Wednesday, September 14, 2011

Maiti ajali ya meli waonekana ufukweni Mombasa

MAITI watano zaidi wanaoaminika kuwa wa ajali ya mv Spice Islander wamepatikana katika ufukwe wa bahari ya Hindi eneo la Mombasa nchini Kenya.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi eneo la Nungwi wakati meli hiyo inayodaiwa kuzidisha uzito ikiwa inatoka Unguja kwenda Pemba.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, alithibitisha jana kupokea taarifa ya kuwapo kwa maiti hao kupitia ubalozi mdogo wa Tanzania ulioko katika Jiji hilo la pwani ya Kenya.

“Ni kweli Balozi wetu mdogo aliyeko Mombasa, alitupa taarifa za kuonekana kwa maiti watano katika ufukwe wa Bahari ya Hindi jijini humo na wanasadikiwa kutokana na ajali ya meli ile,” alisema Aboud.

Alisema kwa mujibu wa taarifa walizopewa na Balozi huyo, Yahya Haji Jecha, maiti hao walizikwa Mombasa kwa heshima zote, baada ya kuonekana wameharibika. Kuonekana kwa maiti hao kunafanya idadi ya waliokufa hadi jana kufikia 202.

Akifafanua, Mohamed alisema maiti watatu ni wanaume, mmoja mwanawake na mtoto mwenye umri unaokadiriwa kuwa mwaka mmoja.

Alisema utafutaji maiti zaidi unaendelea kwa ushirikiano mkubwa wa Jeshi la Polisi wanaotumia helikopta na wapiga mbizi kutoka Afrika Kusini ambao waliwasili nchini juzi. Utafutaji umepanuka hadi Tanga na Bagamoyo.

Wakati huo huo, taasisi mbalimbali pamoja na vyama vya siasa wanaendelea kutoa pole na rambirambi kwa Serikali kutokana na msiba huo mkubwa.

Jana Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa akifuatana na Katibu Mkuu, Wilson Mukama, walifika ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ambapo walikabidhi Sh milioni 10 za ubani.

Akikabidhi msaada huo, Msekwa alisema CCM imesikitishwa na msiba huo mkubwa ambao umepoteza wananchi wengi wa Zanzibar.

“Huu ni msiba mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar, lakini pia kwa Watanzania kwa ujumla na ndiyo maana CCM imeguswa na kuamua kutoa ubani kwa ajili ya wafiwa na tunawataka kuwa na moyo wa subira,” alisema Msekwa.

Jumuiya ya Koja Shia Federation ikiongozwa na Rais wake, Anuar Dharamsi, ilikabidhi jumla ya Sh. milioni 30 kwa wafiwa. Dharamsi alisema Jumuiya imesikitishwa na msiba huo na kusema hiyo ni kazi ya Mungu, ambayo haina makosa.

Balozi Seif aliipongeza jumuiya hiyo kwa moyo wa kusaidia watu waliopatwa na msiba na kusisitiza kwamba fedha zote zilizotolewa zitakwenda kwa wahusika.

Nao wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, walitoa ubani wa Sh. milioni mbili kwa ajili hiyo.

Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeukataa msaada wa maafa uliokuwa utolewe na kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom baada ya wananchi kuilalamikia kwa kuendesha mashindano ya Miss Tanzania, wakati Wazanzibari wakiwa katika msiba wa kitaifa.

Waziri Aboud alithibitisha kuwapo taarifa hizo za SMZ kukataa msaada wa maafa uliokuwa utolewe na Vodacom.

“Ni kweli, tumekataa kupokea msaada huo ingawa hatujui ni kiasi gani cha fedha ... unajua wananchi wengi wametoa malalamiko yao na kukerwa na wafadhili hao wa mashindano ya urembo kuendelea na onesho lao wakati huku Taifa limepatwa na msiba mkubwa,” alisema Aboud.

Aliongeza kuwa wadhamini hao walitakiwa kufahamu wajibu wao kwa jamii zaidi wakati inapokutwa na maafa kama hayo ya kuzama kwa meli na wananchi zaidi 200 kupoteza maisha.

Aboud alisema haieleweki hata kidogo kwa kampuni hiyo iliyodhamini mashindano hayo kuendelea wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, akiwa ametangaza msiba wa kitaifa pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

Wananchi wengi wa Zanzibar walikerwa na kuendelea kwa mashindano hayo ya urembo ya kumtafuta Mrembo wa Tanzania katika kipindi ambapo Taifa lipo katika msiba mkubwa.

Gazeti hili lilifanya juhudi za kuwatafuta wasemaji wa Vodacom ili kuzungumzia hatua hiyo ya SMZ, lakini hawakuwa wakipokea simu zao.

Hata hivyo waandaaji wa mashindano hayo, Kampuni ya Lino International Agency kupitia Mkurugenzi wake, Hashim Lundenga, jana waliomba radhi kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari.

Lundenga alisema walichelewa kupata taarifa za ajali, walipokea saa 9.30 alasiri muda mfupi kabla fainali za Miss Tanzania hazijaanza, pia alisema Shirikisho la Vyama vya Soka Tanzania (TFF), liliendelea na ligi kwa mechi ya Yanga na Ruvu Shooting. Ligi hiyo pia inafadhiliwa na Vodacom.

Alisema hata baa nyingi na kumbi za disko ziliendelea kutoa burudani, na kwamba hata muda wa kupeleka jina la mshindi wa Tanzania, Miss World, ulikuwa umekwisha hivyo kushindwa kuahirisha, lakini pia tamko la kusimamisha shughuli za burudani lilitolewa Septemba 11.

Lundenga akijitetea zaidi akisema hata hivyo warembo walipopanda jukwaani walivalia vitambaa vyeusi mikononi huku watazamaji nao wakisimama dakika moja kuwaombea waliopatwa na maafa hayo.

Kazi ya utafutaji maiti zaidi ndani ya meli ya mv Spice Islander jana ilishindikana baada ya kuchafuka kwa bahari na kusababisha mawimbi makubwa.

Ofisa kutoka katika kikosi cha uokoaji cha KMKM ambaye hakutaka kutajwa jina alisema wapiga mbizi wa Afrika Kusini walishindwa kufanya kazi hiyo kutokana na kuchafuka kwa bahari katika eneo la mkondo wa bahari ya Nungwi ambao ni maarufu kutokana na kina kirefu cha maji.

“Kwa ufupi kazi za uzamiaji na kutafuta miili zaidi ya watu imeshindikana … unajua leo bahari imechafuka sana huku mawimbi makali yakitawala,” alisema ofisa huyo ambaye ni daktari.

Lakini zaidi alisema eneo ilipozama meli hiyo baada ya kupimwa lina kina cha meta 338 wakati vifaa walivyonavyo wazamiaji hao uwezo wao ni wa meta 100.

Waziri Aboud alikiri kazi hiyo kukwama kutokana na hali mbaya ya bahari. “Ni kweli wazamiaji wameshindwa kuendelea kutokana na kuchafuka kwa bahari inayotokana kwa kuwapo mawimbi makubwa eneo la mkondo,” alisema Aboud.

Naye Theopista Nsanzugwanko anaripoti kwamba Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amempongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa uamuzi wake wa kuahirisha ziara ya Canada baada ya kutokea ajali ya meli Zanzibar Jumamosi.

Meli ya mv Spice Islander ilizama katika eneo la Nungwi, Zanzibar wakati ikitoka Unguja kwenda Pemba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 197 na kujeruhi zaidi ya 619.

Hata hivyo ameshangaa kwa nini Waziri wa Miundombinu na Mkurugenzi wa Bandari Zanzibar hawajawajibika kutokana na ajali hiyo, akisema ilitokana na uzembe wa kuzidisha uzito.

Akihojiwa jana na East Africa Radio kuhusu ajali hiyo, Zitto alisema hatua ya Rais Kikwete kufuta ziara hiyo iliyokuwa ni mwaliko wa Gavana wa nchi hiyo inaonesha jinsi alivyoona umuhimu na uzito wa tukio hilo.

Alisema mbali na uzito wa msiba na kutambua heshima ya Watanzania, hakuthubutu hata kumtuma Waziri Mkuu, bali aliiahirisha.

Zitto pia alishangazwa na baadhi ya watu na taasisi zilizoendelea na burudani hadi jioni siku ya tukio.

“Kitendo cha Rais kuahirisha ziara yake kwa nchi kubwa kama Canada ilitosha kuueleza umma wa Watanzania kupokea kwa uzito wa juu msiba huu, lakini kuna televisheni ya Bara iliendelea kutangaza sherehe hadi usiku siku ya ajali,” alisema

Akizungumzia kuwajibika kwa Waziri wa Miundombinu na Mkurugenzi wa Bandari, Zitto alisema hata kama hawakuwapo wakati wa tukio, kitendo cha meli kuzidisha mzigo ni kuonesha kutowajibika.

Alisema katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ni vizuri ikaonekana tofauti na inapoongozwa na chama kimoja, kwa watu kuwajibika pale wanapoisababishia nchi madhara makubwa kama haya.
“Katika hili suala la kujiuzulu halina hata sababu ya kuundwa kamati maalumu aanze Waziri wa Miundombinu na Mkurugenzi afuatie, kwani itaonesha kujali kwa waliopoteza ndugu na majeruhi,” alisema.

Alishauri wamiliki wa vyombo vya majini wakati wa kuchukua leseni waelezwe kuwa na mavazi ya kujiojkolea kulingana na idadi ya watu huku wakiwaelekeza abiria kabla ya kuanza safari kama inavyofanyika kwenye ndege.


Aliiomba Serikali kuwafikiria wavuvi wa eneo la Nungwe waliofanya jitihada za kuokoa watu na kuopoa maiti, ili wapewe mkono wa ahsante, huku akipongeza Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na serikali zote mbili kwa jitihada za kufanikisha kuokoa watu zaidi ya 600.

No comments:

Post a Comment