Friday, September 9, 2011

Udanganyifu mtihani darasa VII:Mwalimu Mkuu na Msaidizi wanaswa

WATU wanne akiwamo Mwalimu Mkuu na Msaidizi wake wa Shule ya Msingi ya Kagwe kijijini Kagwe, katika Kata ya Siloka, Bukombe mkoani hapa, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa wakiandaa majibu ya mtihani wa darasa la saba.

Watuhumiwa hao ambao ni pamoja na Msimamizi wa mtihani huo, wanadaiwa kuandaa majibu ya mtihani wa Taifa wa Kiswahili.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Diwani Athumani, alisema ofisini kwake jana, kwamba watu hao walikutwa na maofisa wa Kamati ya Kusimamia Mitihani ya Taifa wa Elimu ya Msingi kwa kushirikiana na wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Kirima Robert (36), Msaidizi wake, Samson Ngozi (27), Msimamizi wa Mitihani, Peter Matipa (24) na mkulima, Kuya Kunyango (24).

Kamanda Athumani alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi saa 8.50 mchana nyumbani kwa Mwalimu Ngozi wakiandaa majibu hayo wakati mtihani ukiendelea.

Alisema mgambo aliyekuwa akilinda mtihani huo, Mpemba Kachere, alitoroka baada ya kubaini kuwa Mwalimu Mkuu, Msaidizi wake, Msimamizi wa Mtihani na mkulima huyo, wamekamatwa kwa tuhuma hizo.

“Juhudi za kumtafuta mgambo huyo kwa kushirikiana na Takukuru na Kamati hiyo zinaendelea ili kuhakikisha kuwa anakamatwa na kufikishwa mahakamani pamoja na wenzake,” alisema Kamanda Athumani.

Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi nchini ulianza Jumatano na kumalizika jana ambapo wanafunzi zaidi ya milioni moja walikuwa wakitarajiwa kuufanya nchi nzima.

No comments:

Post a Comment