RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa nchini kwa kuwapandisha vyeo wakuu wa wilaya 11 katika mabadiliko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam jana, katika mabadiliko hayo, ameteua wakuu wa mikoa wapya 15, kubadilisha vituo vya kazi watano na wengine saba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko ole Kone amebaki kwenye kituo chake cha kazi wakati
wengine wanne watapangiwa kazi nyingine.
Aidha, wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika, watatangazwa baadaye.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliwataja wakuu wa wilaya 11 waliopandishwa vyeo na kuwa
wakuu wa mikoa, na wilaya wanazotoka kwenye mabano, ni John Tupa (Dodoma Mjini) kwenda Mara; Saidi Mwambungu (Morogoro) Ruvuma; Chiku Gallawa (Temeke) kwenda Tanga; Leonidas Gama (Ilala) Kilimanjaro; Dk. Rehema Nchimbi (Newala) Dodoma na
Elaston Mbwillo (Mtwara) Manyara.
Wengine ni Kanali Fabian Massawe (Karagwe) Kagera; Fatma Mwassa (Mvomero) Tabora; Ali Rufunga (Manyoni) Lindi; Ernest Ndikillo (Kilombero) Mwanza na Magesa Mulongo (Bagamoyo) Arusha.
Wakuu wapya wa mikoa ni Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya (Rukwa) na naibu
mawaziri wa zamani Mwantumu Mahiza (Pwani); Joel Bendera (Morogoro) na Ludovick Mwananzila (Shinyanga).
Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitoka Mwanza; Said Mecki Sadiki anayekwenda Dar es Salaam akitokea Lindi; Dk. Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma; Issa Machibya anayekwenda Kigoma akitokea Morogoro na Joseph Simbakalia anayekwenda Mtwara akitokea Kigoma.
Dk. Parseko ole Kone ataendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida. Waliostaafu ni Mohammed Babu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera; Isidore Shirima (Arusha);
Anatory Tarimo (Mtwara) na John Mwakipesile (Mbeya).
Wengine ni Enos Mfuru (Mara); Brigedia Jenerali Dk. Yohana Balele (Shinyanga) na Said Kalembo (Tanga).
Wakuu wa mikoa wanne waliostaafu na watapangiwa vituo vingine vya kazi ni Amina Mrisho
(Pwani); Dk. James Msekela (Dodoma), Abeid Mwinyimsa (Tabora) na Daniel ole Njoolay (Rukwa).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakuu wote wa mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa Hati za Makabidhiano katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa.
Aidha, wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo nao wanapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya
wakuu wa wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na uteuzi wao.
“Wakuu wa mikoa minne mipya na wa wilaya watakaoteuliwa baadaye, nao watatakiwa kuandaa Hati za Makabidhiano ndani ya siku 14 tangu kuapishwa,” ilisema taarifa
hiyo.
Ilieleza kuwa makabidhiano hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao.
Wakuu wote walioteuliwa na wa mikoa minne mipya pamoja na wakuu wote wa wilaya watakaoteuliwa watatakiwa kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu kwenye Chuo
cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma, kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.
Taarifa ilieleza kuwa wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa kesho saa 4 asubuhi kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa kwa mara ya mwisho Novemba 24 mwaka jana na tangu aingie madarakani Desemba 2005, alifanya uteuzi mara mbili.
No comments:
Post a Comment