Friday, February 3, 2012
Waziri atangaza ukata serikalini
Habel Chidawali, Dodoma
na Boniface Meena, Dar
SERIKALI imekiri kuwa hali yake kifedha ni mbaya, ndiyo maana halmashauri nchini hazina fedha za kuendesha mambo mbalimbali ya kiutendaji.Desemba 6 mwaka jana gazeti hili liliripoti kwamba Serikali inakabiliwa na ukata uliosababisha wizara, idara na taasisi za Serikali zikiwamo baadhi ya vyuo vyake vikuu, kushindwa kufanya baadhi ya kazi zake, lakini Serikali ilikanusha.
Jana, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Singida Magharibi, Mohammed Missanga alikiri ukata huo na kueleza kuwa ni tatizo kubwa.
Missanga alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu ukata uliozikumba halmashauri nchini kwa kukosa fedha kutoka Serikali Kuu, kitendo ambacho kimesababisha zishindwe kufanya mambo mbalimbali ya kiutendaji ikiwamo kuendesha vikao vyake na kusimamia maendeleo ya miradi.
Akijibu swali hilo, Mkuchika alisema halmashauri zina tatizo kubwa la fedha ambalo linasababisha baadhi ya mambo ikiwemo kufanyika kwa vikao vya kiutendaji kusimama. Aliongeza 'Kiwango cha fedha ni kidogo na hili liko mikononi mwa Waziri Mkuu."
Alisema tatizo hilo ni kubwa mpaka Chama cha Serikali za Mitaa (ALAT) kimeomba kukutana na uongozi wa juu wa Serikali, ili kuzungumzia tatizo hilo.
Mkuchika alisema katika halmashauri zote nchini hivi sasa kuna matatizo makubwa yanayotokana na ukata wa fedha ambazo kwa muda mrefu hazijapelekwa huko, huku akikiri pia hata fedha za mwaka jana hazijapatikana. Katika kuthibitisha tatizo hilo, Waziri huyo pia alishindwa kueleza lini fedha hizo zitapatikana na kupelekwa kwenye halmashauri.
“Hata za mwaka jana hatujapeleka huko ndio maana wanalalamika, hata ALAT wameomba kukutana na uongozi wa juu serikalini kuzungumzia jambo hilo, lakini, kwa ujumla hali ni mbaya,’’alisema Mkuchika.
Ukata huo ulisababisha kuchelewa kwa ruzuku ya vyama vya siasa vyenye wabunge na madiwani, hali iliyoathiri uendeshaji wa shughuli za ndani za vyama hivyo kikiwamo chama tawala, CCM.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC), Augustino Mrema alisema ukata huo umesababisha miradi mingi kukwama kutokana na bajeti iliyopitishwa kutotekelezeka.
Alisema ni kweli Serikali inayumba kwa kuwa hali ya fedha ni mbaya. "Alichosema Mkuchika ni sahihi na nampongeza kwa kukiri kuwa hawana fedha kwa kuwa mambo hayaendi kabisa huko kwenye halmashauri."
Mrema aliongeza, "Kwa mfano kule Himo waliniambia wangenipa Sh150m kwa ajili ya mradi wa maji, lakini hadi hivi sasa wametoa Sh50 milioni ambazo haziwezi kufanikisha mradi huo."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment