Wednesday, February 15, 2012

Mali za vigogo 60 kuhakikiwa

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ni miongoni mwa viongozi 60 watakaohakikiwa mali zao kuanzia Jumatatu.

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya maaduili ya Viongozi wa Umma, wengine watakaohakiiwa ni pamopja na wakurugenzi, wabunge, madiwani na makanda wa Polisi wa mikoa.

Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Salome Kaganda, al;isem,a jana Dar es Salaam kwamba kazi hiyo itakamilika Machi mosi katika kanda sita na makao makuu, Dar es Salaam.

Wengine watakaohakikiwa katika awamu ya kwanza pamoja na Sitta na Mnyika ni, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu.

Pia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Liberatus Sabas na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi.

Kadhalika yumo Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Charles Nyamrunda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovic Mwananzila na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu.

Kanda zitakazohusika na uhakiki huo ni Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kusini.

Jaji Kaganda alisema, kutokana na idadi ya viongozi kuwa kubwa, sekretarieti itaanza na uhakiki wa viongozi 60 wenye nyadhifa tofauti na kazi hiyo itafanywa kwa mujibu wa sheria na wanasheria waliobobea wa sekretarieti hiyo na wachunguzi.

“Sheria ya Maadili inamtaka kila kiongozi wa umma anayehusika na sheria hii, kutoa taarifa za mali na madeni katika kipindi cha siku 30 baada ya kupewa wadhifa na kila mwisho wa mwaka yaani ifikapo Desemba 31,” alisema Jaji Kaganda.

Alisema, mwitikio wa urejeshaji wa matamko ya kukiri mali na madeni ya viongozi umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 22.5 kutoka wastani wa asilimia 60 kwa mwaka 2010.

Jaji Salome aliwataka viongozi wote waliopangiwa kufanyiwa uhakiki kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maofisa wa Sekretarieti ili wafanikishe kazi hiyo.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kushirikiana na Sekretarieti kutoa taarifa zitakazosaidia kugundua mali zilizofichika ambazo zinasadikika kuwa za viongozi wa umma wanaoguswa na Sheria ya Maadili.

Alisisitiza kuwa, viongozi waliotajwa kuhakikiwa wasifikiri kuwa wametajwa na wengine na waepuke matapeli ambao wanaweza kuwafikia wakiwataka kutoa rushwa ili wasihakikiwe wakijidai kuwa wao ni maofisa wa Sekretarieti.

Kuhusu vigezo vilivyotumika kuanza na viongozi hao, Jaji Kaganda alisema Sekretarieti iliteua sampuli bila kuzingatia vigezo, katika kila kanda na kupata viongozi hao na kuzingatia kanuni za uwazi ili kila mwananchi ajue kinachofanyika.

Katibu Msaidizi, Idara ya Viongozi wa Siasa, Coletha Kiwale alisema kazi ya uhakiki ni ya kawaida na viongozi waliotajwa hawana tuhuma yoyote bali ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti.

Alisema viongozi wanaohusika wamepelekewa barua na maelekezo yanayostahili na kutakiwa kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazosaidia uhakiki huo.
Mali ni kosa?

Katika hatua nyingine, Jaji Kaganda alisema katika kikao cha Baraza la Maadili kilichokutana mwaka jana kuhoji baadhi ya viongozi ambao hawakujaza fomu ya kutambulisha mali zao, hawakufikia kutoa adhabu ya kufukuzishwa kazi kwa kiongozi yeyote badala yake wapo waliopewa onyo kali.

“Sisi tunafahamu kuwa viongozi wana mali, ila ile inayopatikana kinyume ndiyo isiyostahili…kiongozi kuwa na mali si kosa, bali isiyokuwa halali, nia ya uhakiki ni kurudisha uadilifu kwa viongozi, kwani si siri kuwa uadilifu umepotea miongoni mwao,” alisema Jaji Salome.

Hata hivyo, alisema anafanya utafiti kuhusu sheria itakayotenganisha biashara na uongozi, ili iweke usawa kwa walionacho na wasionacho na isiyoogopesha wananchi kama ilivyokuwa sheria ya uhujumu uchumi.

No comments:

Post a Comment