Kundi la Waislam wenye itikadi kali nchini Somalia, al-Shabaab, limetangaza kuwa linaungana na kundi la al-Qaeda.
Tamko hilo limetolewa katika picha ya video iliyotolewa na makundi hayo mawili.Yusuf Garaad wa Idhaa ya Kisomali ya BBC ambaye ameitazama video hiyo amesema kundi hilo ambalo jina lake kamili ni Harakat al Mujahiddin al Shabaab, limetangaza rasmi kuungana na al-Qaeda.
Madai ya muungano huo yametolewa na kiongozi wa al-Shabaab, Ahmed Godane, au maarufu kama Abu Zubair.
Akizungumzia Marekani, Ahmed Godane amesema wakati wa dola pekee duniani- Marekani - sasa umefikia mwisho na kuwa utawala wa Uislam ndio utachukua mamlaka.
Kiongozi wa al-Qaaeda, Ayman al-Zawahiri, ambaye pia ameonekana katika video hiyo, ameisifia al-Shabaab na kukiri na kukubali kwa kundi hilo kuungana na al-Qaeda.
Amesema hizo ni habari njema kwa wafuasi wake.
Wapiganaji
Al-Zawahiri amesema Somalia itakuwa ngome ya Jihad katika pembe ya Afrika na kuongeza kuwa watateketeza kile alichotaja kuwa ni kiburi cha majeshi ya Kikristo kutoka Marekani, Ethiopia na Kenya dhidi ya Wasomali.Ametoa wito kwa al-Shabaab kulinda watu wake hasa wale ambao ni dhaifu, na pia kutaka kwa wananchi wa Somalia kuunga mkono uamuzi wa vijana wao, akimaanisha al-Shabaab.
Al-Shabaab ni kundi lenye wapiganaji maelfu kadhaa, wengi wao wakiwa ni Wasomali. Hata hivyo wanao pia wapiganaji wa kigeni kutoka katika nchi zinazoizunguka Somalia na hata sehemu nyingine duniani.
Mitindo yao ya upiganaji ni pamoja na mabomu ya kujitoa mhanga na pia ya kutegwa ndani ya magari.
Mwenendo
Al-Shabaab kwa sasa inadhibiti maeneo kadhaa ya kusini na kati ya Somalia.Katika miezi kadhaa iliyopita wamekuwa wakibanwa kutoka pande kadhaa. Mjini Mogadishu wanapambana na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, Amisom, yenye wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Djibouti. Majeshi hayo yanadhibiti zaidi mji mkuu, Mogadishu.
Upande wa kusini, majeshi ya Kenya yameshambulia ngome za al-Shabaab ardhini, baharini na angani. Majeshi ya Ethiopia pia yanashambulia kundi hilo kwa upande wa kaskazini na tayari wameteka mji wa Beled Weyne, mji muhimu katikati mwa Somalia.
Kuungana kwa al-Shabaab na al-Qaeda huenda kukabadili mwenendo mzima wa mzozo wa Somalia.
No comments:
Post a Comment