Friday, February 10, 2012

Mbowe- Tumekubali yaishe

MVUTANO wa wabunge kuhusu suala la wakuu wa wilaya kuwepo au kutokuwepo kwenye sheria ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania umekwisha baada ya wabunge kutoka kambi ya upinzani bungeni kukubali yaishe.

Wabunge hao walitoa msimamo huo leo bungeni mjini Dodoma baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuwaomba wakubali kumaliza mvutano huo ulioanza jana bungeni.

Mvutano huo ulianza baada ya Mbunge wa Same mashariki, Anne Kilango Malecela kupendekeza kubadili mapendekezo ya Serikali ya kumweka Mkurugenzi wa Halmashauri na kumuondoa Mkuu wa Wilaya aliyekuwa amewekwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa bungeni Novemba mwaka jana.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amewaeleza wabunge kuwa, ni bahati mbaya kwa Bunge limefika hapo lilipofika.

Mbowe amesema, pamoja na yote yaliyotokea, lazima wabunge wafikie mwafaka na kulieleza Bunge kuwa kambi hiyo imekubali yaishe.

Amesema, wamekubali yaishe kwa misingi ya ndani ya Bunge na kwamba wamelazimika kuyakubali mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ameonya kuwa, utaratibu huo ukiendelea wa kulazimisha mambo bungeni kwa maslahi ya kisiasa ukiendelea utaligharimu Taifa.

“Huu utaratibu wa kufunika kombe mwanaharamu apite utatucost (utatugharimu) kama Taifa” amesema Mbowe na akadai kuwa, mchakato wa kupata Katiba mpya umefanywa wa kisiasa.

Aliwaomba wabunge wa kambi ya Upinzani wakubali yaishe na kusema kuwa Katiba ya nchi ni muhimu kuliko vyama vya siasa na ina uhai mrefu kuliko Chadema au CCM.

Baadhi ya wabunge jana walipinga kuondolewa kwa Mkuu wa Wilaya kwenye mchakato huo, na wengine walitaka Mkurugenzi wa Halmashauri aondolewe kwenye Sheria ya Marekebisho ya Katiba.

Wabunge hao walionesha mitazamo tofauti wakati wanatoa maoni yao kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Katiba uliowasilishwa jana bungeni.

Katika muswada huo, Serikali ilipendekeza kufuta maneno "Mkuu wa Wilaya" yanayoonekana katika kifungu cha 17 (5) (a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na badala yake kuweka maneno ‘ Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mtaa’

Katika muswada huo, Serikali pia ilipendekeza kufuta maneno “Mkuu wa Wilaya” yanaoonekana katika kifungu cha 17 (5) (b) kinachohusu upande wa Zanzibar na kuweka maneno “Mkurugenzi wa Manispaa au Katibu wa Baraza la Mji”

Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM) alisema, Serikali haishinikizi kwamba ni lazima Bunge lipitishe marekebisho hayo, na kwamba, mapendekezo yote katika muswada huo ni ya Serikali, si ya chama chochote.

Alipinga kipengele kinachomuondoa Mkuu wa Wilaya kwenye sheria hiyo, na aliwaomba wabunge waunge mkono pendekezo lake la kutaka kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kwenye sheria hiyo na kumrudisha Mkuu wa Wilaya.

Alisema, DC ndiye mwakilishi wa Rais kwenye eneo analoliongoza, kiongozi wa dola na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hivyo ana mamlaka tofauti na Mkurugenzi wa Wilaya.

Wakati Bunge lilipokaa kama kamati jana jioni, wabunge walishindwa kuafikiana kuhusu suala hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliiagiza Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kukijadili kifungu hicho ili kupata mwafaka.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Anjela Kairuki leo amelieleza Bunge kuwa jana usiku walishauriana na Kilango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wabunge wengine na kufikia mwafaka kwamba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Mkuu wa Wilaya wote wawepo kwenye kifungu cha 17 cha sheria hiyo.

Kairuki amewaeleza wabunge kuwa, Kilango amekubali marekebisho yaliyopendekezwa na Serikali na pia wabunge wa upinzani waliyakubali.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) aliupinga mwafaka huo kwa madai kuwa yataleta mkanganyiko na kwamba, Bunge linatunga sheria mbaya.

“Ili watu fulani waonekane wameshinda kwa kumbeba huyu kada wa CCM, Mkuu wa Wilaya” amesema Lissu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipinga hoja ya Lissu kwa maelezo kwamba, ni muhimu wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri wote wawepo kwenye sheria hiyo kwa kuwa kuna wilaya zina Halmashauri tatu na kwamba, wakuu wa wilaya ni wachache kulinganisha na Halmashauri zilizopo.

Werema leo amesema , yaliyotokea bungeni kuhusu suala hilo yanasikitisha na kwamba, hoja hiyo ni rahisi sana.

No comments:

Post a Comment