Anthony Kayanda, Kigoma
HALI si shwari ndani ya Chama cha NCCR Mageuzi Jimbo la Kigoma kusini, baada ya Katibu wake, Faida Masudi kujikuta akipigwa makonde na kurushiwa viti na baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo uliofanyika juzi mjini Kigoma, na hatimaye kuvunjika baada ya pande mbili zinazopingana kushindwa kufikia muafaka juu ya masuala kadhaa ya chama.
Dalili za tafrani hizo zilionekana mapema asubuhi baada ya Wajumbe kadhaa kuanza kuwapinga wenzao kwa madai ni mamluki wa Chama fulani kikongwe nchini, waliodaiwa kuwa na dhamira ya kuleta mpasuko ndani ya chama hicho ambacho tayari kiko katika mgogoro kati ya uongozi wa Jimbo na Taifa.
Taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya kikao zinaeleza kuwa, chanzo cha ugomvi ni kitendo cha Katibu wa NCCR Mageuzi Jimbo la Kigoma kusini kuwakingia kifua wasiondolewe ukumbini watu wanaodaiwa kuwa mamluki waliotaka kuhudhuria mkutano huo, ilhali wakidaiwa si Wajumbe halali.
"Huyu Katibu anatuvuruga sana kwa sababu kuna kila dalili kwamba amehongwa ili atuharibie Chama chetu ambacho tumekipigania kwa muda mrefu, amekuja na watu ambao si Wajumbe na hawajulikani. Anadai yeye ndiye anayetoa mialiko kwa Wajumbe, ni sawa, lakini kwa nini amlete mtoto wake na baadhi ya Watu kutoka Vyama vingingine? Hatuwezi kukubali upuuzi huu" alilalamika Iddi Kahawa.
‘Tunajua ameandaliwa kuja kufifiza hoja ya Mbunge wetu Kafulila (David) ili tumuone hafai, lakini sisi tumeamua kufanya lolote hata kama ni kuachana na hiyo NCCR Mageuzi ambayo ipo Kigoma tu katika Tanzania nzima, lakini hawa jamaa wanataka kutuchezea na kutuona sisi hatuna akili’ .alilalamika zaidi kwa jazba.
Wanadai Wajumbe waliamua kuwatoa kwa nguvu Watu wanne ukumbini hapo wanaodaiwa ni mamluki, jambo lililopelekea Katibu wa Jimbo, Faida atoke meza kuu na kuja walipokaa Wajumbe ili kuzuia wasitolewe ukumbini, jambo lililowakasirisha Wajumbe na ndipo walipoamua kumchapa ngumi hadi alipookolewa na Wasamaria wema na Polisi waliokuwa wamealikwa mapema kulinda usalama katika mkutano huo.
Licha ya kulalamikiwa kwa kupenyeza Wajumbe mamluki, pia Katibu huyo anashutumiwa kwa kuwafukuza isivyo halali Makatibu wa Kata wa Chama hicho, Caltus Damas wa Nguruka na Thobias Kichwa wa Itebula kwa madai ya kuwatukana Viongozi wa Taifa na kuzuia mikutano yao katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo .
‘Katiba ya NCCR Mageuzi haimruhusu Katibu wa Jimbo kumfukuza Kiongozi yeyote, mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Halmashauri kuu ya Taifa pekee ambayo nayo lazima itoe tuhuma na Kiongozi husika apate nafasi ya kujitetea, vinginevyo haiwezekani hata kidogo’. alifafanua Diwani wa Kata ya Nguruka, Abdallah Hussein.
Mwenyekiti wa Jimbo hilo , Venance Mwaka alieleza kwamba kwa muda wa saa tano, kikao hicho kilishindwa kufunguliwa kutokana na baadhi ya Wajumbe mamluki kuwamo ukumbini, jambo lililoashiria kuwapo kwa hila mbaya ndani ya Mkutano Mkuu huo wa kawaida katika Jimbo.
Anasema kwa kawaida Mkutano Mkuu huandaliwa na Kamati ya utendaji ya Jimbo ambayo pia hupanga agenda za mkutano, sambamba na kufanya maandalizi mengine yenye lengo la kufanikisha mkutano husika.
‘Hadi leo siku ya mkutano (Jumanne) mimi kama Mwenyekiti wa Jimbo nimeingia ukumbini sijui agenda za mkutano, hata Wajumbe ambao kimsingi ni lazima waandikiwe agenda katika barua zao za mialiko hawakuelezwa chochote, na ndiyo maana Wajumbe wengi wamemuona huyu Katibu wa Jimbo si mwadilifu na alikuwa na hila mbaya dhidi ya Chama chetu’ alisema Mwaka.
Diwani wa Kata ya Kandaga, Fidelis Kumbo alilalamikia kitendo cha Kamishna wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Kagera, Peterson Mshenyela kuingilia isivyo halali mkutano wao na kuonekana dhahiri akimpiga vita Mwenyekiti wa Jimbo hilo , jambo lililozidisha mpasuko kwenye mkutano.
Anasema kwa mujibu wa Katiba ya NCCR Mageuzi, Mshenyela si Mjumbe halali wa Mkutano mkuu wa Jimbo lao kwa vile yeye anatoka Mkoa wa Kagera, na sio mkazi wa Jimbo hilo kama Katiba ya Chama chao inavyofafanua sifa za Wajumbe wa mkutano mkuu wa Jimbo.
‘Hata kitendo chake cha kugawa posho za mkutano na kulipa nauli kwa Wajumbe ni ubatili mtupu kwa vile sisi tunaye Mweka hazina wa Jimbo ambaye ndiye aliyestahili kushughulikia mambo yote ya kuwalipa Wajumbe haki zao, sasa huyo Mshenyela yeye alifanya kazi hiyo kwa maslahi ya nani? Bila shaka hata hizo pesa zilizotumika pengine si za Chama, labda kuna mahali zimetoka kuja kutuvuruga’ alifafanua Kumbo.
Wakati Katibu wa Jimbo akitakiwa kutoa ufafanuzi juu ya ugomvi uliotokea ukumbini hapo, alijikuta akizuiliwa kusema chochote na Kamishna wa Chama hicho wa mkoa wa Kagera, Mshenyela kwa madai kwamba ni lazima wakaandae taarifa rasmi ya Chama kabla ya kuitoa kwa Waandishi wa habari hapo baadaye.
Hata hivyo baadhi ya Wajumbe wameeleza kuwa mgogoro mkubwa unaokitafuna NCCR Mageuzi katika Jimbo hilo ni kitendo cha NEC ya Chama hicho kumfukuza uanachama Mbunge wa Jimbo hilo, David Kafulila na hivyo kuendeleza rekodi ya Wabunge wa upinzani katika Jimbo hilo kushindwa kumaliza vipindi vyao vya Ubunge kwa mujibu wa sheria kutokana na sababu mbalimbali, kama ilivyowahi kutokea kwa Kifu Gulam hussein wa Chama hicho mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment