ya juu kwenye magari yao mawili pia aina ya Mitsubishi Fuso na kusababisha kelele nyingi katika eneo walilokuwapo.

Misafara yaingiliana
Wakati muziki ukiendelea, Chadema walitangaza msafara wao utakavyokwenda na kuanza kuwapanga wafuasi wao na magari yao huku CUF nao wakijipanga. Msafara wa Chadema ulipoanza kwenda ofisi za msimamizi wa uchaguzi na wa CUF nao uliingia.

Msafara wa CUF ulipita katikati ya ule wa Chadema na baada ya kufika mbele ukaziba njia.

Kitendo hicho kilitafsiriwa na wafuasi wa Chadema waliokuwa wametanda barabara nzima kuwa ni uchokozi hali iliyosababisha wafuasi wa vyama hivyo kuonyeshana ubabe kwa dakika kadhaa kabla ya Chadema kufanikiwa kupenya na kuendelea na safari ya kwenda Ofisi za Tume ya Uchaguzi.

Mzozo hadi kwa msimamizi
Chadema wakiwa na wafuasi wao, walifika katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi saa 8:00 mchana na mgombea wake kukabidhi fomu zake, lakini kabla hawajatoka, CUF nao waliingia na mgombea wao.

Nje ya ofisi ya msimamizi wa uchaguzi, nusura vurugu zitokee baada ya wafuasi wa vyama hivyo viwili kutaka kuchapana lakini walidhibitiwa na watu waliokuwapo katika eneo hilo. Mgombea wa CUF alikabidhi fomu yake saa 8:10 mchana huku wafuasi wao na wa Chadema wakizozana nje ya ofisi ya msimamizi huyo wa uchaguzi.

CCM, UPDP, wakabidhi kimyakimya

Wakati vyama hivyo viwili vikionyeshana ubabe, vyama vingine vya CCM, Chausta, UPDP, AFP na SAU vilirudisha fomu zao bila mbwembwe wala maandamano yoyote.

Mgombe wa CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu alirudisha fomu yake saa 11:00 asubuhi akiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho na kusema kuwa kwa upande wake hali si mbaya na anategemea ushindi kutokana na kuwania nafasi hiyo mara tatu na kushindwa katika kura za maoni ndani ya chama hicho, hivyo kuwa na imani kuwa wananchi wengi wanamfahamu.

“Wapiga kura wasiwe na wasiwasi wa kunichagua kwa kuwa watakuwa wamepata mbunge ambaye anafaa. Nitatoa kipaumbele kwenye maji na barabara hasa za vijijini na pia Daraja la Mbutu ni changamoto. Hayo na kilimo cha pamba na ufugaji kufanya viwe vya kisasa ni mambo muhimu.”

Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu, Dk Kafumu alitaja mikakati yake kuwa ni pamoja na kuifanya Igunga kuwa na maendeleo alisema miongoni mwa mambo atakayoyapa kipaumbele katika kuijenga Igunga ni kuboresha huduma za maji, miundombinu ya barabara hadi vijijini ikiwamo inayounganisha Igunga na Manonga.

“Baadhi ya mambo haya yameshafanywa kwa kiasi chake na mbunge wetu aliyepita, Rostam Aziz nitahakikisha kuanzia pale alipoishia na kuyaboresha zaidi," alisema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba alisema Dk Kafumu ndiye mwenye majawabu ya matatizo ya wananchi wa jimbo hilo tofauti na wa vyama vingine ambao alisema vina majibu tu.

Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye alisema atafanya kampeni za kistaarabu kwa kuwa shamrashamra zilizoonyeshwa na wananchi wa Igunga zimedhihirisha kuwa anakubalika.

“Nitafanya kampeni za kistaarabu wana Igunga wananikubali umati huu ni mkubwa, mwenyewe umeuona hiyo inajidhihirisha yenyewe,” alisema Kashindye.

