Saturday, February 4, 2012
JK akiri hali ni mbaya serikalini
James Magai
RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa katika kipindi hiki Serikali iko katika hali mbaya kifedha kiasi kwamba inashindwa kutekeleza shughuli katika idara mbalimbali kwa wakati. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa salaamu za maadhimisho ya Siku ya Sheria zilizofanyika nje ya Viwanja vya Mahakama Kuu Dar es Salaam. Kauli hiyo ya Kikwete ilitokana na kilio cha Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman kuwa Mahakama nchini imekuwa ikishindwa kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio kutokana na ama kucheleweshewa pesa au kupewa chini ya mahitaji.
Jaji Othman alisema fedha zilizoidhinishwa na Bunge mwaka 2011/2012 kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama ni Sh 20bilioni, lakini katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 31 walitegemea kuwa na Sh 10bilioni, lakini wamepewa Sh6,327,796,972 tu. Akijibu kilio hicho, Rais Kikwete alikiri kuwepo kwa uhaba wa fedha serikalini, lakini akabainisha kuwa hali hiyo imetokana na hatua ya kulipia malimbikizo ya madeni ya nyuma.
“Sehemu kubwa ya mapato ya Serikali katika hii nusu ya kwanza, imetumika kwa ajili ya kulipia malimbikizo ya madeni ya nyuma,” alisema Rais Kikwete bila kufafanua madeni hayo yaliyolipwa na kuongeza kuwa hata wizara nyingine nazo hazikuweza kupewa pesa kama zilivyostahili kwa mara moja. Alisema karibu madeni hayo yatamalizika kulipwa na kwamba mpaka sasa zimebakia kama Sh 40bilioni tu.
Pia Kikwete aliihakikishia Mahakama kuwa ataipatia kiasi chote cha fedha iliyoidhinishwa na Bunge huku akikiri kuwa hata kiasi hicho pia bado ni kidogo. “Itabidi hata tupunguze sehemu nyingine, kuna maeneo mengine wana bajeti ya matrilioni ambazo sidhani kama katika kipindi hiki cha miezi sita zitaweza kuwa zimetumika zote kwa mara moja,” alisema Rais Kikwete.
Jaji Mkuu Othman akifafanua zaidi ucheleweshaji wa pesa za matumizi ya Mahakama alisema kuwa inakuwa ni vigumu kuweza kupata mafanikio ya wazi na kwamba hali hiyo inachangia kukwamisha uendeshaji wa Mahakama.
“Tunashindwa kuwalipa wafanyakazi haki zao wanazostahili kwa sababu ya ukosefu wa stahili za uhamisho, pia inakuwa vigumu kuwahamisha mahakimu na wafanyakazi wengine," alisema.
Hivi sasa kuna mahakimu wa Mahakama za Mwanzo 75 na wafanyakazi wa kada nyingine 500 ambao wamekaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya miaka kumi. Hili linapunguza motisha, ufanisi na tija,” alisema Jaji Othman.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment