Monday, September 5, 2011

Ngeleja: Makali ya mgawo kupungua Desemba

Na Stella Aron

SERIKALI imewaomba wananchi kuwa wavumilivu kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea maeneo mbalimbali nchini na kuahidi ifikapo Desemba mwaka huu, tatizo hilo
litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja, aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Symbion, Aggreko na Jacobsen iliyopo Ubungo.

Alisema Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza mgawo kwa kuhakikisha inafanya kazi usiku na mchana.

“Tunaelewa kutokana mgawo huu, uchumi wa nchi umeyumba, watu wanapoteza ajira hivyo tunalazimika kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mgawo huu unakwisha kabisa na ifikapo Desemba utakuwa umepungua,” alisema Bw. Ngeleja.

Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu na kumtaka Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. William Mhado, kutoa taarifa yanapotokea mabadiliko.

“Kama kuna mabadiliko ya ratiba ya mgawo ni vyema mtoe taarifa kwa umma badala ya kukaa kimya, hili ni tatizo la wote sio nyinyi peke yenu,” alisema Bw. Ngelena na kuongeza kuwa, ahadi ya kupunguza makali ya mgawo aliitoa bungeni kwa kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu, mitambo yote mitatu itakuwa ikizalisha umeme.

Kwa upande wake, msimamizi wa mtambo wa Symbion Bw. Moses Mwandenga, alisema mtambo huo ambao unatumia gesi na mafuta una uwezo wa kuzalisha megawati 112 za umeme na kuna mitambo minne yenye uwezo wa kuzalisha megawati 20.

“Mtambo huu wa Symbion ambao unazalisha megawati 112 tunauwasha kesho (leo), hivi sasa unazalisha megawati 75,” alisema.

Msimamizi wa miradi hiyo kutoka TANESCO, Bw. Saimon Jirima, alisema mradi wa Jacobsen ambao unasimamiwa na Bw. Marrkko Rapo, ulitarajiwa kukamilika Juni 2012 lakini kutokana na dharura iliyopo, mradi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya kipindi hicho.

Alisema mradi huo wenye mashine tatu zenye uwezo wa kuzalisha megawati 35 kila moja, tayari umeanza kufungwa vifaa ambapo mtambo wa Aggreko, una mashine 63 zilizokamika katika kituo cha Ubungo badala ya 50 zilizokuwa kwenye mkataba wa makubaliako.

“Vituo viko viwili, kimoja Ubungo na kingine Tegeta, kila kimoja kinatakiwa kuwa na mashine 50 lakini wameleta na mashine za  ziada ili kuziba pengo kama litatokea tatizo,” alisema Bw. Jirima.

Hata hivyo, Bw. Mhando alisema hadi sasa kuna megawati 570 za umeme ambazo zinazalishwa nchi nzima na bado jitihada zinaendelea kufanyika ili kupunguza kero iliyopo ambapo mitambo hiyo inatarajiwa kuanza kuzalisha umeme mwezi huu.

Wakati huo huo, Bw. Ngelaja aliwashukuru waumini 200 wa madhehebu mbalimbali ambao walikwenda kufanya maombi ya kuomba mvua katika Bwawa la Mtera, mkoani Iringa.

Alisema maombi hayo yaliongozwa na mchungaji Charles Gadi kutoka Kanisa la Goodnews For All ambapo Serikali imetambua mchango wao na kuwaomba waumini wengine kuendelea kufanya hivyo ili mvua zinyeshe.

No comments:

Post a Comment