Kuhusu CUF kuingilia msafara wao alisema: “Wananchi hawakuonyesha aina yoyote ya kutaka ugomvi lakini chama hiki (CUF) kinatuingilia wakati hata bado hatujamaliza kazi yetu. Barabarani wameingilia msafara na ofisi ya msimamizi pia wameingia wakati hatujamaliza kuwasilisha, huu si ustaarabu.”

CUF, SAU wajinadi
Mgombea wa CUF, Leopald Mahona alisema Wana Igunga wategemee maisha mapya ya kisiasa hasa kwa kuwa wana shida ya maji kitu ambacho ni kipaumbele cha kwanza. Pia alisema ataboresha sekta ya kilimo na mifugo kwa wakazi hao.

Akizungumzia kuingilia msafara wa Chadema alisema haoni kama kuna tatizo kwa kuwa hizo ni mbwembwe tu za kisiasa kwa hiyo hakuna shida.. “Wasukuma ni watu wapole na hakuna anayeweza kuleta vurugu. Amani itakuwapo ila ugomvi utaletwa na watu wengine ambao wana chuki binafsi.”

Mgombea wa SAU, John Magid alisema matarajio yake ni kuhakikisha kuwa katika kampeni anawaelimisha wananchi juu ya mabadiliko wanayoyahitaji kwani muda umewadia.

“Huu ndiyo muda wa muafaka wa kuyafikia matarajio hayo kwa njia ya kunipigia kura ili niwe mbunge wao na niweze kukaa nao na kuangalia mbinu za kuweza kufikia mafanikio katika uchumi,” alisema.

Sirro atua Igunga
Mkuu wa Kikosi cha Operesheni Maalumu cha Jeshi la Polisi, Simon Sirro aliwasili hapa jana kwa ajili ya kuhakikisha kampeni za uchaguzi huo zinafanyika kwa amani.

Sirro alisema kuwa jeshi la polisi limejipanga vyema kusimamia usalama katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2 mwaka huu... “Tumejipanga vizuri na kazi inaendelea vizuri, nitakuwapo muda wote kwa kuwa ndiyo kazi yangu.”

Mbowe, Slaa kutua leo
Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa wanatarajiwa kuwasili leo mjini hapa kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho kesho.

Mbowe alisema jana kwamba pia watakuwapo wakurugenzi wote wa chama hicho na
wabunge mbalimbali katika timu hiyo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Seif Sharif Hamad ameishauri Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Igunga kuacha kuingilia masuala ya uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika Oktoba 2 mwaka huu ili kuepusha vurugu.

Katibu huyo imevitaka vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Igunga kufuata taratibu na kutoingiliana katika mikutano yao ya kampeni.

Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alitoa kauli hiyo jana akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kiserikali katika Mkoa wa Tabora, siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo mdogo unaoshirikisha vyama tisa vya siasa.

“Kiutaratibu, uchaguzi husimamiwa na Tume ya Uchaguzi ambayo kimsingi ni huru na isiyoingiliwa na upande wowote, lakini uzoefu unaonyesha kamati ya usalama huingilia kazi za tume. Acheni kuingilia kazi za tume ili uchaguzi huo uweze kufanyika kwa uhuru. Naamini hiyo pia itaepusha vurugu.”

Alisema kwa sasa Kamati ya usalama ya Wilaya inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario ina kazi ngumu ya kuhakikisha uchaguzi huo unamalizika kwa amani na utulivu.

Alisema kama tume itaachiwa ifanye kazi yake kwa uhuru na kutenda haki, itawezesha wananchi wa Jimbo hilo kusikiliza sera za vyama na kuchagua mwakilishi anayewafaa.

Hamad alizitaka mamlaka kuachia vyama vya siasa kunadi sera zao akisisitiza kuwa hatua hiyo itawezesha wananchi kuchagua mbunge wanayemtaka. Alisema wakati mwingine uchaguzi hufanyika kwa amani na tulivu lakini tatizo huja wakati wa kujumlisha kura ambako nguvu hutumika bila sababu za msingi.

Kampeni za uchaguzi huo zinaanza leo katika kata 26 za Jimbo la Igunga mkoani Tabora.

No comments:

Post a Comment